IMEANDIKWA NA IDDI MAKENGO
SIMULIZI; BABA MIKONO YANGU ITAOTA LINI!
Mke wangu alinipigia simu na kuniambia kuwa anataka kuja kumchukua mtoto, niliikata na kumuambia kama akikanyaga kwangu basi atajua mimi ni nani? Nilimtishia na kumuambia kuwa hawezi kuwagusa wanangu kwani kwa kitu alichokua amenifanyia sikutaka hata kumuona. Nakumbuka ilikua siku ya Jumamosi, nilikua nimejikalia tu nyumbani, nikitegemea kutulia na familia yangu mke wangu aliniaga kuwa anatoka.
JOIN US ON TELEGRAM
Aliniambia anenda kuonana na Shangazi yake ambaye alikua anamsindikiza sehemu, sikujali sana kwani kutoka lilikua ni jambo la kawaida. Lakini wakati anajiandaa simu yake iliita, kwakawaida hatushikiani simu, alikua bafuni hivyo hakuisikia, niliiacha mpaka ikakatika, lakini iliita tena kwa mara ya pili, jina lilikua ni Shangazi, kwakua nilijua wama miadi naye niliamua kuipokea ili kumuambia kuwa yuko bafuni.
Nilipokea na kuanza kwa kusema “Hallooo!” kisha nikasalimia, lakini ghafla upande wa pili wa simu ulikua kimya, hakukua na kitu, niliita na kuita ndipo niligundua kuwa simu ilishakatwa. Nilijua labda hakua na salio alikua anambeep hivyo nilichukua ile namba na kuipiga kwa simu yangu (sikuwa na namba ya Shangazi yake). Ilipokelewa, nilishtuka kusikia sauti ya kiume ikisema “Haloo!”
Nilimsalimia na kujifanya kukosea namba. Wakati huo mke wangu alikua anatoka bafuni, nilimpa simu yake na kumuambia ajiandae harakaharaka kwani Shangazi alikua aigia. Alishtuka kidogo, akaichukua simu na kuanza kuangalia “Ulipokea?” Aliniuliza. “Ndiyo lakini hakuongea chochote, labda alikua hana salio unaweza kumpigia umuambie unaenda…” Niliongea kwa utulivu, sikutaka kuonyesha kupaniki ingawa nilikua nawaza huyo Shangazi ni yupi.
Nilimchukua mwanangu mdogo na kumuaga mke wangu, nilimuambia natoka natembea tembea kwenda kwa rafiki yangu mmoja, aliniitikia sawa, nilitoka lakini sikwenda mbali. Nilitembea hatua kadhaa na kwenda kukaa katika duka moja hivi pembeni ya barabara, sehemu ambayo nilikua naiona nyumba yetu, niliangalia mpaka nilipomuona mke wangu akitoka na gari, kuna kijana alikua pale pembeni.
“Mpeleke huyu nyumbani…” Nilimuambia huku nikimkabidhi mtoto, ni kijana wa jirani, nilitoka pale na kuchukua Bajaji na kumuambia alifuate Gari la mke wangu. Lilikua ni gari langu ambalo tulikua tukitumia wote mimi na mke wangu, alilifuata mpaka katika nyumba moja ya kulala wageni ambayo haikua mbali sana na nyumbani, kama mtaa wa tatu hivi. Mke wangu aliingiza gari ndani, niliendelea kubaki pale kwenye Bajaji kuangalia.
Baada ya kama dakika kumi hivi mtu mmoja aliingia, hakua mgeni sana kwangu, nilimfahamu kupitia moja ya picha za mke wangu za zamani. Alikua ni X wake, mwanaume ambaye waliachana kabla ya mimi kukutana naye, nilimkumbuka kwani kuna wakati alimuomba urafiki Facebook na wakawa wanatumiana meseji za ajabu ajabu wakikumbushiana mambo ya zamani, mke wangu alidhani anafanya siri.
Lakini alisahau kuwa ingawa alibadilisha Password ya akaunti yake ya Facebook lakini alisahau ile ya email address yake ambayo mimi ndiyo nilimtengenezea hivyo kila mara walipokua wakitumiana meseji zilikua zikiingia pia kwenye email na nilikua naziona. Mwanzoni walikua wanachat tukawaida lakini baadaye mwanaume alianza kujifanya ana matatizo katika ndoa yake, mkewe ni msumbufu na ujinga ujinga kama huo.
Kama mwanaume nilijua hiyo gia kwani rafiki zangu wengi wanaitumia, kwakua nilikua nampenda sana mke wangu sikutaka kusubiri anisaliti kwanza ndiyo nimuambie, nilimuambia kila kitu na kumuonya kuendelea kuwasiliana na huyo mwanaume. “Sina kitu cha kukusamehe kwasasa lakini siku nyingine nikija kugundua kama mnawasiliana naye hata kama kalazwa hospitalini mahuituti nitajua umemchagua yeye na nitakuacha!” Nilimuambia mke wangu na alionyesha kunielewa.
Sikutaka kumfuatilia tena, sikuona tena meseji zao za kuchat na kwakua nilikua nampenda sana mke wangu niliamua kumuamini kwani nilijua atafanya kitu sahihi. Kweli hakunionyesha dalili za kuendelea kuwasiliana naye au kuchepuka mpaka siku hiyo, nilipomuona yule mtu hasira zilinipanda, nilitamani kwenda kuwafurumua kabla ya kufanya chochote lakini niliwaza inawezekana haikua mara ya kwanza wao kukutaka hivyo isingesaidia.
Nilitoa noti tatu za Shilingi elfu kumi kumi na kumpa Dereva Bajaji, nilimuambia nataka asubiri na mimi na anifuate ninapokwenda. “Usiniruhusu kufanya kitu kibaya.” Nilimuambia alikua kijana lakini alishaelewa nini kilikua kinaendelea, aliitikia kwa kichwa kisha bila kusema chochote, nilisubiri pale kwenye Bajaji kwa muda wa kama nusu saa hivi kisha nikaenda katika ile nyumba ya kulala wa geni.
Nilijitambulisha kisha kumuambia mhudumu kuwa mke wangu yuko humo ndani kaingia na mwanaume hivyo nilimtaka kunipeleka katika chumba walipo. Alitaka kuleta ubishi lakini nilimuangalia kwa jicho ambalo alinywea, nilimuelekeza namna alivyokua amevaa, aliniomba amuite meneja nikamuambia hatanyanyua mguu pale nahitaji kwenda kumuona mke wangu. Huku binti wa watu akitetemeka alinipeleka mpaka kwenye chumba wachokua mke wangu na mchepuko wake.
Aligonga kuomba kufunguliwa walipomuuliza shida niliinama na kumuambia waambie kuna shoti ya umeme na inatokea kwenu umekuja na fundi. Aliwaambia na kweli walifungua, mke wangu alikua kitandani kajifunika shuka, yule mwanaume yeye alikua kafunga taulo. Nilimuangalia mke wangu ambaye alikua kaloa jasho, cha kushangaza badala ya kupandwa na hasira nilijisikia kinyaa kabisa, nilimuangalia kwa karibu dakika tano bila kusema chochote, wote tulikua kimya.
SIMULIZI; BABA MIKONO YANGU ITAOTE LINI—SEHEMU YA PILI
(ILIPOISHIA SEHEMU YA KWANZA; Ninamfuatilia mke wangu mpaka kwenye nyumba ya kulala na wageni. Namuona akiingia na X wake, naamua kumfuata mpaka chumbani, nafungua mlango na kumkuta kakaa kitandani na Khanga moja tu, X wake anakuja kutufungulia na taulo lake. ENDELEA… Kama hukusoma sehemu ya kwanza bonyeza hapa Iddi Makengo
Mambo mengi yalipita kichwani kwangu, niliwaona wanangu, niliwaza hivi kweli wanaweza kulelewa na mwanamke kama huyu? “Si alikuambia kashamchoka mke wake basi vitu vyako utavikuta kwake, kwa heri nilikupenda sana lakini naamini nilikua sitoshi ndiyo maana umerudi kwa mwanaume ambaye alikuumiza.” Niliongea kwa sauti ya upole kabisa kisha nikafunga mlango na kuondoka. Niliwaacha mule ndani, kila mtu alishangaa, walijua nitaleta vurugu lakini wapi, nilifanya kinyume chake.
Niliondoka pale mpaka nyumbani, nikakusanya nguo zote za mke wangu na kila kitu chake. Nilivipakia kwenye gari na kuondoka, mwanzoni baada ya kuona yule jamaa anawasiliana na mke wangu nilianza kumchunguza, nilikua na hasira kipindi hicho na nilitaka kumfanyia kitu kibaya lakini nikaamua kuongea na mke wangu kwanza, baada ya kuahidi kuacha basi sikuchunguza tena lakini nilikua najua alipokua akiishi hata mkewe nilikua nikimfahamu.
