Search This Blog

Wednesday, June 22, 2022

BABA YANGU, MAMA YANGU

  


IMEANDIKWA NA IDDI MAKENGO




Mvua kubwa ilikua inanyesha, mimi nilikua ndani chumbani nimejifungia, Baba alijua kuwa nimelala kwakua nilikua nishazima taa tayari. Lakini bado nilikua macho, niliweza kuchungulia katika kona ya dirisha na kama unavyojua mtu ukiwa kwenye giza basi ni rahisi kuona nnje kwani taa ilikua inawaka. Ingawa mvua ilikua inanyesha lakini niliweza kuona kila kitu kilichokua kikiendelea nnje.

Gari ya Baba ilikua imesimama nnje, Mama alikua yuko bize kufunga geti kwani ndiyo alikua katoka kumfungulia. Baada ya kufungua geti Mama alitaka kurudi ndani lakini Baba alidfungua mlango kidogo na kuonekana kama kamuita, Mama alisogelea gari ya Baba, sikusikia walichokua wameongea kwani nilikua mbali na mvua ilikua inanyesha. Lakini nilimuona Baba akimpiga Mama mateke.

Kwanza alimpiga teke la tumbo, mam alipepesuka na kudondoka chini, hakukua na matope kwani nyumba yetu ilikua na nyasi nzuri na sehemu lilipokua gari kulikua na zege. Bila kujali mvua Baba alishuka kwenye gari, alionekana kupepesuka pepesuka, alimfuata Mama pale chini na kuanza kumpoiga mateke, alionekana kuongea kwa hasira, nilimuona namna alivyokua kabadilika kama mnyama, alikua akintyanyua mdomo kwa nguvu ingawa sikusikia chochote.

Mama alikaa chini na kujikunyata huku akizuia tumbao lake, alijikunja sana kuzuia tumbo, sikujua kwanini mpaka baadaye nilipokua mkubwa ndiyo nilikuja kugundua alikua akizuia kupigwa tumboni kwani kipindi hicho ndiyo alikua na ujauzito wa mdogo wangu Rajabu (Sio jina lake halisi). Sikujua walikua wanagombania nini lakini niliogopa sana, Baba alionyesha hasira na alikua akimpiga Mama bila huruma, katika maisha yangu nilikua sijawahi kumuona Baba katika hali ile.

Baba yangu alikua mtu mstaarabu, mswali hina, kipindi hicho nikiwa mtoto wake wa pekee alikua akinipenda sana, hakuwahi kunipiga wala kunifokea na mara nyingi nilikua namuona yeye ni mtu poa kuliko Mama. Mpaka siku hiyo nilikua nampenda Baba yangu kuliko Mama yangu, sikuwahi kumuona akiwa kakasirika, sikuwahi kumuona akimpiga mtu na wala sikuwahi kufikiria kama anaweza kunyanyua mkono na kumpiga mtu yeyote achilia mbali kumpiga Mama.

Alimpiga sana Mama, Mama hakulia wala kupiga kelele, alikua kakaa chini tu kajikunyata, wakati akiendelea kumpiga alishuka Rahma (sio jina lake halisi) huyu nilitambulishwa kama Shangazi. Alikua ni mgeni ambaye alikua kakaa pale nyumbani kwetu kwa kama wiki moja hivi, ingawa ilikua ni mara yangu ya kwanza kumuona lakini Baba aliniambia kuwa ni Shangazi yangu na alikua masomoni simjui. Nilimpenda sana Ant Rahma kwani alikua akiniletea zawadi, alikua akinipenda na mara nyingi alikua akinitembeza sehemu mbalimbali.

Aliposhuka niliona kama anamuinamia Mama na kumuongelesha maneno ambayo pia sikuyasikia. Baada ya kumuongelesha alimsukuma Mama na viatu vyake virefu. Kwanza nilishangaa kwa namna alivyokua amevaa, alikua kavaa kisketi kifupi ambcho kama angeinama basi ungeweza kuona nguo yake ya nadni, alikua kavaa viatu virefu na minywele inaonekana. Nilishangaa kwani kwa kawaida ni mtu wa kuvaa mahijabu na kujitanda.

Sikuelewa kwakweli, usiku ule kila kitu kilikua kigeni kwangu, wakati nikiwa nawaza ni kitu gani kilikua kinaendelea nilimuona Shangazi Rahma akimvamia Baba, walimkumbatia na kuanza kunyonyana ndimi, ingawa nilikua bado binti mdogo nina miaka nane tu lakini nilikua najua wanafanya nini. Nilishaona hayo mambo katika michezo ya kuigiza ya wanaigeria na wazungu hivyo nilijua ni kufanya mapenzi, nilishangaa sana kwani kama yule alikua shangazi inamaanisha ni ndugu wa Baba yangu.

