Search This Blog

Tuesday, June 21, 2022

PIGO LA MUNGU

  

IMEANDIKWA NA IDDI MAKENGO

SIMULIZI; PIGO LA MUNGU


Ingawa siku zote nilitamani sana mume wangu kupata mtoto lakini niliumia sana nilipozipata habari zile, namna nilivyozipata na ile hali kuwa si mimi niliweza kumpa mtoto ilinifanya kuchanganyikiwa kabisa.


JOIN US ON TELEGRAM

Ulikuwa ni ujumbe katika simu yangu kwa njia ya Whatsapp kutoka kwa wifi yangu ambaye muda mrefu kama ndugu wengine wamume wangu walikuwa wakinipiga vita kwa kushindwa kumpatia kaka yao mtoto.


“Sasa hivi utaondoka tu wanaingia watu na vizazi vyao…” Ulisomeka ujumbe ule ukiambatana na picha kama kumi hivi za mume wangu akiwa na mwanamke mwingine ndugu zake na mtoto mchanga.


Kusema kweli nilifurahi hasa nilipoliona tabasamu la mume wangu na namna alivyomshikilia yule mtoto, nilikuwa sijawahi kumuona mume wnagu akiwa na furaha namna ile.


Katika kipindi chote cha kuishi naye, miaka mitatu kama mpenzi na miaka saba ndani ya ndoa sikuweza kumuona akiwa amefurahi namna ile. Nilifurahi kwaajili yake lakini wakati huo huo niliumia kwani nilitamani mimi ndiyo ningempa yule mtoto.


********


Mume wangu hakuniambia chochote kuhusu mtoto, siku na miezi ilipita bila kuniambia, nilitamani kumuuliza lakini nilijua italeta ugomvi, hivyo na mimi nilijifanya kutokujua chochote ingawa nilikuwa nikiumia sana.


Alianza tabia ya kuchelewa na nilipomuuliza alisema tu kazi nyingi, alirudi kachoka kuliko kawaida yake, sikutaka kumchokonoa sana kwani nilijua sababu na nilijua kama ningeleta kiherehere ningefukuzwa.


Siku moja alikuja Mama mkwe akiwa ameongozana na wifi yangu pamoja na yule mwanamke aliyezaa na mume wangu, hawakua na mtoto. Nilimtambua kutoka kwanye picha lakini nilijifanya kutokujua chochote.


Niliwakaribisha vizuri, mume wangu alikua bado hajarejea kutoka kazini lakini ulikuwa ndiyo muda wake. Niliwakaribisha na wakati nikiwaandalia juice kwani kulikua na joto sana ile narejea sebuleni sikuwakuta.


Nilijua wameondoka hivyo nilitoka nnje kuwaangalia lakini sikuwaona, nilitoka mpaka nnje ya geti lakini sikuwaona, nikasema poteli ya mbali nikarudi ndani, ile naingia nawakuta wanazunguka zunguka mule dani kujaribu kufungua kila chumba.


Mama mkwe na wifi yangu walikuwa wakimuonyesha nyumba yule mwanamke, wakimuambia nyumba kubwa, wakimuonyesha chumba chake, ambacho ni chumba nilichokua nikilala mimi na mume wangu wakimuaonyesha chumba ambacho anaweza kukifanya cha watoto.


Niliwaangalia kwa hasira mpaka walipomaliza na kurudi kukaa, sikusema chochote, ulitawala ukimya kidogo mpaka wifi yangu aliposema.


“Nilikuambia utatoka tu, wenye vizazi vyao wanaingia. Nyumba kama hii inahitaji watoto sio watu wa kukaa tu…!”


Nilitamani ni mjibu lakini nilijizuia, nilijua ningenyanyua mdogo ningemtandika na makofi. Waliendelea kujiongelesha ili kunipandisha hasira lakini sikuwajibu chochote, niliamua kufanya hivyo wala sikuondoka, nilikuwa nimechoka na maneno yao na nilikuwa nikimsubiri mume wangu kuja pale.