Nilichukua vitu na kuvipeleka kwa mke wake, nilimuambia ni mizigo yake, nikaviacha pale nnje na kuondoka zangu. Mke wangu hakurudi nyumbani, alienda kwao na kukaa huko kama siku tatu, mwanzo hakuwaambia sababu ya kwenda lakini baada ya kuona simtafuti aliamua kuwaambia, walituma watu kuja kuomba msamaha lakini nilikataa na kumkumbusha kuwa nilishamuambia tangu mwanzo kuwa siku nikimfumania siwezi kumsamehe.
Nilimuambia arudi kwa X wake asubirie talaka na kwangu asikanyage tena kwani siku akikanyaga basi nisije kulaumiwa. Sikuongea sana hivyo hakukua na mjadala, kwangu ilikua ngumu sana kumsamehe. Aliondoka hata wazazi wangu walipoingilia kati na kumuombea msamaha sikukubali, bado nilikua na hasira, nilimfukuza na kumkataza kabisa kuja nyumbani, hata watoto sikutaka awaone kwa kuhofia kuwa atawaharibu.
***
Pamoja na kumuacha mke wangu lakini bado nilikua nampenda, baada tu ya kuachana naye nilibadili tabia, nilijikuta naanza kunywa pombe kitu ambacho nilikua sijawahi kukifanya katika maisha yangu, nilikua mtu wa hasira na kubadilisha wanawake. Miaka mitano ya ndoa yangu nilikua sijawahi kutembea na mwanamke mwingine zaidi ya mke wangu, lakini miezi sita tu baada ya kutengana naye nilishabadilisha wanawake zaidi ya kumi.
Maisha yalikua mabovu na niliona kabisa tabia zangu zinawaathiri wanangu wawili, mmoja mkubwa akiwa na miaka mitano na mdogo akiwa na miaka mitatu. Kwa sababu hiyo niliamua kutafuta mwanamke wa kuishi naye, pamoja na kwamba tulikua bado hatujatalikiana lakini niliamini sitarudiana naye tena. Nilitafuta mwanamke na kaunza kuishi naye, huyo nilimuona kama mke wangu tunapika na kupakua huku akinisaidia kulea wanangu.
Hasira zilipungua hivyo nilimruhusu mke wangu kuwaona watoto mara moja moja ingawa nilikataa katakata yeye kuishi nao. Baada ya kuanza kuishi na mwanamke mpya nilianza kuwa na amani kidogo, nilainza kuwa na familia hivyo nilitaka kuanza mchakato wa talaka na kauchana kabisa na mke wangu, lakini ndugu zangu hawakumpenda yule mwanamke, waliongea maneno mabaya, walitafuta historia yake, wakaniletea umbea mwingi ambao sikuusikiliza, kwangu mimi nilifurahia mtu mpya.
Maneno maneno ya ndugu zangu ndiyo yalinisukuma zaidi kuharakisha suala la talaka, mwanamke yule alikua mwema kwangu na alikua anawapenda wanangu. Niliharakisha mpaka kupata talaka ya mahakamani, nikatengana na mke wangu, nilihonga sana mpaka kuhakikisha watoto pamoja na udogo wao nabaki nao mimi. Mke wangu hakua na kitu kwangu, nilimpa mali tulizochuma wote na sikutaka kabisa kumsikia.
Mara chache chache tulikua tunawasilianja hasa kuhusu watoto ambao nilikua nikiishi nao mimi na mke wangu mpya. Ndugu zangu ni kama tuligombana, bado alikua wakitaka niishi na mke wangu wa kwanza Alana (Si jina lake halisi) lakini mimi nilishafunga huo ukurasa, ingawa kila sehemu walikua wakimtambua mke wa zamani lakini mimi niliamua kubaki na Eliza (mke mpya-si jina lake halisi).
Kwakua nisingeweza kufunga ndoa nyingine ya kanisani niliamua kufunga ndoa ya kiserikali mimi na Eliza. Ndugu zangu wote walinisusia, hakuna aliyehudhuria hata wadogo zangu hakuna aliyekuja, nilifanya sherehe kubwa ya upende mmoja tu, nilikua bado nampenda mke wangu wa zamani lakini niliamuni kwa kuoa tena nitakuja kuwa na furaha, maumivu aliyonipa sikuweza kuyahimili.
Kwangu ishu kubwa haikua kuchepuka, ishu ilikua ni mtu aliyechepuka naye, alikua ni X wake, mwanaume ambaye nilijua alikua anampenda kabla yangu. ile hali ya kuchepuka ilinifanya kuamini kua mimi nilikua simtoshi ndiyo maana akakumbuka alikotoka. Mpaka leo sijui ni sababu gani waliachana lakini tetesi nikuwa huyo mwanaume ndiyo alimuacha mke wangu, bado nilikua naumia ni kwanini amrudie mwanaume ambaye alimuacha na kuoa mwanamke mwingine.
Niliumia sana nikiamini mke wangu hakua akinipenda na katika kipindi cha miaka saba ya mahusiano mpaka ndoa alikua anaigiza tu, sikua tayari kumsamehe kwa hilo. Baada ya ndoa maisha yaliendelea, taratibu nilianza kumsahau mke wangu wa zamani na kujikuta simkumbuki tena, hata alipokua akipiga simu kuhusu watoto sikutaka kupokea, ilifikia hatua nikamkataza kunipigia simu, nilimuambia kama anataka kujua kuhusu watoto basi amuulize Mke wangu mpya kwani yeye ndiyo Mama yao.
Alana alikasirika na kwenda kuongea na Mama yangu mzazi, Mama alinipigia simu na jibu lililkua ni hilo hilo. Wote walikasirika na kuanza kuhisi labda mke wangu kaniwekea dawa, niliwahsangaa kwani kila kitu nilikua nafanya kwa akili zangu, sikua tu nikitaka kuongea na mke wangu wa zamani. Kila wakati akinipigia simu niliona kama ananicheka, picha ya yeye akiwa kitandani na mwanaume mwingine ilinijia, sura ya X wake na taulo lake siku ile ilikuja kichwani mwangu.
Nilishindwa kuisahau na nilijua njia pekee ya mimi kuwa na furaha ni kwa mimi kuacha kupokea simu zake kabisa. Hata watoto sikuruhusu akae nao, kichwani pamoja na kujua kuwa alikua anawapenda lakini sikua na muamini kabisa. Kuna kitu kilikua kinaniambia anaweza kuwafundisha tabia mbaya hivyo nilimpiga marufuku kwenda kukaa nao, kila alipohitaji kuwaona alikuja nyumbani tena akisimamiwa na mke wangu, sikutaka aondoke nao kabisa.
***
Siku moja nilipata safari ya nnje ya nchi, nilitaka kwenda na mke wangu kwa wiki mbili na sikutaka kuwaacha watoto na binti wakazi hivyo nililazimika kuwaacha na Mama yao mzazi. Ingawa mke wangu alitaka niwapeleke kwao lakini sikutaka, nililazimisha wakae na Mama yao kwa muda. Niliporudi aliwaleta watoto, nilikua nyumbania, mara nyingi akija huwa sitoki nnje lakini siku hiyo nilikua narekebisha kitu falani kwenye gari yangu.
Alikuja na kunisalimia, kwakua watoto walikuepo na sikutaka wajue mimi na Mama yao kilichotokea nilijitahidi kumjibu vizuri na kumchekea, hata yeye alijua mbele ya watoto siwezi kumjibu vibaya. Aliomba tuongee pembeni, nilikubali tu kishingo upande, tukatoka nnje na kuwaacha watoto ndani, mke wangu alikua ndani, sikujua kua alikua akituangalia kupitia jikoni, hivyo aliona nilivyoenda kuongea naye.
“Mnaishije na hawa watoto?” Mama Anna (Alana) aliniulza. Nilimshangaa ni swali gani? Maisha yangu hayakumhusu hivyo nilimuambia asiingilie, kama anashida nyingine aseme ila maisha ya mimi na mke wangu na namna tunavyowalea wenetu sitaki aingile. Niliongea kana kwamba mimi ndiyo mzazi pakee nisiyetaka kurekebishwa, kwangu Alana nilimuona kama mpita njia tu mwanamke asiyestahili kuitwa Mama.
“Sio hivyo, lakini Anna hayuko sawa, nimemchunguza muda mrefu alikua hana amani kila tukikutana lakini wiki hii nimeongea naye na nimemuangalia, ana vitu sehemu za siri, kuna kitu umuangalie mtoto. Huyo mtoto anapigwa, hali vizuri, ukimuangalia mgongoni unaweza kufikiri ni ramani…” Aliongea huku akifuta machozi, nlijua alikokua anaelekea, anajua nawapenda wanangu na alitaka kunigombanisha na mke wangu kutaka kuonyesha kama mke wangu alikua akinyanyasa watoto.