Nilishangaa ni kwanini Baba anapeana mate na Shangazi tena mbele ya Mama. Walishikana kimapenzi na bila aibu Baba alinyanyua kigauni cha Rahma na kutaka kumvua nguo, walitaka kufanyia mapenzi palepale. Wakati huo mvua ilishakata na kulikua na manyunyumanyunyu. Mama kuona vile alinyanyuka na kuwavamia.
“Mume wangu kuna watoto ndani mnataka kufanya nini?” Mama alipiga kelele ambazo nilizisikia, Baba aliacha kufanya alichokua akikifanya na kumvamia Mama.

Alianza tena kumpiga hukua kimuambia asimpangie maisha ile ni nyumba yake na kama hataki kuona kinachoendelea basio aondoke.
“Kwanini unaning’ng’ania, si uondoke!” Baba alipiga kelele. Mama alikua anamuambia amuogope Mungu na kuacha kufanya ushenzi wake mbele yake.
“Si uondoke! Mwanamke umeletewa mwanamke mwingine mpaka ndani lakini hutaki kuondoka! Ondoka tuachie nyumba yetu tufanye mambo yetu kwa uhuru!” Rahma aliongea huku akiwa kama anamsuta Mama.

Mama hakusema chochote, alinyamaza kimya, alianza kutembea kwa shida kuingia ndani lakini Baba alimfuata na kuanza kumpiga tena. Kule ndani nilikua nimechanganyikiwa, kwangu ile ilikua kama sinema, kuna wakati nilijihisi kama vile naota nikaanza kujifinya finya mimi mwenyewe kuona kama niko macho. Sikuwahi kumuona baba namna ile wala sikuwahi kufikiria kuwa anaweza kumpiga Mama, nilitamani kutoka na kuuliza lakini niliogopa sana.

Baba alikua tofauti na kawaida yake, alimpga Mama kama mbwa na baada ya kumaliza kumpiga aliingia ndani na Rahma, walifunga mlango kwa ndani na kumuacha Mama pale nnje. Niliumia sana, mama alitembea mpaka kwenye kibaraza na kujibanza ukutani, kwa sehemu niliyokua sikuweza kumuona tena kwani aliegemea ukuta, nilikaa pale dirishani mpaka nilipopitiwa na usingizi nikalala.

***

Kutokana na kukesha usiku asubuhi nililala sana, ulikua ni wakati wa likizo hivyo hakukua na shule, siku hiyo Mama hakutaka hata kuniamsha mapema. Nilikuja kuamshwa asubuhi kwenye saa tatu hivi na Dada (Mfanyakazi wetu wa ndani).
“Njoo umuage Shangazi aonaondoka, Baba anakuita!” Aliniambia, nilijikuta nanyanyuka harakaharaka kwenda kumuona Shangazi, alinichangamkia sana na kuniahidi kurudi tena, ingawa ilikua ni siku ya kazi lakini Baba alikuepo.

Alionekana kuja kumsindikiza Shangazi.
“Mama yuko wapi?” Nilijikuta nauliza, bado nilijihisi kama niko ndotoni, mambo ya jana yake sikuyaona kama mambo halisia, nilijihisi nimeota kitu kibaya. Wakatiwanaongeana Rahma kujiongelesha kama mtu mwema mimi kichwa changu kilikua kikizunguka mambo ya jana.
“Bado ana usingizi huyu, kwanini umemuacha akalala mpaka sasa hivi?” Baba aliongea bila kujibu swali langu, nilikua kimya sana kama nimeshikwa na bumbuwazi.

Rahma alijiongelesha ongelesha na kuondoka na Baba, sikujua ameenda wapi na wala sikujali.
“Jana usiku mvua ilinyesha?” Nilimuuliza dada, bado nilikua na wenge la usingizi, akili yangu ilikua haijakubali kama Baba anaweza kumpiga Mama.
“Mimi sijui nilikua nimelala lakini nnje majani yameloa, itakua ilinyesha. Kwanini unauliza?” Dada alinijibu, sikua na jibu kamili hivyo nilinyamaza tu kimya.

Nilirudi chumbani kwangu nikiwa sina raha kabisa, kuna mambo mawili yalikua yananichanganya, moja ni kwa Baba kumpiga Mama na jingine ni kwa Baba kukumbatiana na kulana mate mwanamke mwingine ambaye nilimjua kama Shangazi. Siku ile ilikua ndefu sana, sikua na amani mpaka jioni, Mama ndiyo alitangulia kurudi kutoka kazini, nilimsalimia kwa kumkumbatia huku nikimkagua kagua kuona kama vile kaumia.