*****


Haikuchukua muda mume wangu alirejea, alistuka sana kuwaona kwani bado alikuwa hajaniambia chochote. Aliwasalimia huku akijifanya kutokumjua yule mwanamke.


“Msalimie vizuri mzazi mwenzako…” Mama yake alimuamrisha baada ya kuona kama anazunga, mume wangu hakufurahishwa na ile hali, alimshika Mama yake mkono na kutoka naye nnje. Waliongea kama dakika kumi hivi kisha wakarudi.


Mama mkwe alirudi akisema “Twendeni! Twendeni! Huyu ameshalogwa..” Aliongea kwa hasira huku akiwashika wifi na yule mwanamke na kuondoka nao. Rohoni nilitabasamu kichwani nilijua mume wangu kamuweka sehemu yake na kamkatalia.


Baada ya kuondoka nilitegemea kusikia msamaha kutoka kwa mume wangu, nilishajiandaa kumsamehe kwani nilijua siwezi pata mtoto na kama mwanaume ilikua nilazima angetafuta mtoto. Mume wangu aliniambia nikae huku akionge kistaarabu alisema.


“Sikutegemea iwe hivi kwani nakupenda sana, lakini kama unavyoona hali si shwari, tumekaa kwenye ndoa miaka saba bila mtoto na mimi nilichoka kuonekana kama si mwanaume kamili…”


Alitulia kidogo kisha kuendelea. “Nilitoka nnje ya ndoa na nimebahatika kupata mtoto…” Nilitamani kumuambia kuwa namuelewa na nipo tayari kumlea mtoto kama wangu lakini hakuniruhusu aliendelea.


“Yule aliyekuja na Mama ni Mama wa mtoto wangu, tuna mtoto wa miezi mitano sasa, tumekua tukiishi mbali lakini naona siwezi tena, mwanangu anahitaji malezi ya Baba na Mama hivyo naamini niwakati nimchukue.


Nimepata wakati mgumu sana kujua namna ya kukuambia ila nilazima uondoke kwani hamuwezi kuishi wote hapa na kusema kweli siwezi kuishi mbali na mwanangu. Nakupenda sana lakini ndiyo hivyo niwakati tuachane kila mmoja aendelee na maisha yake”


Alimaliza kuongea maneno ambayo yaliniziba mdomo, ingawa nilishahisi lakini sikuamini kuwa ninaachwa, nilishindwa hata kuongea nikabaki nimeduwaa, nilitamani kulia lakini hata chozi halikutoka….


Unataka kujua nini kiliendelea…Basi endelea kufuatilia ukurasa hu. Kama bado hujalike ukurasa huu basi Bonyeza Hapa Iddi Makengo Ili usipitwe na kitu.


SIMULIZI; PIGO LA MUNGU SEHEMU YA PILI


(INAENDELEA… Kama hukusoma sehemu ya kwanza bonyeza hapa Mume wangu aliniambia tuachane kwakuwa alishapata mtoto na mwanamke mwingine baada ya ndoa yetu ya miaka saba…..Endelea)


Sijui nini kilinitokea lakini nilijikuta naingia chumbani na kuanza kukusanya nguo zangu, nilikuwa kama chizi, nilikusanya nguo zangu chache nakutoka na begi na pochi yangu ndogo ambayo niliichukua tu sikujua hata ina nini ndani.


Sikusema chochote, sikulia wala kulalamika, nilikuwa kama nimepigwa shoti ya umeme. Mume wangu alinifuata na kuniambia sikutakiwa kuondoka wakati ule ningeweza kulala pale lakini sikunyanyua hata mdomo, alijiongelesha maneno mengi lakini hata hayakuingia masikioni ni kama nilikuwa sipo pale.


Nilisukuma begi langu mpaka getini nikatoka na kuanza kutembea kusikojulikana, kwakifupi nilikuwa sijielewi, mume wangu alinifuata nyuma akinibembeleza kurudi lakini sikumsikiliza, niliona Bajaji inakuja nikaisimamisha nakupanda.


Bado mume wangu alikuwa akinikimbilia na alisimama pembeni ya Bajaji kujaribu kunizuia akisema tuongee kiutu uzima lakini sikumsikiliza nilimuamuru Dereva wa Bajaji aondoke na yeye alinisikiliza.