“Anna ana makovu mwilini hivi unamkagua mtoto kweli wewe?” Aliendelea kuongea, hasira zilinipanda na kutaka hata kumpiga makofi. “Mshaanza ujinga wenu, nilijua tu, hivi ni kwanini wewe mwanamke una hila hivyo, wewe si ndoa ilikushinda sasa kwanini unaingilkia ninavyolea wanangu! Ungekua Mama bora si ungetulia na mumeo zaidi ya kwenda kuhangaika na wanaume wengine huko!”
“Haya si mambo ya mimi na kuchepuka, nilishafanya kosa na kiroho safi kabisa nimekubali kuachika, lakini siwezi kukaa chini na kukubali wanangu wateseke hapana sitaki kuja kuchukua maiti!” Aliongea kwa hasira, nilimshaangaa na kumuacha akiongea, nikarudi ndani lakini alinifuata. Nilimsukuma kwa nnje na kufunga Geti, kisha nikaingia ndani, nilirudi kwenye gari na kuendelea kuitengeneza.
Sikutaka kuruhusu maneno yake kuingia kichwani kwangu, moja kwa moja nilijua kuwa ule ulikua ni wivu, kawaona watoto wanafuraha bila yeye sasa anataka kunigombanisha na mke wangu. Sikua tayari kuruhusu hilo litokee. “Wanawake nawajua, yaani wiki mbili tu kaakaa na watoto kashatafuta kasoro, mimi si mjinga kuacha wanangu wateseke, wangekua wananyanyaswa ningejua tu!”
Niliwaza, kuna kitu kiliniambia kawakague watoto lakini nilikizuia, niliona ni kama kukosa uaminifu kwa mke wangu. Niliendelea na kazi mpaka mke wangu aliponiita kwa chakula cha mchana, alijaribu kunidodosa sababu za mimi kuzozana na X wangu lakini sikua tayari kumuambia, nilijua kama nitamuambia basi nitamuumiza hisia zake. Niliamua kukipotezea kile kitu ingawa sikua na amani kabisa.
Nilitoka ili kwenda kupoteza mawazo, nilianza kunywa bia kuanzia saa mbili usiku mpaka saa sita, nilirudi na kwenda moja kwa moja kitandani. Mke wangu aliponigusa nilimuambia nimechoka hivyo aniache nayeye alinielewa. Nilijaribu kulala usiku lakini usingizi haukuja. Moja ya sababu ya kutotaka X wangu kukaa karibu sana na wanangu ilikua ni kwaajili ya kuwalinda, nilishamuona kama Mama mbaya hivyo sikutaka awaambukize tabia mbaya wanangu.
Katika maisha yangu hakuna kitu nilichokua nikikipenda kama wanangu hivyo sikua tayari kuona wakiteseka. Ingawa sikumuamini X wangu lakini ilikua ni lazima kuthibitisha, nisingeweza kulala kama wanangu wanateseka. Usiku ule na Pombe zangu niliamka, nilienda mpaka chumba cha watoto, nikafungua mlango na kuwasha taa, nilimuamsha Anna ambaye ndiyo mkubwa, kipindi hicho ana miaka sita.
Bado alikua na usingizi usingizi, pamoja na kuona aibu lakini alikua mwanangu, nilimvua nguo ya kulalia, mimi ni mwanaume hivyo sidili sana na wanangu na ilikua ni mara yangu ya kwanza tangu akiwa mdogo ana miaka miwili kumuangalia akiwa vile. Nilifunua na kuona mgongo, ulikua na makovu mengi mengi, ingawa si kama Mama yao alivyosema lakini ilinilazimisha kuangalia sehemu za siri.
Huko ndiyo nilichanganyikiwa zaidi, katika miguu juu ya magoti alikua ni kama kafinywa na kisu, kulikua na vidonda vidonda vingi havijakauka. “Nani kakufanyia hivi!” Niliuliza kwa hasira, Anna sasa aliamka vizuri, alikua akitetemeka kwa uoga, niliuliza tena kwa hasiera nikaona kama namtisha ndipo nilishusha hasira na kumuuliza taratibu. “Mmma…maa…maa” alijaribu kuongea kwa uoga, sikumuelewa nilimuuliza tena. Ndipo akajibu vizuri “Mama ndiyo kani…”.
Nilishindwa kuvumilia, sikua na hata haja ya kumkagua Kelvin, mdogo wake, nilinyanyuka naye nikiwa nimembeba mpaka chumbani. Nilifungua mlango wa chumbani kwangu kwa nguvu, hasira nilizokua nazo kwa mke wangu nilijua nitamuua. Mara nyingi huwa nasikia mambo ya Mama wa kambo sikutaka kuwa mwanaume mjinga ambaye hulemazwa na mapenzi na kuacha watoto wateseke, kwangu wanangu walikua ni kila kitu.
Mke wangu alijifanya kulala, nilimuamsha na kuanza kufoka, Nilimuonyesha vidonda vya mtoto na kumuuliza vimetoka wapi? Alinyanyuka taratibu kama vile hakuna kitu kilichotokea, taa ilikua inawaka hivyo alifikiacha fikicha macho kuviona. Alionekana kutulia hakupaniki kama mimi, kichwani niliona kama anataka kucheza na kichwa changu. “Hanijui huyu na muulia hapahapa nifungwe…” Niliongea huku nikimuweka Anna chini ili niweze kumuonyesha mimi ni nani na hakuna mtu anayechezea wangu.
ITAENDELEA…
SIMULIZI; BABA MIKONO YANGU ITAOTE LINI—SEHEMU YA TATU
(ILIPOISHIA SEHEMU YA PILI; Nilishindwa kulala hivyo kwenda kumuangalia mwanangu, nilikuta amefinywa na kuumizwa sehemu za siri na mgongoni. Nilimuuliza nani kakufanyia hivi kwa uoga alinijibu Mama. Kwa hasira nilinyanyuka na kwenda chumbani kwa mke wangu na kumuamsha. ENDELEA… Kama hukusoma sehemu ya kwanza na ya pili bonyeza hapa Iddi Makengo )
“Nilitaka kwanza utulie ndiyo nikuambie, umechoka sana mume wangu hayo mambo tutaongea kesho, najua umekasirika lakini nishampaka dawa!” Aliongea kwa kujiamini, nilishangaa kwani sikujua anazungumzia nini? “Nilishakuambia kuhusu Mama yake, yule mwanamke ni mtu mbaya sana, yote hayo ni ili tu kutugombanisha, kama ni ndoa si aseme tu kuliko kuwatesa watoto!” Alizidi kuongea, nilishindwa hata cha kuongea, alikua akinichanganya tu na maneno yake.
“Anna mwanangu… “Aliongea huku akimsogelea Anna ambaye ni kama alimkwepa, uso wake ulijaa uoga. “Usiogope mwanangu Mama yako hayuko hapa, hakuna wa kukupiga tena. Hembu muambie Baba yako kilichotokea maana mimi nikisema nitaambiwa ni wivu! Yaani wiki mbili tu tumemuachia mtoto halafu anamfanyia mambo yote haya, mume wangu hembu muangalie mtoto alivyoharibika, hivi ni Mama yake kweli yule!”
Aliongea huku akimgeuza Anna alimuonyesha mgongo alivyokua na alama alama. “Unamaanisha nini? Mbona mnanichanganya nyie wanwake nani kamfanyia mwanangu huu unyama?” Niliuliza kwa hasira, Eliza hakutaka kuongea, kwa kujiamini alimgeukia Anna na kumuambia aongee kila kitu. Nilishangaa namna Anna alivyokua akiongea. “Ni Mama, nilivyoenda nyumbani aliniambia ananifanyia hili umuache Mama mdogo, anasema unanipenda sana hivyo kukiona ninateseka utamuacha Mama mdogo na kumrudia yeye! Amesema nikiulizwa niseme ni Mama mdogo kanifanyia hivi!”
Kusema kweli nilishindwa kuelewa, Anna alikua akiongea kwa uchungu machozi yanamtoka, haikuingia akilini kuwa Mama yake mzazi angeweza kumfanyia vile. Mama wa kambo sawa lakini Mama mzazi haikuingia akilini, nilimuuliza mara kumi kumi na majibu yake yalikua yale. “Najua ulitamani iwe mimi lakini hivi hujiulizi, nimekaa na hawa watoto kwa mdua gani? Ni lini umeniona hata nawafokea, hata kuwapiga wakikosa, kila siku naishi nao vizuri lakini kawachukua wiki mbili tu umeona kilichotokea?”