Alijitahidi kucheka ingawa nilimuona kabisa hayuko sawa.
“Una nini wewe mbona unaniangalia hivyo? Nimebadilika?” Aliniuliza, sikua na jibu, bado nilikua sina uhakika na kitu nilichokiona jana yake hivyo sikuongea chochote. Baadaye Baba alikuja, walisalimiana vizuri tena kwa kukumbatiana, kama kawaida Baba aliniletea zawadi, nilizipokea lakini sikua na Bashasha, akili yangu bado ilikua inawaza mambo ya jana yake, ingawa sikutaka kuamini lakini nilimuogopa sana Baba.

Niliingia ndani nikiwa na mawazo sana, kwa kawaida Baba si mtu wa kutoka sana, mara nyingi anakua nyumbani akinisaidia homework na kunibembeleza mapaka kulala, mara nyingi anakuja chumbani kwangu kunisomea hadithi na huwa tunacheza pamoja. Kama kawaida siku hiyo alikuja, lakini sikutaka kuongea naye hivyo niolivyomsikia tu anafungua mlango nilipenda kitandani, nikafunga macho na kujifanya kulala.

Alisimama kwa muda wa kama dakika mbili kisha akatoka na kufunga mlango, nilipoona katoka nilitembea mpaka mlangoni kumchungulia.
“Asha (si jina lake halisi) atakua anaumwa, leo kutwa naizma hana raha kabisa, sijui ana nini ila namuona kaingia kalala.” Baba alimuambia Mama ambaye alikua kakaa kwenye kochi anaangalia TV.
“Sijui, ngoja nitamuangalia ana nini?” Mama aliongea lakini Baba alimkataza akimuambia hataki nisumbuliwe kwani nishalala.

Nilimuona Mama akinyong’onyea, ukimya ulitawala kidogo, nilirudi ndani kulala, kichwani nilikua na mawazo mengi tu, nilikua na maswali mengi kuliko majibu. Niliwaza mpaka kupitiwa na usingizi. Nyumba ilikua na amani kwa muda mrefu, furaha ilirejea, sikuwahi kumuona Baba akimpiga au kumkasirikia tena Mama, kuna wakati niliamini kabisa labda nilikua naota kwani kila mtu alikua na amanai na sikuona kitu chochote kibaya.

Siku moja nakumbuka nilikua kwenye gari, ilikua ni wiki moja kabla ya kufungua shule, zilishapita zaidi ya wiki tatu tyangu kile kitendo kutokea. Nilikua nimekaa siti ya nyuma nimelala, tulikua tunatokea kijijini kwa bibi ambapo nilipelekwa kusalimia.
“Unajua tunatakiwa kutoa ada angalau nusu?” Nilimsikia Mama akisema. Usingizi ulikua unakuja na kurudi lakini wao alijua kuwa nimelala.
“Kwahiyo? Si utoe unaniambia nini?” Baba alijibu kwa hasira, aliongea kwa sauti ya juu kiasi cha kunishtua, lakini sijui kwanini, sikushtuka, niliendelea kufunga macho ili kusikiliza, nadhani umbea ulikua unanisumbua.

“Sina pesa mume wangu, mwaka jana uliniambia hivyo hivyo nitoe, nikachukua mkopo lakini hukulipa, hapa nadaiwa, mshahara wangu nakatwa deni la nyumba na sasa hivi natakiwa tena kumtumia mdogo wangu kaosa mkopo chuo, nisaidie mume wangu…” Mama aliongea kwa kulalamika.
“Kwahiyo ndugu zako unaona ni wamhuhumu sana kuliko mwanao! Mimi sina pesa na kama hutaki asome muache abaki nyumbani, wewe si unasomesha ndugu zako, waache wasome wakati wakwako anabaki nyumbani!”

Bbaa aliongea kwa hasira, Mama alikaa kimya kwa muda wa kama dakika tano, kule ndani ya gari kila kitu kilikua kimya kimetulia mpaka Mama alipoongea tena.
“Lakini wewe mshahara wako unaenda wapi? Hutoi pesa ya chakula, nyumba nimejenga mimi, mavazi mimi na hata ada ya…” Mama aliongea lakini kabla ya kumalizia Baba ambaye alikua ndiyo anaendesha gari alichukua simu yake ambayo ilikua kwenye dashboard na kuirusha, ilimpiga Mama kwenye pua.

“Mshenzi mkubwa wewe! Mimi ni nani kwako unaanza kunihesabia vitu unavyovifanya ndani ya nyumba yangu! pumbavu Malaya mkubwa wewe!” Baba aliongea kwa hasira, simu ilimpiga Mama puani, alipiga kelele moja tu “Nakufaaaa!” Baba alikua kama kachanganyikiwa, aliacha usukani na kumrushia ngumi Mama, ya uso, alionekana kukasirika zaidi. wakati anafanya hivyo gari ilianza kuyumba, kwakua tulikua kwenye mwendo kasi, ilipoteza uelekeo na kuacha barabara. “Nakufaaaa! Nilipiga kelele nilipoona mti mkubwa uliokua mbele yetu na gari ilikua ikiufuata!”