“Tunaelekea wapi Dada?” Aliniuliza dereva, sikuwa na jibu nilikaa kimya kwa muda wa kama dakika kumi , aliendelea kuendesha mpaka alipofika sehemu nzuri akapaki kisha akanigeukia na kuniuliza tena.


“Hata sijui mdogo wangu, wewe endesha tu…” Nilimjibu huku nikitoa noti tano za elfu kumi katika pochi yangu, nilimuambia akaongeze mafuta kisha tuanze kuzunguka mpaka nitakapo choka.


Kusema kweli sikua nikijua niwapi pakwenda, sikuwa na ndugu Mwanza zaidi ya marafiki tu ambao hata hawakua marafiki zangu wa karibu kihivyo. Nilitaka kutoa simu ili kumpigia Mama yangu nimuelezee kilichotokea lakini niligundua kuwa sikubeba simu, niliiacha nyumbani hivyo nilitulia tu.


Tulizunguka kwa muda wa kama masaa mawili, giza lilishaingia na Kaka wa watu alikuwa bado hajui naenda wapi? Alishajua kilichotokea kwani nikiwa ndani ya Bajaji bila kujijua nilikuwa nalia huku nikiongea mwenyewe, Kaka wa watu alinisikiliza bila kuchoka wala kusema chochote.


Baada ya kuona nimechoka nimenyamaza alisimamisha Bajaji katika nyumba ya kulala wageni, alienda kuchukua chumba na kuja kunichukua. “Dada pumzika hapa ukiwaza nini chakufanya, ukiendelea kuzunguka hivi vijana wanaweza hata kukuibia, usiku huu…”


Aliongea kwa upole huku akinishika mkono kunitoa ndani ya Bajaji, alichukua begi langu na kulipeleka mpaka kwenye chumba alichochukua. Aliniuliza nataka kula nini nikasema nimeshiba lakini hakukubali, alitoka na kwenda kuchukua Chips Kuku na soda kisha kuniletea, alikaa pale nakunilazimisha kula mpaka nikamaliza.


Yule kijana alikuwa akiitwa Nick, kusema kweli alikuwa mchangamfu na aliongea maneno mengi sana kiasi cha kunifanya nisahau kidogo shida zangu. Nilikuwa mkubwa kidogo kwake nikimzidi kama miaka mitatu hivi.


Baada ya mimi kumaliza kula aliniaga huku akiandika namba yake ya simu kwenye kikaratasi na kuniachia. “Dada nitapita baadaye kukuangalia, sasa hivi ngoja nikakamilishe hesabu…” Aliongea huku akiweka ile elfu hamsini niliyompa pale mezani.


Nilimuambia achukue ni zake kwaajili ya muda niliompotezea alinijibu kwa upole “Dada unazihitaji kuliko mimi, angekuwa ni Dada yangu kafanyiwa hivyo ningependa mtu atakayekutana naye amsaidie..”


Aliongea nakuondoka, nilimuangalia machozi yalinitoka. Sikulia kwasababu ya mume wangu bali kwasababu ya kitu alichokuwa amenifanyia, nimuda mrefu ulikua umepita kufanyiwa kitu cha kiubinadaam namna ile. Wakati huo ilikuwa ni kama saaa mbili usiku kwani niliwasha TV na kukutana na taarifa ya habari.


Nilikaa tu pale kitandani nikiwa sina hili wala lile, nilijikuta naanza kulia tena kama mtoto, nililia sana loakini baada ya muda niliona nitakufa kwa mawazo niliamua kutoka kwani kwenye ile nyumba ya wageni kulikuwa na baa. Niliagiza mzinga mkubwa wa Konyagi na kuanza kunywa.


Ingawa nakunyw apombe lakini si mnywaji sana mara nyingi huwa nakunywa wine lakini siku ile nilitaka kulewa harakaharaka, na kweli nililewa kwani ule mzinga nilikuwa nikiunywa kama maji. Kulikuwa na mziki unapigwa pale hivyo nilinyanyuka na kucheza mara kwa mara.