Eliza aliongea kwa kujiamini, maneno yake ingawa yalikua magumu kuamini lakini yalifanana na ukweli. Tuliishi naye zaidi ya mwaka na nusu na hakuna hata siku moja niliwahi kumuona akiwafokea watoto, mara nyingi aliwaonyesha upendo, hata walipokosea alikuja kuniambia mimi. Mara nyingi mimi ndiyo nilikua namfokea nikimuambia kuwa wale ni sawa na wanae hivyo asiogope kuwaadhibu. “Sitaki kuonekana mbaya si unajua Mama wa kambo tunavyosingiziwa Mambo!”
Hakuna kitu kiliniuma kama kile, nilishamsamehe mke wangu kunisaliti, alikua ameniumiza mimi lakini sasa anawatumia watoto kutaka kurudiana na mimi kwa kuniiharibia ndoa yangu! “Ni mwanamke wa aina gani huyu?” Niliwaza huku nikinyanyuka, nilichukua ufungua wa gari na kutoka, kichwani nilikua na mawazo mengi, sikujua nia ya X wangu lakini kamwe sikutaka kuruhusu yeye awatese wanangu kiasi kile.
Kwa wanangu huwa nakua kama kichaa hivyo niliingia kwenye gari nakuanza kuendesha usiku ule kumfuata X wangu. Tayari alishahama kwao alikua akiishi peke yake katika moja ya nyumba ambazo tuligawana. Nilienda na kugonga mlango, alinifungulia kwa wasiwasi kidogo, aliona hali yangu, kabla ya kusema chochote nilijikuta naanza kumtandika makofi, alishangaa lakini sikumpa hata muda wa kujieleza.
Maneno ya mke wangu na maneno ya Anna yalinifanya niamini kuwa yeye ndiyo alikua akiwatesa wanangu. Kusema kweli nilimpiga sana huku nikimtukana na kumuambia kitu alichokifanya, alijaribu kujitetea lakini sikumsikiliza nilimuambia hiyo ndiyo ilikua mara yake ya mwisho kuwaona watoto na kama angejaribu kuwachukua ningemuua yeye na familia yake yote. Niliondoka na kumuacha akiugulia maumivu nikarudi nyumbani kwa familia yangu.
***
Nilikata kabisa mawasiliano na mke wangu wa zamani lakini yeye aliendele akunitafuta, kichwani kwangu nilimuona kama mnyama. Pamoja na mimi kumkatia mawasiliano lakini hakukata tamaa, alienda kwa Mama yangu na kumuambia kila kitu, kwakua alishakua na shaka na alikua hampendi mke wangu mpya |Mama naye alikuja juu na kuniambia kama nimeshindwa kuelewa wajukuu zake nimpelekee.
Mimi nilikataa na kugombana kabisa na ndugu zangu wote, kwa mara ya kwanza niligombana na Mama ikafikia hatua hata hatusemeshani, lakini yeye hakujali kila mara alikua akija kwangu na mara zote alipokua anakuja nikiwepo mke wangu alikua akimpokea vizuri ingawa yeye hakuitikia hata salamu yake. Hali hiyo ilinifanya kumuona mke wangu kama mwema zaidi na kujua fika kuwa ndugu zangu ndiyo wenye matatizo.
Walihangaika ikiwa ni pamoja na kuniita vikao lakini ilifika wakati hata simu za Mama yangu na ndugu wengine sipokei, walianza kusema nimelogwa lakini mimi sikujali, nilikua nafuraha na mke wangu. Baada ya kuishi naye kwa kama miaka miwili hivi alipata ujauzito kitu ambacho kilinifanya kumpenda zaidi nikisubiria mtoto. Wakati mmoja nilikua nimesafiri nilienda Mbeya kikazi na nilikaa huko kama wiki moja.
Siku moja nikiwa najiandaa kurudi nilipokea simu kutoka namba ngeni. Nilisikiliza sauti na kukuta ni ya X wangu Mama Anna, ilishapita kama miezi mitatu hivi akiwa hanitafuti tena kutaka kuchukua watoto kama zamani. Niolihisi amekata tamaa, ila kusikia sauti tu nilikata simu na kutaka kuizima, lakini kabla ya kuzima iliingia meseji. “Hembu pokea simu, watoto hawajaenda shule siku ya nne sasa, nahisi kuna kitu kibaya kimetokea Please! Please! Fanya chochote najua unawapenda…”
Alimalizia, niliipuuza ile meseji kwakua ni jana yake tu nilikua nimeongea na Anna na akaniambia shule inaenda vizuri. Kwa watoto sikua na utani nilikua nawajali sana hivyo pamoja na kuwa nilikua simuamini sana X wangu lakini nilitaka kuhakikisha. Nilimpigia mwalimu wa darasa ambaye nilikua na namba yake na mara nyingi tunawasiliana kuhusu maendeleao ya watoto, nilimuuliza akaniambia ni kweli walikua na siku nne hawajakanyaga shule.
Nilipaniki na kumpigia mke wangu, alinijibu tu kwa kifupi. “Kelvin anaumwa hivyo niliona ni bora wabaki wote.” Nilishangaa kwani kila siku tulikua tunaongea na hakuwahi kuniambia hilo, ingawa mara zote alisema Kelvin kalala. Kabla sijamuuliza kwanini hajaniambia chochote alikata simu na baadaye kunitumia meseji “Sijisikii vizuri!” Nilishindwa kuendelea kumjibu, nilimtumia meseji X wangu na kumuambia Kelvin anaumwa, alitaka kujua anaumwa nini lakini hata mimi sikua na majibu, nilimtukana na kumuambia asinisumbue.
Siku ile sikutaka kulala Mbeya, nilichukua gari ya rafiki yangu na kuanza kuendesha nilisafiri mwenyewe usiku wa manane, sijui kwanini lakini moyo wangu ulikua mzito sana na kila wakati nilihisi kuna kitu kibaya kimetokea. Nilifika Dar asubuhi mke wangu alinipokea vizuri kama vile hakukua na kitu kibaya, nilimuuliza Kelvin yuko wapi aliniambia Kalala, Anna siku hiyo alienda shule.
Nilienda chumbani kumuangalia Kelvin, alikua kalala fofofo hata nipomtingisha hakunyanyuka, lakini hilo halikunishtua, kilichonishtua ilikua ni mikono yake, kuanzia kwenye kifundo cha mikono mpaka viganja vilikua vimefungwa na khanga iliyochanwa, ni kama alikua na vidonda, nilitaka kuvigisa ndipo alishtuka na kupiga kelele za maumivu.
“Muache nimempa dawa za usingizi ndiyo inaishia hapo akimka nikulia tu hata chakula hataki!” Mke wangu aliongea, hakuonekana kuwa na wasiwasi. “Kafanya nini mikono?” Niliuliza. “Mwanao mtundu sana, Dada yake alikua anapika maandazi si kaenda kudumbukiza mikono, sijui alidhani ni maji!” Mke wangu aliongea kama vile hakikua na kitu kikubwa kabisa. Nilishtuka na kumuambia kwanini hakumpeleka hospitali alinijibu kwa dharau.
“Una akili kweli wewe, hivi huoni hii hali yangu nianze kuhangaika na magari, nimemfunga hapo nimempa dawa za usingizi atapona tu kwanza vishaanza kukauka.” Mwili nilihisi kama vile nimepigwa ganzi, nilitamani kumvamia na kumpiga mke wangu lakini nilijikuta naywea. Sijui ni nini lakini nilijiona mdhaifu mbele yake. Nilimnyanyua Kelvin ili kumpeleka Hospitalini.
“Kwahiyo ndiyo unaondoka huniambii hata habari za huko?” Aliniuliza, kuna kitu kiliniambia baki lakini Kelvin aliamka, dawa za usingizi ziliisha na sasa alianza kulia. “Mpe tena hizi atalala tena hatasumbua, ukimuacha hivyo atasumbua sana!” Mke wangu aliongea akinileteka kidogo cha dawa za usingizi, kusema kweli sikumuelewa lakini chakushangaza sikufanya chochote. Nilimchukua mwanangu mpaka kituo cha afya cha jirani, kule walifungua mikono.
Kwanza ilikua inatoa harufu kama vile kitu kimeoza, ngozi ilikua imeshikana na kugandaganda, Daktari aliyekua anamfungua mikono alifanya hivyo akiniangalia, machozi yalikua yananitoka. “Amefanya nini?” Daktari aliniuliza, sikua na jibu sahihi zaidi ya lile nililopewa na mke wangu. Aliniuliza ni kwanini sikumpeleka hospitalini hapo sikua na jibu kabisa.