Kila kitu kilikua kinatokea haraka lakini nilikiona, pamoja na umri wangu mdogo lakini ile picha iliendelea kubaki kichwani kwangu mpaka sasa. Baba aliuona ule mti, alijaribu kuukwepa gari ikawa inaenda kama kuugonga kwa upende wake, lakini ghfla nilimuona akigeuza usukani na kuligeuza na kuugonga ule mtu kwa uapende wa Mama. Nilisikia kishindo kikubwa na baada ya hapo sikuelewa ni kitu gani kingine kilikua kimetokea.

“Hajaumia popote, naona kama ni mshituko tu, hajazindika lakini viungo vyake viko salaama, atazinduka, havuji damu kwa ndani….” Nilisikia sauti nzito ambayo sikuielewa, nilikua katika usingizi mzito, mwili ulikua umechoka na nilijaribu sana kugumbua amcho lakini hayakufunguka. Mara nilisikia mtu ananishika mkono, hakusema chohote lakini alionekana kukaa pembeni yangu, nilijitahidi sana kufungua macho yangu, alikua ni Baba, alikua mzima kabisa kakaa pembeni yangu.

Kulikua na watu wengine wengine pale chumbani lakini kwa sasa siwakumbuki, walikuja kunisalimia. Nilipepesa macho nikijaribu kuwaza kilichokua kimetokea. Nilijitahidi kunyanyuka lakiniBaba alinishika, alinirudisha kulala.
“Pumzika kwanza…” Aliniambia kwa kunibembeleza, mikono yake ilikua usoni kwangu aliniuliza maswali maswali namna nilivyokua nikijisikia, mimi nilibaki kimya nikishangaa, bado nilikua sijazinduka vizuri, lakini taratibu picha ya lile tukio ilianza kuja kichwani kwangu.

Niliiona ile ajali kama ndiyo kwanza ilikua inatokea, niliona namna ambavyo Baba alimpiga Mama na kisha kuanza kugombana mpaka alipoligongeshea gari kwenye mti.
“Muache Mama! Muache Mama! Usimuue!” Nilijikuta napiga kelele huku nikimpiga makofi Baba, nilijitoa katika mikono yake na kujirusharusha, nilipoga kelele nyinyi lakini yeye hakupaniki, alinishikilia chini na kuniambia nipumzike ni mshituko wa ajali lakini nitakua salama.

Nilijaribu kujitoa mikononi mwake lakini nilishindwa, nilipiga kelele sana mpaka nikachoka, baadaye nilituliamwenyewe, aliwaomba watu waliokua mule ndani kutoka na kunaicha nipumzike. Alitoka na kuniacha mwenyewe, alikaa nnje kwa muda kidogo kisha akarudi, alikua na chakula na alitaka kunilisha, tayari akili yangu ilishaanza kukaa sawa na nilijua nini kilikua kimetokea.
“Mama yuko wapi?” nilimuuliza baada ya kuingia, alijaribu kubadilisha mada lakini sikumruhuhusu, bado nilikazania kujua alipokua Mama yangu.

“Yuko chumba kingine, anaendelea vizuri.” Aliniambia hukua kikaa pembeni yangu na uji mkononi.
“Nataka kumuona…” nilimuambia, alikataa na kuniambia kuwa nile kwanza kama natataka kuonana na Mama yangu. nilijaribu kubisha lakini huo ndiyo ulikua ni msimamo wake, aliniambia kama nataka kumuona Mama basi nile chakula kwanza, alijaribu kunibembeleza, kunichekea lakini kila nikimuangalia sikuona tena picha ya Baba wa zamani, nilimuona Baba mpya ambaye alikua anampiga Mama na kugongesha gari upande wa Mama.

Nilikula harakaharaka, nilikua najisikia vizuri na baada ya kumaliza kula niliweza kunyanyuka, alinisaidia kunishika akidhani labda nilikua nimeumia lakini sikua nimeumia popote, sikupata hata mchubuko, kama alivyokua Baba mimi nilitoka salama kwani nilikua katika siti yangu nimefunga mkanda lakini pia nilikua ule upande wa Baba hivyo sikuumia popote. Nilitaka kwenda kumuona Mama lakini alinikatalia.

Kwa namna alivyokua anakataa nilijua lazima kuna kitu kibaya kimetokea, moja kwa moja nilihisi Mama amekufa, nilianza kupiga kelele na kumlaumu yeye kwa kumuua Mama yangu, alijaribu kunisihi kwa kuniambia kuwa Mama yuko salama na hajafa lakini sikumuamini, nilihisi ananidanganya na kumuambia kama kweli yuko salama basi anipeleke kumuona. Kwa namna nilivyokua nikisumbua hakua na namna, aliniambia twende kumuona Mama.