Katika meza niliyokuwa nimekaa kulikuwa na wakaka wawili waliokuja kukaa pale na baada ya muda tulizoeana na kaunza kuongea kama vile tunafahamiana, mmoja wao alianza kunitongoza na kwa namna nilivyokuwa nikinywa walijua kabisa nimalaya nimeenda kutega.


Sijui ni pombe, maumivu ya kuachwa au kukata tamaa na maisha lakini nilijikuta namkubalia na kuamuambia kua nimechukua chumba pale. Ndiyo katika miaka kumi nilikua tayari kufanya mapenzi na mwnaaume tofauti na mume wangu na wala sikuhisi kitu kibaya.


Alikataa nakusema kuwa tunaondoka wote, alitaka tubadilishe kijue twende sehemu nyingine sikubisha nilinyanyuka huku nikiwasisitizia tuondoke, yaani mimi ndiyo nilikuwa na haraka ya kuondoka kuliko wao, bila kukumbuka kama chumba nimefunga au la nilikuwa tayari kuondoka tulinyanyuka na kanza kuondoka.


******


Wale wakaka walilipa bili tukaanza kutoka, ilibidi wanisaidie kutembea kwani sikuweza hata kusimama vizuri. Walikuwa na gari na walinikokota mpaka karibu na gari yao, kabla ya kufungua mlango na kuingi kuna Bajaji ilipaki pembeni, alikua ni Nick yule dereva wa Bajaji aliyenipeleka pale.


Aliniona na kushuka harakaharaka, aliingilia kati nakuwauliza wananipeleka wapi? Wale wakaka walimkoromea kumuuliza kuwa yeye ni nani. Nick alisema mimi ni mkewe na siwezi kuondoka nao. Wale wakaka walaianza kumtukana kwa dharau kuwa hawezi kuwa na mwanamke kama mimi, waliniuliza nikasema simfahamu.


Mmoja wao alimsukuma Nick ambaye alipepesuka na kuangukia kwenye jiwe lililokuwa pembeni, alinyanyuka huku akichechemea. Hakuwafuata tena alirudi kwenye Bajaji yake, wale wakaka walianza kuniingiza kwenye gari yao, Nick hakuondoka, kumbe alienda kutoa sime kubwa kwenye bajaji yake na kuwarudia.


“Broo nitawageuza mishikaki sasa hivi, muacheni huyo Dada?” Aliongea kwa kujiamini lakini wale vijana kutokana na pombe waliendelea kubisha, Nick hakuwa na utani, aliinyanyua ile sime na sijui alifanyaje lakini Kaka mmoja alianza kupiga kelele za maumivu huku akishika kifua, Nick alimchana kwa sime yule Kaka kifuani.


Yule mwingine aliyekuwa amenishikiliakuona vile alinisukuma pembeni nakutaka kwenda kumuokoa mwenzake lakini Nick alikuwa mjanja alirudi kwa nyuuma nakuanza kuwatishia, sasa madereva wa Bodaboda walishajazana na kuanza kumshangilia Nick wakiwatukana wale akina kaka.


Kuona vile wale akina Kaka waliingia kwenye gari yao na kuondoka. Nick alinichukua nakunipeleka ndani, alinilaza kitandani ambapo dakika mbili tu niliala fofofo.


*******


Nilistuka asubuhi kichwa kinauma balaa, nilikuwa najisikia vibaya na kabla ya kufanya chochote nilielekea chooni ambapo nilianza kutapika, yaani nilitapika kwa zaidi nusu saa, kila nikirudi kulala natapika, hali ilikuwa mbaya na nilianza kujutia zile pombe.


Baada ya muda kutapika kuliisha, nilioga nakubadili nguo, niliamua kutoka ili nipate chochote na kwakua kulikua na baa pale basi kulikuwa na supu, nilipiga bakuli la supu na malimau ya kutosha baada ya kushiba nilirudi ndani.