Alianza kunilaumu kwani mikono ya Kelvin ilikua imeoza, hapa nikupelekwa Muhimbili. Aliongea huku akiendelea kumsafisha na kumpatia huduma ya kwanza. Baada ya kumaliza nilishangaa Polisi wakija, nilikamatwa na kupelekwa ndani huku mwanangu akipelekwa Muhimbili. Nilionekana kama vile namnyanyasa mtoto, Daktari ndiyo alipiga simu Polisi baada ya kuona mtoto kaungua ndani na kuachwa bila matibabu.
Nilikaa ndani kwa siku tatu nikihojiwa, chakushagaza katika siku zote hizi sikuwahi kumtaja mke wangu kuwa ndiyo alihusika, kwangu niliona lile tukio kama ajali hivyo niliwaambia nilikua safari na sijui nini kilikua kimetokea. Ndugu zangu walikuja na kuanza kumshutumu mke wangu kusema yeye ndiyo kamfanyia vile mtoto lakini bado niliendelea kumtete eliza nikisema hawezi kufanya hivyo hizo ni njama tu kwakua hawamtaki.
Mpaka wakati huo nilikua naamini ile stori ya kudumbukiza mikono kwenye mafuta kwa bahati mbaya. Nikiwa bado mahabusu nililetewa habari mbaya, viganja vya mwanangu Kelvin vilikua vimeoza sana, alikua katika hali mbaya, dawa za usingizi alizokua akipewa kila siku zilishaanza kumuathiri, vidole vilioza mpaka mifupa na walisema ili kuokoa mikono yake na kumuondoa katika maumivu nilazima akatwe viganja.
ITAENDELEA
SIMULIZI; BABA MIKONO YANGU ITAOTA LINI—SEHEMU YA NNE
(ILIPOISHIA SEHEMU YA TATU; Nikiwa mahabusu nilikataa katakata kumtaja mke wangu kuhusika, ndugu zangu walimlaumu lakini sikujali. Nikiwa huko nikapata taarifa kuwa mwanangu Kelvin anatakiwa kukatwa mikono yake. ENDELEA… Kama hukusoma sehemu ya Tatu basi Bonyeza hapa Iddi Makengo )
Mtu pekee wa kulaumiwa katika lile tukio alikua ni binti wa kazi, hata mimi nilimlaumu yeye. Mke wangu alijua kuwa nilazima atakamatwa kama akiendelea kubaki pale nyumbani, ingawa alijua mimi siwezi kumfanya chochote lakini aliwajua ndugu zangu, pia alimjua Mama Anna asingetaka mambo yaishe kimya kimya, ile tu mimi kuondoka kumpeleka Kelvin hospitalini alikusanya kilicho chake akapakia kwenye gari, alitafuta dereva akamchukua binti wa kazi na kuondoka naye.
Ndugu zangu walipoenda nyumbani hawakumkuta, alipotafutwa kwenye simu na Polisi aliwaambia yeye alikua Morogoro muda mrefu alienda kujifungua. Sijui kwanini lakini nilipoulizwa niliwaambia ilikua ni kweli. Wakati naondoka kwenda Mbeya kikazi mke wangu nilimpeleka kwao kujifungua, kwakua alikua mjamzito na alikaribia kujifungua hawakua na namna zaidi ya kuamini, Polisi waliamini lakini X wangu na ndugu zangu wengine walijua fika namtetea.
Lawama zote tulimshushia binti wa kazi, mimi nililaumiwa kwa kuondoka na kuiacha familia yangu na binti mdogo kama yule ambaye naye hakuonekana, Eliza aliondoka naye na kumficha kwa ndugu yake mmoja, lengo lilikua ni kupoteza ushahidi ionekane kwamba baada ya mimi kurudi na kuona hali ile ya mwanangu basi aliamua kutoroka. Pamoja na mimi kukamatwa lakini sikua na kosa lolote.
Ushahidi ulionyesha nilikua Mbeya na mimi ndiyo nilimpeleka mwanangu hospitalini baada ya kuja na kumkuta kaumia. Kabla ya kutolewa ndipo nilipata habari kuwa Kelvin anatakiwa kukatwa mkono. Sijui kwanini lakini sikujali, muda wote huo akili zangu zilikua kwa Eliza, nilikua nauliza kama anendeleaje, kama amejifungua na mambo mengine mengi, kwa bahati mbaya hakukua na mtu wa kunipa taarifa zake.
Ndugu zangu hawakutaka hata kulisikia jina lake na hakukua na ndugu yake hata mmoja ambaye alinitembelea. Baada ya kuonekana kama hakuna ushahidi wowote niliruhusiwa kutoka, RB kwaajili ya binti wangu wa kazi ilitolewa na kuanza kutafutwa, mimi sikujali sana, akili yangu haikua kwake kabisa, ile kutoka tu nilitaka kwenda Morogoro kumuangalia Eliza. Nilitaka kujua kama kajifungua au la, moyoni nilikua na wasiwasi sana.
Nilijaribu kumpigia simu lakini simu yake ilikua haipatikani, nikampigia Mama yake ambaye hakupoke, ilinibidi kuanza kutuma meseji mfululizo mfululizo ambazo hazikujibiwa. Kwa namna flani nilijihisi kama kuwehuka kwa kushindwa kujua nini kilikua kinaendelea kwa Eliza. Sikuenda hata hospitalini kujua hali ya mwanangu, ile kutoka tu mahabusu na kuanza kuhangaika kumtafuta Eliza na kumkosa niliwasha gari na kwenda kumuangalia.
Nilifika Moogoro jioni kabisa nikafika kwao, ndugu zake walinipokea kwa mashaka sana, wote walijua kilichotokea hivyo walidhani labda nilienda kufanya vurugu. Lakini Eliza hakua na wasiwasi, ile kuniona tu nilishangaa anaanza kulia, alikua akilia huku akilalamika ni kwanini ndugu zangu wanamshutumu kwa mambo ya uongo, kwanini wasingemuuliza hata Anna nini kimetokea, kwanini wanamuona kama mnyama, alilia sana, nilijikuta napata kazi ya kumbembeleza.
Kila wakati alikua akiniambia kama simuamini basi nibora nikamuacha kwani yeye anatarajia mtoto na hataki mtoto wake kuchukiwa na Baba yake. Kweli niliumia sana na kuanza kumbembeleza, kwa wakati huo sikuona hata kosa lake. “Mtu anaumwa ni mjamzito halafu aanze kuendesha gari si itakua shida, vipi mimba ikiharibika…” Nilianza kuwaza, ni kama alikua akilini kwangu kwani aliongezea.
“Hivi ningeendesha gari usiku nikapoteza mtoto unafikiri ingekuaje, ungenisamehe kweli kama hii mimba ingetoka? Si bora yake mikono tu?” Aliniuliza maswali ambayo kwa wakati huo niliyaona kama ya msingi. Niliamuambia aache kuwaza kwani ndugu zangu nawafahamnu tangu muda mrefu walikua hawampendi hivyo ni majungu yao, nilimuambia hata kama wakimchukia wote lakini mimi ndiyo nampenda na hilo ndiyo la muhimu.
“Sawa lakini sasa hivi sitaki kuishi na mtoto wa mtu, sitaki kuonekana kama mkatili hivyo nikishajifungua unawarudisha watoto wako kwa Mama yao, labda akifa ndiyo nitawalea lakini kwa sasa nataka nilee wakwangu!”Aliniambia huku akilia, sikuwa na pingamizi nilimkubalia na kumuambi asiwe na wasiwasi, hata mimi sikutaka tena kuishi na wale watoto kwani kelele za ndugu zilizidi, nilitaka kuishi na mke wangu na mtoto wetu mtarajiwa. “Kama Mama yao anawaharibu awaharibu! Siwezi kuharibu ndoa yangu kwaajili yao!” Nilijiambia huku nikimkumbatia Eliza.
***
Sikupiga hata simu kuulizia maendeleo ya Kelvin, lakini siku ya pili baada ya mimi kutoka jela Mama yangu alinipigia simu, Kelvin alikua amekatwa mikono yote miwili kwa kuondolewa vidole vyote katika mkono wa kulia na kwenye mkono wa kushoto aliondolewa vidole vitatu vya mwanzo na kubaki na kidole gumba na kidole cha shahada. Nilijikuta natoa machozi kumuonea huruma lakini sikutaka kumlaumu mke wangu.
“Alishazidi utundu…” Nilimuambia Mama ambaye alikaa kimya kwa muda kisha akauliza “Uko nahuyo mwanamke?” Sauti yake ilionyesha kukata tamaa, tofauti na siku nyingine ambazo nikiharibu Mama huniongelesha kwa sauti ya juu ya kunifokea siku ile alionyesha huzuni ambayo niliihisi upande wa pili. “Ndiyo Mama niko na mke wangu, anakaribia kujifungua ananihitaji sana wakati huu…” Nilimjibu, Mama alikaa kimya kwa kama dakika mbili hivi kisha akasema “Daaah! Tushakupoteza mwanangu, kwanini Mungu hata maombi yameshindikana!”