Alinipeleka mpaka kwenye chumba kimoja, hapo niliona watu wamekaa nnje, wengi nilikua nawafahamu, kulikua na Shangazi zangu, Mama zangu wadogo na ndugu wengine wengi wengi.
“Kaaa hapa, Mama yako yuko huko ndani kwenye chumba cha upasuaaji,a lipata ajali na wote tunasubiria.” Aliniambia, sikua naelewa kitu nilitaka tu kumuona Mama, nilipiga kelele mpaka kulazimika kuondolewa pale, nilirudishwa chumbani na kuchomwa sindano moja nikalala.

***

Nilikua nimetoka likizo kwa Bibi, pamoja na kwamba nilikua nasoma day lakini baada ya ile ajali nilihamishiwa bweni. Siku ile nilipozinduka nilikua nimetulia kidogo, mama alishatoka katika chumba cha upasuaji na niliruhusiwa kumuona, alikua kalala kitandani haongei chochote zaidi ya kupepesa macho kuniangalia, hapo ndipo nilijua kuwa Mama yangu yupo hai. Hakuonekana kuumia sehemu yoyote, usuo ulikua hauna michubuko mingi, alivimba kidogo na bandeji kidogo.

“Mama yako huyo hapo, anaendelea vizuri hivyo kama unataka apone basi usimsumbue, muacha apumzike.” Baba aliniambia kwa upole, sijui ni nini lakini nilimuelewa, siku hiyo ndiyo akili zangu zilianza kuwa za mtu mzima. Lakini pia siku hiyo ndiyo ilikua mara yangu ya mwisho kumuona Mama hospitalini, nilirudi nyumbani na huko Baba aliniambia natakiwa kwenda bweni. Nililia sana na kugoma lakini alikataa, nakumbuka nilikua naingia darasa la nne na Baba alitumia kisingizio cha mtihani wa taifa kwa mimi kwenda kukaa bweni.

Nilitaka kwenda kumuona Mama lakini alikataa, aliniambia Mama ni mgonjwa na haruhusiwi kuoanana na watu. Nakumbuka nilisoma kwa bidii nikisubiria likizo ili kwenda kumuona Mama, lakini ilipofika nilipelekwa kijijini, wakati huo Mama alikua kashapona na niliweza kuongea naye kwenye simu, alikua anaongea vizuri tu na niliambiwa kuwa nina mdogo wangu wa kiume. Nilikua na hamu sana ya kumuona na kumjua lakini nilipigwa tarehe mpaka likizo ya mwezi wa kumi na mbili, kipindi naingia darasa la tano.

Walitaka kunipeleka kijijini kwa bibi lakini nilikataa, nililia sana mpaka nikaruhusiwa kwenda kumuona Mama.nilichokiona kilinishangaza sana, Mama alikua kakaa kwenye kiti, kapooza kuanzia kiunoni kushika chini, mikono yake nayo ilikua haifanyi kazi vizuri, ilikua inanyanyuka kwa shida hivyo kila kitu alikua ni mtu wa kufanyiwa. Alikua anaongea vizuri lakini alionekana kuwa katika maumivu makali, alijitahidi sana kutokunionyesha kuwa anaumia au anaumwa lakini ukweli nikuwa alikua katika hali mbaya.

Mdogo wangu ambaye wakati huo alikua na kama miezi sita kama sijakosea alikua haishi na Mama, alishachukuliwa na Shangazi na yeye ndiyo alienda kumlea, nilienda kumuona na nilifurahi sana kua na mimi nilikua na mdogo wangu. kitu kilichoniumiza sana ni hali ya Mama, si hali ya ugonjwa bali hali yake ya kiafya, alikua kakonda sana, alionekana kama mtu mwenye mawazo, kulikua na dada wa kazi pale nyumbani kwaajili ya kumhudumia lakini ni kama vile hakuepio.

Mama alikua mchafu, nguo zinanuka, alikua hawezi kufanya chochote hivyo mara nyingi alikua anajisaidia hapohapo kwenye kiti chake na kuja kusafishwa baadaye, lakini hakukua na mtu wa kumsafisha na huyo dada wa kazi naye aliku akimntukana na kumlalamikia kwani alikua halipwi vizuri. Baba alikua si mtu wa kukaa nyumbani na hata akikaa alikua hakai chumba kimoja na Mama, kipindi nipo alijitahidi kuigiza ili mimi kumuona kama Baba bora lakini alishindwa.