Nilianza kujisikia sawa na nilianza kukumbuka yaliyonitokea, sikutaka kulia tena nilianza kuwaza namna ya kuwasiliana na nyumbani kwani sikuwa na simu na nilihisi labda mume wangu kawapigia kuuliza kama nimewasiliana nao na wangekuwa na wasiwasi sana.


NIlitoka nnje na kumfuata mhudumu mmoja, nilimuomba simu yake kuongea na mtu, ilikuwa haina salio hivyo nilitoa noti ya elfu kumi alinipa nikajiunga kisha nikampigia Mama.


Kumbe mume wangu hata hakuwapigia kuwaambia kuwa sipo nyumbani, tuliongea mengi akanishauri nirudi Dar, nilimuambia sitaweza nataka nikaonane na mume wangu nijue nini kitaendelea, alikataa katakata na kusema atamtuma mdogo wangu wakiume kuja kunichukua.


Basi tuliagana na wakati huo Nick alikua ashafika, alinisalimia, nilimjibu kwa aibu kutokana na mambo niliyoyafanya jana yake. Alinitania tu huku akicheka na kunipigia story za kunichangamsha, aliniuliza kama nimewasiliana na ndugu zangu nikamuambia ndiyo, alitoa simu yake moja na kunipa akiniambia niitumie kwa kipindi hicho.


Aliniaga kuwa anaenda kutafuta riziki na kuniambia kama nitahitaji chochote nimpigie, nilimuambia niko sawa. Nilirudi ndani mpweke nikitamani kumpigia mume wangu lakini nilisita. Siku ile ilienda nikiwa na mawazo sana, Nick alikuja baadaye tukaongea sana, tulishaanza kuwa marafiki alikaa mpaka usiku wa manene na kuaga kuondoka.


Sijui kwanini lakini alipoondoka nilianza kujisikia vibaya, jana yale nilikua nimelewa sana lakini hakunigusa hata kidogo na siku ile tulikaa na kuongea wawili tu chumbani lakini hakunigusa. Sio kwamba nilitaka kufanya naye mapenzi lakini nilitaka hata anitamani.


Nilianza kujihisi kama mbaya, nilipoteza kujiamini na kila mara nilijiangalia kwenye kioo kama nina kasoro. Mara zote aliniita Dada kitu ambacho nilipokuja kufikiri baadaye kiliniumiza kwani nilijiona kama mzee sana ingawa ndiyo nilikuwa na miaka 32 na siku zote nilijihisi bado mbichi.


Nilijikuta nataka tamaa, usingizi ulipotea nikabaki na mawazo, sikuwa nikiwaza sana ndoa bali kuzeeka kwangu, wakati mwingine nilimtetea mume wangu kuwa labda ameniacha sababu ya uzee na si kutokuzaa, niliumia sana.


Niliamka nakuanza kujaribu nguo zote nilizokuwa nazo kujiangalia kama nimzuri. Sijui kwanini lakini nilitamani Nick hata angenigusa au kuniangalia kwa kunitamani na si kuniangalia kama Dada yake, nilijikuta nalia, nalia kwa kuzeeka.


******


Siku iliyofuata Nick alikuja asubuhi, Mdogo wangu ambaye alikuwa ni umri wa Nick (hata yeye nimemzidi miaka mitatu) alikuwa ashaondoka Dar na kwakuwa alikuwa na gari binafsi nilitegemea atawahi.


Akiwa pale nilijaribu kimtega, kujiliza nikimuegemea kuona kama nitamshawishi anitamani lakiniwapi. Kusema kweli sikuwa nikimtaka kimapenzi nilitaka tu anitamani nijisikie vizuri lakini hakufanya vile, Nick alikuwa akiongea kwa heshima mpaka ilikua inaboa, niliumia sana.


Aliniambia anataka kunitoa nikapunge upepo lakini nilikataa, nilijifanya sitaki kuiona Mwanza, napata uchungu, ingawa haikuwa kweli, nilitaka aendelee kukaa pale labda nikiendelea kumtega atanitamani lakini wampi, tulikaa mpaka jioni mdogo wangu alipofika nilimtambulisha Nick kama rafiki yangu mtu aliyenisaidia.