Kabla sijajibu chochote Mama alikata simu, nilibaki natafakari maneno yake lakini sikupata jibu, kwa wakati huo sikujua anamaanisha nini? Nikiwa pale Mama mkwe wangu alikuja na kuniona nikiwa katikati ya mawazo, aliniuliza kilichokua kinanisumbua. “Ni Kelvin, mwanangu mdogo, wamemkata mikono…” Niliongea kwa huzuni, aliniangalia kwa kunionea huruma kisha akanishika begani, “Ni mipango ya Mungu mwanangu, usiwaze sana hakuna wa kulaumiwa.”
Aliongea na kuondoka, nilimuona kama vila hataki kuniangalia, nilinyanyuka kumfuata. Alitembea akielekea chumbani kwa mke wangu, ndiyo chumba tulichokua tunakaa sisi, aliingia na kuanza kuongea na mke wangu. Sikutaka kuingia nilisimama nnje nikiwa sijielewei welewi. “Sasa mimi nifanyeje? Kwani mimi ndiyo nimemkata hiyo mikono?” Nilimsikia mke wangu akibishana na Mama yake.
“Mtoto ni shetani wewe, hivi hayo yote angekufanyia mtu kwa mwanao ungesemaje? Una roho mbaya sana!” Mama mkwe alikua akimtukana mke wangu. Walibishana kwa muda, nilitamani kuingia kwani mke wangu alionekana kuzidiwa, kwa hali aliyokua nayo sikutaka asumbuliwe. Mara alianza kupiga kelele za maumivu, nilishindwa kuvumilia nikafungua mlango na kiuingia wote walishtuka na kunyamaza, hata mke wangu aliacha kupiga kelele na kubaki ananiangalia.
“Vipi unajisikiaje?” Nilimuuliza, alianza kudeka huku akishika tumbo, aliongea kwa kulalamika nikajua hajisikii vizuri. Mama yake alikua anamuangalia tu hafanyi chochote, hata nilipomuambia anisaidie hakufanya chochote. Alitoka na kutuacha pale nikihagaika naye. Niliumizwa sana na ile hali kwani nilijua mke wangu yuko kwenye maumivu makali na hakupaswa kumfanyia vile.
“Kwani mimi nimekosea wapi? Eti mume wangu kuna kitu nimekosea, si mipango ya Mungu kwa Kelvin kuumia? Nani anapanga mambo kama hayo? Nimeishi naye muda gani lini ushasikia hata nimewapiga watoto? Kama si utundu wake yote hayo yangetokea? Mbona Anna naishi naye vizuri tu!” Alilalamika sana mpaka kunifanya kuchanganyikiwa, nilimuonea huruma na kumuambia kama anaona hawezi kuishi pale kwao, kama anaona Mama yake hawezi kumuelewa basi nimtafutie sehemu ya kuishi.
Aliniambia hamna shida Mama yake anammudu. Nilimuelewa, kwa wakati huo sikua nikiwaza kitu kingine zaidi yaka na mtoto aliyekua anakaribia kuzaliwa. Usiku wa siku ile alipatwa na uchungu na tulipompeleka hospitalini alijifungua kwa njia ya upasuaji mtoto wa kike. Nilimpigia simu Mama yangu kumuambia kilichotokea lakini hakujali, kwake ile haikua habari, sauti yake ila ya kukata tamaa niliendelea kuisikia.
***
Nilikaa Morogoro kwa wiki moja, kazini walianza kupiga simu, nilikua nimeondoka bila kutoa taraifa yoyote ile, hata suala langu mimi kukamatwa na Polisi sikuliwasilisha ofisini. Tangu kuondoka Mbeya nilipokua kikazi nilikua sijawasiliana na mtu yeyote. Kwa shingo upande niliamua kuondoka, nilitaka kuondoka na mke wangu lakini kutokana na hali yake nilikataliwa, alikua amejifungua kwa upasuaji na kwangu kulikua hakuna mtu wa kumhudumia.
Niliondoka kwa shingo upande, kazini walisikia mambo yaliyotokea, walikua wakinipa pole lakini hakuna mtu hata mmoja ambaye alinipa hongera ya mke wangu kujifungua ingawa kila mtu nilimuambia. Jambo lile lilinikera sana kila mtu aliyekua mbele yangu nilimuona kama adui vile, niliona kama vile wote wanamchukia Eliza. Nilizidi kupata hasira na kuona kama ulimwengu mzima unamchukia mke wangu, mimi sikuwahi kuona ubaya wake.
Hali hiyo ilinifanya kuwachukia hata wanangu wengine, kwa namna flani niliona kama watu wanamchukia mke wangu kwa sababu yao, hii ndiyo maana tangu kurudi sikuenda kumsalimia Kelvin ingawa kila siku Mama alikua akinipa habari zake. Nilimaza miezi miwili bila kwenda kuwaona wanangu lakini kila mwisho wa wiki nilikua Morogoro kumuangalia mke wangu na mtoto wetu mpya ambaye nilimpa jina la Mama yangu.
Ndugu zangu walishakata tamaa na mimi, tulikua hatuwasiliani, mtu pekee ambaye alikua bado hajakata tamaa alikua ni Mama yangu, kila siku alikinipigia simu na mara nyingi kila baada ya kumaliza kuongea na mimi aliniomba tupige magoti tuombe na mara zote nilifanya hivyo. Kila siku alikua ananisihi niende kuwaona watoto, mara zote alikua akiniambia kuwa wanangu walikua wakiniulizia lakini mimi sikujali, sikukataa lakini sikwenda pia.
Kila alipoanza kuongea habari za watoto nilimuambia nitaenda lakini si kwenda. Hali ile ilikua inanikera sana na isingekua ni Mama yangu naamini ningemtukana. Siku moja nilichelewa kurudi nyumbani, ilishaanza kuwa kawaida yangu kwani tangu kuondoka kwa mke wangu nilikua mpweke sana, kukaa nyumba kubwa kama ile peke yangu ilikua inaboa hivyo nilikua napita mtaani nakaa narudi usiku kulala, nilikua sinywi Pombe Eliza alishanikataza kunywa nikiwa peke yangu.
Nilirudi nyumbani na kuingia ndani, kama kawaida nilitaka kwenda moja kwa moja mpaka chumbani lakini nilimkuta Mama yangu kakaa sebuleni. Nilishangaa kwani hakuniambia kama atakuja, mara ya mwisho naongea naye alikua ananisisitizia niende kuwaona watoto lakini hakuonyesha dalili kuwa anataka kuja. Kabla sijawaza kuwa kaingiaje nilikumbuka kuwa alikua na funguo za kwangu wakati niko jela alibaki na funguo za nyumbani kwani mke wangu alitoroka na kuacha milango wazi.
Nilimsalimia na kujiongelesha ongelesha maneno ambayo hayaeleweki, nilikua katika wakati mgumu sikujua hata cha kuongea naye. “Babaaa! Babaaaa! Shikamoo Babaaaa!” Sauti kali ilipenya masikioni mwangu, ni muda sana nilikua sijaisikia sauti ile, kabla hata sijakaa nilisikia sauti ya mwanangu Kelvin, alionyesha uchangamfu wa hali ya juu, kwake ni kama hakukua na kitu kimetokea.
Alinichangamkia kama ambavyo mara zote hunichangamkia ninapokua ninarudi kutoka safari, alinikimbilia na kunikumbatia miguuni. “Baba ulikua wapi mimi mwenzio mikono yangu imepunguzwa! Wameikata chaaa! Angalia Baba ilikua inaumaaaa!” Aliongea hukua kinionyesha mikono yake iliyokua imekatwa, niliinangalia na kuanza kutokwa na machozi, kwake kilikua ni kama kitu kidogo tu, hakujua kama ndiyo amekua mlemavu wa kudumu.
Nilikaa chini na kumnyanyua, Mama aliniangalia huku machozi ya kimtoka. “Sasa namuona mwanangu…” Mama aliongea huku akinyanyuka, alitoka nnje nisijue anaenda wapi kumbe alienda kuingia kwenye gari na kuanza kulia. Kelvin alikua ananielezea stori nyingi, alikua akiniambia kuhusu hospitalini, aliniambia zawadi ambazo watu wamempelekea na kuniambia kuhusu Mama yake namna anavyomuogesha.