Niliumia sana kumuona Mama katika hali ile, alikua ni mtu wa mawazo, mtu wa kufungiwa ndani, dada wa kazi akiwa na mizunguko yake angeweza kumfungia Mama ndani kwa kutwa nzima bila hata kumpa chakula, kwakua Baba naye alikua hajali anaweza kukaa hata wiki bila kurudi nyumbani basi dada alifanya kile anachojisikia bila kujali kama kuna mtu atajua au atapoteza kazi. Hakua anapika kwa wakati na suala la kumbadilisha nguo ilikua mtihani.

“Nani wakufua kila saa mtu mwenyewe atakuja kujinyea tu, bora ayakusanye nikija nafua jumla.” Alikua anapenda kuongea mara kwa mara. Hali ile iliniumiza sana, Mama alikua hajiwezi hata kulishwa alihitaji kulishwa lakini angeweza kukaa kutwa nzima na njaa bila kupata mtu wa kumhudumia. nililazimika kubeba jukumu la kumhudumia Mama, kitu ambacho nilikua siwezi ilikua ni kumsafisha kwania likua ni mzito sana, lakini kwa hali yake ileile alijitahidi kujinyanyua na kujigeuza na wakati mwingine nililazimika kutoka kwenda kuomba watu nnje wanisaidie kumnyanyua.

Wakati wa kurudi shule ulipowadia nilikataa kabisa kwenda bweni, nilimuambia Baba nataka kubaki na Mama ili kumsaidia, Baba alaijaribu kunibembeleza lakini sikukubali. Nilimuambia kama hanirudishi nyumbani basi sitasoma kabisa, alikasirika sana na kunitukana, Baba yangu ananipenda na katika maisha yake alikua hajawahi kunikaripia wala kunipiga lakini siku hiyo alikasirika na kuniambia kuwa nitaenda shule na kunipiga makofi, nilikataa na kumuambia kuwa sitaenda nitakaa na Mama! Tena nilizidisha zaidi kwa kumuambia kuwa yeye ndiyo kasababisha Mama kuwa vile.

Nilimuona Baba akikiasirika zaidi, alivimba na kutaka kunipiga lakini alijizuia, alikua akikaa na kusimama ara kwa mara, kwa namna alivyokua niliogopa, lakini na mimi hasira zilishanipanda, sikua tayari kumsikiliza, nilimuambia kabisa siwezi kwenda shule kwani Mama anateseka. Baada ya kuona kuwa hawezi kunishawishi na kunibadilisha msimamo wangu aliamua kunywea, akakubalia na kuniambia kuwa nitakaa nyumbani atanitafutia uhamisho.

Aliniomba msamaha kwa kunikaripia na kunipiga akiniambia kuwa haitakuja kutokea tena, nilimuelewa. Mimi nina chumba changu lakini kutokana na hali ya Mama nilikua nalala naye chumbani kwake alipokua katelekezwa kwa Baba, kwakua mara nyingi Baba alikua halali nyumbani na siku akiwepo basi nalala chumbani kwangu hakua akilijua hilo. Usiku ule nilikua chumbani kwangu, nikijua kuwa Baba hajarudi kwani sikuiona gari yake niliamua kwenda chumbani kwa Mama kumpa kampani,.

Nilitembea mpaka chumbani kwa Mama, lakini ile nafika mlangoni nilisikia sauti ya Baba ikiongea taratibu.
“Nitakuua! Yaani nimekuweka hapa sijataka kukuacha kwakua watu wataniona mnyama lakini leo unataka kumgeuza mwanangu ili anichukie, umemuambia nini mwanangu!” Baba alikua akiuliza, nilimsikia Mama akikohoa kama vile anataka kuongea kitu lakini hawezi, ilikua kama vile anakabwa, sijui nilipata wapi ujasiri lakini niliusukuma mlango kwa nguvu nikigonga na kupiga kelele ili Baba aufungue kwani ulikua umefungwa kwa ndani.

Baba ambaye alikua anajua kuwa nimelala alikurupuka na kufungua mlango, taa ilikua imezimwa, alinipiga kikumbo pale mlangoni na kutoka kukimbia, sikumjali, niliingia ndani na kuwasha taa ili kumuangalia Mama. Nilimsogelea alikua hatingishiki wala nini, nilichanganyikiwa nikafanya kama watu wa kwenye TV kumuangalia mapigo yake ya moyo, hakukua na kitu, Mama alikua katulia tuli kitandani.

Kama hukusoma sehemu ya kwanza ya simulizi hii basi fuatilia katika ukursa wangu wa Instagram Azirani Magazine ambapo utapata sehemu ya kwanza pamoja na muendelezo wa sehemu ya tatu.



Nilianza kumsukuma Mama ili atingishike lakini hakutingishika, sijui wazo lilikuja wapi nilimnyanyua kichwa kwa juu kidogo na kuanza kumtingisha huku nikimbonyeza kifuani, ghafla alianza kukohoa, alikohoa sana kama anatafuta pumzi.
“Baba alikua anataka kukuua kama kwenye gari!” Niliongea kwa hasira baada ya kuona kuwa kashaakaa sawa, aliniangalia kwa uchungu, macho yalikua mekundu sana kama vile alikua analia kutwa nzima ingawa alikua halii. Nilirudia tena maneno yangu nakumalizia kuwa namchukia Baba.

“Hapana mwanangu, hakua anataka kuniua, Baba yako ananipenda sana na anakupenda, sana, ile ilikua ni ajali na hapa tulikua tunacheza tu, hakua anataka kuniua….” Mama alijaribu kumtetee, nilipendwa na hasira na kutaka hata kumukuma au kumpiga makofi, lakini nikiangalia macho yaek nilimuonea huruma, hakua akilia lakini machozi yalikua yakimtoka, alijaribu kunyanyua mukono yake isiyokua na nguvu ili kunifuta machozo lakini alishindwa.

Nililazimika kumfuta mimi machozi, sikuongea chochote kwani nilikua na hasira na niliona kabisa kuwa Mama anaumia.
“Mwanangu usije kumchukia Baba yako hata siku moja, mimi nayeye tunaweza kugombana lakini bado ataendelea kubaki kuwa Baba yako, kamwe usije kumchukia wala kumkosea heshima…”
“Lakini mama…”
“Hakuna cha lakini, yule ni Baba yako, anakupenda sana na anakujali, ni lazima kumsikiliza kwa kila kitu, mambonyote anayofanya ni kwaajili yako, wewe na mdogo wako, anafanya kwakua anakupenda ndiyo maana nataka uende shule…”

Aliongea kwa kujilazimisha lakini alishindwa kumalizia, machozi yalianza kumtoka tena nikalazimika kumfuta.
“Mama nikienda wewe utabaki na nani hapa?” Nilimuuliza, alikaa kimya kwa muda kisha akaniambia.
“Kuna mfanyakazi, si kazi yako kunihudumia, wewe bado mtoto mdogo, hutakiwi kubeba haya majukumu, nenda kasome kapate elimu, utakuja kuisaidia familia yako, una mdogo wako wa kumuangalia, sitakua na amani nikijua kuwa husomi kwaajili yangu. nataka ubaki shuleni, msikilize Baba yako rudi ukasome.”

Alikua katika maumivu makali, si maumivu tu ya matendo aliyokua akifanyiwa lakini pia alikua katika maumivu ya kimwili.
“Mama una nini, mbona unakua hivyo….” Nilimuuliza baada ya kuona kama anapumua kwa shida, kabla ya kunijibu niliona pua zake zinatoa damu. Hazikua damu nyingi lakini ilionekana kama kuna kitu kimepasuka kwa ndani.
“Mbona pua zinatoa damu, vipi zinauma?” Nilimuuliza, alitingisha kichwa kusema hapana lakini nilijua kabisa anaumia, akili yangu ilitaka kumpeleka hospitalini lakini ningempelekaje.

Nilitoka kule chumbani na kumfuata Dada wa kazi, nilimuambia kuhusu Mama na kumuambia kuwa ntunatakiw akumpeleka hospitalini.
“Una hela wewe?” Aliniuliza. Nilimjibu sina, aliniambia hata yeye hana na hawezi kuhangaika na Mama, alianza kulalamika mambo mengi akisema kuwa hawezi kujihangaisha kwakua hata kumlipa hawamlipi hivyo anakaa pale kwakua ana mipango yake na ikikamlika anaondoka.

“Ningekua na pakuishi ningekua nishaondoka muda mrefu!” Aliongea hukua kiwasha TV kuangalia, hakujali chochote. Nilitoka na kurudi nyumbani kwa Mama, alikua kafunga macho kama vile kalal, niligopa sana, tangu ile ajali huwa naogopa sana, nikiona mtu kalala hata kipindi niko shuleni nilikua namuangalia mara mbili kuona kama yuko hai au la. Nilimkimbilia Mama na kumuamsha kumuangalia kama yuko hai, alinyanyuka na kuniambia kuwa anajisikia vizuri nisihangaike nimuache alale.

Pamoja na kusema hivyo lakini hakua akiendelea vizuri, nilimuambia niende kuamsha majirani alikataa katakata na kuniambia yeye yuko vizuri. Sikua na namna zaidi ya kulala pembeni yake, nilipitiwa na usingizi mpaka asubuhi, Mama ndiyo alikua mtu wa kwanza kuamka, niliamka na kwenda kumfuata dada ili kuandaa chai lakini hakuepo, nilikagua chumba chake na kukuta kuwa ameshachukua kila kitu chake, nilikuja kumuambia Mama, hakuonekana kushtuka.