“Baba mimi sitaki kuogeshwa tena na Mama, si umesema nishakua mkubwa mimi ni mwanaume…” Aliongea akinikumbusha maneno ambayo mara nyingi kila ninaposafiri namuambia kuwa awalinde Dada na Mama yake wa kambo kwani yeye ndiyo mwanaume wa nyumba. Nilisikiliza huku nikitoa machozi, “Babaa usilie, unafikiri inauma tena, hata haiumi, angalia, angalia naweza hata kupiga ngumi…”
Kelvin alinibembeleza kila mara nilipokua nikitoa machozi kwa kuangalia mikono yake. “Baba mimi sijalia sana, Mama alivyonichoma tu ndiyo nililia lakini sasa hivi silii tena…” Aliendelea kujiganmba. “Baba Mama mdogo yuko wapi nimuombe msamaha, mimi sikupanga kumpiga lakini alikua anampiga Dada, sitaki kuwa mtoto mbaya, mwalimu alisema mtoto mbaya haendi kwa Mungu anachomwa moto, sitaki kuchomwa tena Baba inauma sana…”
Alisema kwa uoga, sasa machozi yalikua yanamtoka. “Umuombe msamaha, kwanini umuombe msamaha?” Nilijikuta nauliza kwani kwa mara ya kwanza nilianza kusikia kilichotokea. “Mama mdogo alikua anampiga dada mimi nikaishika fimbo yake na kumuambia asimpige tena. Niliposhika fimbo ndiyo akasema mikono yangu inanitia kiburi akachukua na kuiloweka kwenye maji ya kupikia maandazi (mafuta yaliyokua yakichemka) mimi nikaungua.”
Nilijikuta natetemeka kwa hasira, kwangu ilikua ni kama mara ya kwanza nasikia, kuna kitu kilinipiga kichwani kama nyundo si nyundo lakini kiliniamsha. “Eliza anaweza kufanya kitu kama hiki kweli?” Nilijiuliza bila majibu, kwa mara ya kwanza nilianza kumuonea hasira Eliza. “Eti Baba kwani mikono yangu itaota lini, nataka kurudi shule Baba lakini siwezi kurudi bila mikono, itaota lini Baba?” Kelvin aliuliza huku akinionyesha mikono yake iliyokatika, maumivu niliyoyapata nilitamani kutembea kwenda Morogoro kwa miguu.
ITAENDELEA
SIMULIZI; BABA MIKONO YANGU ITAOTA LINI—SEHEMU YA TANO
(ILIPOISHIA SEHEMU YA NNE; Mama alikuja nyumbani akiwa ameongozana na Kelvin, baada ya kumuona tu nilibadilika na kuanza kumuonea huruma, Kelvin alianza kunielezea namna alivyochomwa mikono yake moto na Eliza huku akiniuliza kama mikono yake itaota lini? ENDELEA… Kama hukusoma sehemu ya Nne Bonyeza hapa Iddi Makengo )
Nilinyanyuka kutoka nilikokua nimekaa, kwa hali ilivyokua nisingeweza kukaa na Kelvin hata kwa dakika tano zaidi, nilihisi kupasuka, alikua akiongea bila kujua nini kimetokea katika maisha yake. Nilitoka nnje na kumkuta Mama kakaa kwenye gari, nilishindwa hata kumuangalia na kuongea naye, nilitoka nnje kabisa na kuanza kuzunguka nikitembea kama mwehu flani.
Pombe zote ziliniisha, akili ilikua ikimuwaza Eliza, sikujua ni kwa namna gani binadamu anaweza kuwa mnyama kiasi kile. “Amenifanyia nini? Mbona sikuona mateso ya wanangu?” Nilijiuliza bila majibu, nilitembea mwendo wa kama masaa mawili hivi mpaka nikachoka, nilikua naenda nakurudi mwisho nilirudi nyumbani, nilimkuta Mama amekaa Kelvin ameshalala. Siku ile Mama alidhamiria kukaa pale mpaka nizinduke.
“Kakupa nini huyo mwanamke?” Aliniuliza swali ambalo sikua na majibu yake. “Unajua alichokua anamfanyia binti yako?” Hata hilo sikua na majibu nayo. “Unajua kua binti yako alitaka kujiua mara tatu?” Aliniuliza lakini sikua na majibu, kwangu kila kitu kilikua ni kipya, nilishangaa sana kwani Anna alionyesha kumpenda sana Mama yake wa kambo na hata siku moja Eliza hakuwahi kunionyesha kama anawachukia wanangu.
Mama alianza kunisimulia mambo ambayo mke wangu alikua akiwafanyia wanangu hasa Eliza. Sikutaka kuamini, niliona kama niko ndotoni na kwa namna flani nilijiaminisha kuwa labda Mama anadanganya kwakua anamchukia Eliza. Yalikua ni mambo mazito ambayo sijui kwanini aliyafanya kwani kila kitu alikua akikipata na hata siku moja sikuwahi kumuonyesha dalili kuwa simpendi.
“Anawachukia wanao kwakua unawapenda….” Mama aliniambia lakini sikutaka kuamini, hiyo haikua sababu pekee ya kuwafanyia wanangu mateso kiasi kile. Kwa mambo aliyoniambia Mama nilitaka kusikia mimi mwenyewe kutoka kwa mwanangu, sikua nikiamini chochote. Nilitaka kwenda kwa mke wangu wa zamani ambapo ndipo Anna alikua lakini Mama alinizuia, ulikua usiku sana na Anna atakua amelala.
Nilipanda kitandani lakini usingizi haukuja, mambo mengi yalipita kichwani kwangu, nilikua na waza mambo aliyoyafanya Eliza na sababu za kufanya hivyo, nilikua nawaza ni kwa namna gani nimeweza kuishi naye kipindi chote hicho bila kujitambua, bila kuona mateso waliyokua wakifanyiwa wanangu. Sikulala, asubuhi na mapema niliamka na kupanda gari nilitaka kumuwahi Anna kabla ya kwenda shule, ilikua nilazima niongee naye na kuujua ukweli.
***
Mama yangu alishaongea na X wangu, alimuambia kila kitu kilichotokea kua nilikua naenda kuonana na Anna. Ingawa mwanzo ilikua ngumu lakini X wangu alielewa na kutaka kunipa nafasi ya mwisho. Niliingia ndani nikiwa natetemeka kama mtoto mdogo, sijui kwanini lakini nilikua naona aibu sana, tofauti na nilivyotegemea alinipokea vizuri, Anna alikuja na kunisalimia kitu cha kwanza alichoniambia kiliniuma zaidi “Baba mimi sirudi tena kwa Mama mdogo ataniua!”
Aliongea huku akitetemeka kwa uoga, alionyesha ujasiri kidogo, tofauti na umri wale alionyesha kuelewa alichokua akiongea. “Nataka uongee na mwanao, nataka umsikie mwenyewe. Anna mwanangu muambie Baba yako yote…” Mama Anna aliongea kisha kuondoka, hakutaka kusikiliza nilivyokua nasimuliwa. “Baba Mama mdogo anatuchukia…” alianza kuongea. Ni kama alishaizoea ile stori, wakati mimi nilikua nabubujikwa na machozi kama mtoto mdogo yeye aliongea kwa kujiamini bila kutoa hata chozi.
“Anasema sisi ndiyo tunamfanya asiishi vizuri na wewe kwani unatupenda sana. Anasema kama ukifa kwakua yeye alikua hana mtoto basi mali zote tutachukua sisi hivyo alitaka utuchukie. Ukiwa upo alijifanya kutupenda lakini kila ukiondoka mimi na Kelvin tulikua tunaamshwa saa tisa usiku, anatoa nguo nnje na kutuambia tufue kisha kusafisha nyumba nzima. Dada (Binti yangu wa kazi) hutusimamia nai, tunapoanza kufua anataka tuiname tu kama tukisimama basi ni viboko.
Baada ya kumaliza kufua ni kuosha vyombo vya usiku, anataka tuoshe vitakate hivyo mimi ndiyo hua naosha kwani Kelvin ni mdogo hawezi kuosha vyombo. Baada ya vyombo ndiyo husafisha nyumba hata kama si chafu kisha tunajiandaa kwenda shule. Hiyo ndiyo ilikua kazi yetu ya kila siku mpaka tumezoea. Alishatishia kumuua Kelvin kama mimi nikikuambia kitu chochote na alikua anamaanisha.
Siku nilipokuja kwa Mama na kumuambia Mama mpaka akaja kukuambia kuwa tunanyanyaswa hakunipiga mimi, alisubiri ulipoondoka akijua utachelewa kurudi, alimchukua Kelvin na kuanza kumchapa kwenye makalio. Alimchapa sana na kumfungia ndani, alipolia sana alimpa dawa za usingizi, ilia sipige kelele, baada ya Kelvin kulala alinifuata na kunichukua, alinionyesha makovu ya Kelvin kwenye makalio.