“Mwanangtu hata kama ni mimi nisingekaa, ana zaidi ya miezi sita hajalipwa pesa yake…” Mama aliongea kwa uchungu, nilimuangalia na kumuambia kuwa siwezi kwenda shule tena. Alinisihi na kunibembeleza lakini nilimuambia hapana. “Nikiondoka hapa Mama utakufa, Najua Baba hatoi chakula nikiwa sipo, lakimi mimi ananipenda hawezi kuniacha nife njaa, namjua, nikiondoka ukabaki peke yako basi atakuacha ufe humu ndani lakini mimi nikiwa nipo hawezi kukufanya chochote, najua ananipenda na anaogopa nikimchukia, nitabaki kukulinda.”

****
Baba yangu alikua ananipenda kuliko kitu kingine chochote kile, kila wakati alikua akijaribu kunifanyia mambo ili kuniridhisha, alitaka nimuone Baba mwema, hakutaka nijue namna alivyokua akimnyanyasa Mama. Nilikuja kugundua mateso aliyokua akipitria Mama baada ya kuanza kumhudumia. Alikua na makovu mengi sana mgongoni na kwenye mapaja, alikua kachanywa na viwembe mgongoni na alikua kachomwa na pasi kwenye mapaja.

Ingawa Mama hakuwahi kunielezea wala kuniambia kilichokua kimetokea lakini nilikua na akili zangu, nilikua naona na nilijua kuwa yale yalikua ni mateso aliyokua akiyapata kutoka kwa Baba. Kila siku mama alinisisitiza kumpenda Baba, alikua akisingizia ajali kuwa kapata yale makovu kwa ajali lakini wapi! Nilishajua sababu na sikudanganyika, mara kadhaa nilijifanya mjinga kumuamini ili ajisikie vizuri lakini moyoni nilijua kabisa kuwa Baba yangu ni mshenzi wa kutupwa.

Nilimuambia Baba sitaenda bweni na kama akilazimisha basi aje kuchukua maiti shuleni, nilikua namaanisha na kweli alikubali nibaki kutwa kumhudumia Mama. Ingawa nilijaribu sana kumpenda lakini baada ya kugundua ushenzi wake kila kitu kilibadilika, tulianza kuwa kama paka na panya, sikua nikimheshimu tena kama Baba na hata alipokua akiniletea zawadi nililazimisha tu kuzipokea na kucheka lakini sikua na furaha kabisa.

Maisha yaliendelea hivyo hivyo, Baba liatafuta mfanyakazi mwingine lakini nilijua kabisa hakutafuta kwaajili ya Mama bali kwaajili yangu. Alitafuta mtoto mdogo kabisa, ingawa kiumri alikua mkubwa kwangu lakini kiumbo nilimzidi na alionekana dhaifu, singeweza klumsogeza Mama. Pale nyumbani Baba alikua anakuja mara moja moja, sijui alikua anaishi wapi kwani hata Anti Rahma aliyekua akiishi kwake mwanzoni walishaachana na alishaolewa.

Alikua anaweza kuja kukaa siku mbili na kuondoka wiki bila kurudi nyumbani, hakua akileta tena marafiki zake na hakukua na ndugu aliyekua anakuja kumuangalia Mama. Kwakifupi ni kama tulikua tumetegwa na nilijua fika Baba anatamani kumfukuza Mama ila anaogopa nitaondoka naye kitu ambacho alikua hakipendi. Niliendelea na masomo mpaka nilipofika darasa la saba, nilijitahidi sana kufanya vizuri darasani ili kupata zawadi kutoka kwa Baba na kuziweka kwaajili ya Mama.

Kama kawaida yangu sikuwahi hata kushika namba mbili darasani, pamoja na hali ngumu ya pale nyumbani lakini nilijitahidi sana katika masomo. Kila siku Mama alinisisitiza kusoma na kusoma ili nije kuwa na maisha yangu. kweli nilifanya hivyo, mpaka namaliza chuo nilikua sina mawasiliano mazuri na Baba, hali yake ya maisha ilianza kubadilika baada ya mimi kumaliza chuo na kupata kazi.

Alikua ni mtu wa kuumwaumwa ndipo ilikuja kugundulika kuwa alikuakaarthirika, alirudi pale nyumbani ambapo mpaka leo Mama anamhudumia, baada ya mambo yake kuwa mabayahakuna ndugu hata mmoja alitaka kumsikia Baba, sasa hivi tuna maisha mazuri, nawahudumia wazazi wangu, kuna wakati nikikumbuka mambo aliyomfanyia Mama nakua na hasira lakini Mama ananituliza na kuniambia, pamoja na yote huyu ni Baba yako, yaani nashindwa kuelewa Mama ana moyo wa namna gani kumsamehe na kuendelea kuishi na mwanaume kama Baba ila sina chakuingilia, nwahudumia wote vizuri kwani ni wazazi wangu.

MWISHO 

0 comments:

Post a Comment

BLOG