Alikua anatoa damu na akaniambia kama nikiongea tena na kumuambia mtu basi atamchoma choma visu makalioni na kumuulia mbali. Niliogopa sana na kumuahidi kuwa sitasema chochote. Hakua akitupa chakula, baada ya wao kula chakula cha kawaida ndiyo sisi hula mabaki ya chakula kama hawajabakiza basi sisi hulala na njaa, hivyo kama nikiona mabaki ni kidogo inabidi nimpe Kelvin na mimi nilale njaa.
Baba unamkumbuka yule Anko alikua anakuja mara kwa mara?” Aliniuliza, kwani kuna ndugu yake mmoja alikua anakuja karibu kila mwezi, aliniambia nimfanyabiashara hivyo anapokuja Dar kuchukua mzigo anakua hana sehemu ya kushukia basi hushukia kweli. Sikua na wasiwasi kwani kuna mara nyingi tu nilishawakuta nyumbani kwangu na Mama mkwe wangu hivyo nilijua ni ndugu zake.
“Yule hakua ni ndugu yake, alikua ni mganga wake, kila mwezi huja kuweka dawa, alikua anakuwekea wewe pamoja na kutupa sisi. Alikua anasema ili utuchukie nilazima wote tutengenezwe, tulikua tunalazimishwa kunywa na kama tukikataa basi ni kupigwa sana. Alikua ananipiga na wakati mwingine hunifinya kwa kisu, Baba ukiangalia mimi nimekatwa katwa sana, amenikata kata huku mapajani na kila sehemu na aliniambia kuwa kama nikionyesha mtu basi atamuua Kelvin kisha kukuua na wewe ili achukue mali na mimi nitabaki yatima.”
Anna aliongea huku akinionyesha sehemu kubwa ya mwili wake, ilikua ina makovu ambayo yalifichwa tu na nguo, yalishaanza kupona. Ingawa baadhi nilishayaona lakini kwangu ilikua kama ndiyo nimezinduka na kuyaona upya. Nilijikuta nalia na kuomba msamaha. “Baba mimi nimeshakusamehe najua si wewe ulishatengenezwa…” Anna aliongea kwa uchungu kidogo, kwa umri kama ule alishajua mambo ya kishirikina, nilishangaa nilikua wapi kipindi chote kile nisimuone mwanangu akiharibikiwa.
“Siku aliyomchoma Kelvin…” Aliendelea, hapa alinyamaza kidogo nilimuona akifuta machozi, alionyesha kuumia zaidi. “Nisamehe Baba, ni kosa lanngu, mimi ndiyo nimesababisha Kelvin hana mikono….” Aliendelea kulia, nilimtuliza na kumuambia hakufanya kosa lolote, nilimuambia apumzike na kama hawezi kuongea basi hakukua na haja ya kuongea. “Hapana Baba nitaongea, siku Kelvin alipochomwa moto nilikua mimi napika Maandazi, najua Baba kupika kila kitu.
Wakati napika kumbe nilizidisha sukari, akaja kuonja na kukuta sukari imezidi, alianza kunipiga akisema kuwa namharibia sukari yake. Alinipiga sana mpaka nikaanza kutapika, nilikua natapika Damu, Kelvin alipoona akakasirika na kumshika ilia sinipige, ndipo alishika mikono ya Kelvin na kuitumbukiza kwenye mafuta ya moto. Hakujali kelele zake, alipiga kelele sana lakini kama kawaida yake Kelvin alikua akilia sana anampa Dawa za usingizi analala.
Lakini siku hiyo hakulala, pamoja na dawa za usingizi lakini alikua na maumivu makali hivyo hakulala aliendelea kupiga kelele. Mimi nilikasirika nilijua kama nisipotoka kuomba msaada basi mdogo wangu atakufa, nilitaka kukimbia kutoka nnje kuomba msaada lakini Dada aliniwahi akanikamata wakatufungia ndani mpaka asubuhi, waliwasha mziki kwa nguvu ili majirani wasisikie chochote na hakuna mtu aliyesikia kelele.”
Nilitaka kumnyamazisha asiendelee lakini alitaka kuongea, nililia kama mtoto lakini yeye hakulia tena zaidi ya alipotaja ishu ya Kelvin kuchomwa mikono. “Mimi ndiyo nilikua namfunga mikono na wote tulifungiwa ndani hata chakula tulikua tunapewa mara moja moja ili tu tusitoke. Siku ulipokuja ndiyo siku niliruhusiwa kutoka alijua utakuja ndiyo maana aliniambia niende shule na aliniambia kama nikimuambia mtu yeyeote atamuua Kelvin.
Niliogopa sana, nilienda mpaka shule kimya kimya lakini nikashindwa kuvumilia, mchana nilimuambia Mwalimu ambaye alimpigia simu Mama. Mama alikuja nyumbani na Polisi alipofika akakuta Mama mdogo kashaondoka na wewe ushamchukua Kevin nakumpeleka Hospitalini. Nisamehe Baba mimi ndiyo nimesababisha mdogo wangu hana mikono.” Aliendelea kuomba msamaha na kuongea, nilishindwa kuvumilia nikatoka nnje, sikujiona tena kama mzazi nilijiona kama shetani kuruhusu yote hayo kutokea.
***
Nilitoka nnje na kuanza kulia, nililia kama mtoto modogo, wakati niko pale kama nusu saa hivi simu yangu iliita, kuangalia alikua ni mke wangu Eliza, sikutaka kuipokea kwa hasira niliipiga simu chini. Nilinyanyuka kutaka kuondoka, nilitaka kuingia kwenye gari na safari ya Morogoro kuanza. Kabla ya kufanya hivyo Mama alikuja, ingawa nilimuacha nyumbani lakini alinifuata baadaye.
“Unakwenda wapi?” Aliniuliza, sikua na jibu la maana, aliniambia nikae nitulie na nisitoke ndani mpaka nijisikie vizuri, nilichanganyikiwa, nilikua kama chizi hivyo kulazimishia kuondoka, alipiga kelele watu wakaja na kunishika, nilirudishwa ndani na kutulia kidogo. Lakini sikuweza kukaa wanangu walikua pale na kila nilipowaangalia nilishindwa kuvumilia. “Mama nataka kumuona yule mwanamke, nataka tu kumuona!” Nilimuambia, alinisihi lakini sikujali. Nilimuambia ilikua ni lazima niende Morogoro siku ileile.
Alinielewa lakini aliniambia nilazima niende na mtu, aliwapigia simu wadogo zangu wawili mmoja wakiume na mwingine wakike. Aliwaambia kila kitu na baada ya kama lisaa limoja hivi walifika na kuanza safari ya Morogoro. Mke wangu sikumuambia kitu hivyo nilivyofika alishangaa kidogo. Alishangaa zaidi kuona nilivyokua nimeongozana na wadogo zangu watu ambao walikua wakimchukia kama nini?
Alitukaribisha vizuri na kujishauashaua, nilikua na hasira sana sikutaka kuongea naye. Sikutaka kukaa wala kugusana naye. “Nimefahamu kila kitu ulichowafanyia wanangu, sikulaumu sana najilaumu mimi kwa ujinga wangu kwanza wa kumuacha mke wangu kwa kosa dogo la kibinadamu lakini kwa kukuacha uichezee akili yangu!” Niliongea kwa utulivu kabisa, sijui kama niliupata wapi lakini nilitulia na kuongea kwa busara sana.
“Unabahati una mtoto mdogo kitu ambacho ningekufanya usingeamini! Sitaki kukuona kwangu na wala sitaki kukusikia tena katika maisha yangu!” Alijaribu kujitetea na kujiongelesha lakini Mama yake alimzuia nadhani aliona hasira zangu na alijua kama akizidi kuniongelesha basi ningefanya kitu cha ajabu. Sikutaka kumchukua mtoto kwani nilijua hana kosa lolote, mambo ambayo Mama yake aliyafanya hayamhusu.
Niliondoka bila kuongea kitu kingine chochote, sikutaka kuendelea kubaki katika ile nyumba. Nilirudi mjini na kuendelea na maisha yangu. Sina maisha tena baada ya mambo yaliyonitokea, wanangu hawataki kuishi na mimi wala mimi sidhani kama naweza kuishi nao tena au hata kuwaangalia usoni. Sijui namna ya kuendelea na maisha baada ya hili, bado mtoto wangu niliyezaa na Eliza namhudumia, namtumia pesa kila mwezi ingawa hatuongei nasubiri akuekue nikamchukue mwanangu, najua atanipa kwani anajua alichonifanyia kama akigoma kunipa.
***MWISHO
0 comments:
Post a Comment