Mdogo wangu ni mtu wa kuongea na mchangamfu walisalimiana na alilazimisha tutoke tukale burudani ili nichangamke, tulitoka ingawa sikunywa wao walikunywa na kweli nilifurahi. Siku iliyofuata nilikuwa naondoka, Baba alimuambia nisirudi kwa mume wangu na wala nisiwasiliane naye tena.


Tulimuaga Nick, nilichukua mawasiliano naye na kumuahidi kumtafuta, nilijikuta natokwa machozi kwa wema wake ambao haukuhitaji chochote, nilitaka kumpa pesa lakinia likataa nakuaniambia “Wewe nii Dada yangu na haya ni maisha nafurahi uko salama hilo kwangu nimalipo tosha..” Nilijikuta natokwa na machozi tuliagana na Nick tukaanza safari ya Dar.


*****


Maisha yaliendelea, nilirudi nyumbani nakupokelewa vizuri, wiki za kwanza zilikuwa ngumu lakini nilianza kuzoea, mpaka nwakati huo mume wangu alikulua bado hajampigia ndugu yangu yeyote simu zaidi ya marafiki zangu kuwauliza kuhusu mimi. Baba aliniambia nisihangaike naye kwani kama angekuwa mwanaume kweli basi angenirudisha nyumbani mwenyewe kwa heshima kama alivyonichukua.


Nilianza kuwa nafuraha ambayo ilitokana na kuongea na Nick kila siku, tulikuwa tukiongea kirafiki karibu kila kitu tukitaniana laki bado alikuwa hajanitongoza au kuonyesha dalili za kunitaka. Mwanzoni nilihisi labda ana mke lakini wapi aliniambia hana.


Nikaanza kuhisi kwamba labda ana matatizo sio riziki lakini stori zake kuhusu wanawake zilizidi kunivuta kwake, kwani kusema kweli alikuwa mtu wa majanga na kwakuwa muda mwingi tulikua tukizungumza kama marafiki basi alinisimulia kila kitu, namna anavyofumaniwa, aliniambia sababu ya kutokuoa ni kushindwa kutulia na mwanamke mmoja.


Kusema kweli nilishangaa kutokana na ustaraabu aliokuwa nao lakini kwa upande wa wanawake alikuwa kicheche sana tena sio wa wanawake wa kutongoza bali wale wasiku moja kalale mbele. Nilijipa moyo labda ndiyo sababu ya yeye kukataa kunitongoza mimi kuwa ni mstaarabu sana, ingawa bado suala la uzee lilinisumbua.


Rafiki za mdogo wangu nao walikuwa wakija nikunisalimia Dada mpaka nikajikuta nakasirika kabisa. Kusema kweli ile hali ilinisumbua na kwakua sikua mtokaji, miezi mitatu baada ya kuachika sikuwahi hata kutongozwa na mtu.


******


Nilishachoka kukaa nyumbani, nilipata taraifa kua mume wangu kashamchukua mama wa mtoto wake na wanaishi pamoja niliazidi kupata hasira kwani nilijua kua mimi ndiyo basi tena. Nilitaka kutafuta kazi, miaka saba baada ya kumaliza chuo na kuamua kuwa Mama wa nyumbni nilitaka kufanya kazi.


Suala la ajira kwangu kwa Dar halikuwa shida sana kwani Baba yangu alikuwa akifahamiana na watu wengi, tatizo lilikuwa ni vyeti, kila kitu changu niliacha kwa mume wangu. Ingawa tulijenga pamoja na kununua viwanja na mali nyingi lakini Baba aliniambia nisichukue hata kijiko kwani sicho kilichokuwa kimenipeleka.


Kweli hata mimi sikutaka mali zake, sikutaka kuonana naye tena na mchakato wa talaka najua ungeniumiza kama ningetaka mali, lakini vyeti ilikwua nilazima nikachukue kwani nisingeweza kuajiriwa bila vyeti.


Baba alitaka mdogo wangu kwenda kuchukua lakini nilikataa nilitaka kwenda mwenyewe, alitaka tuongozane naye nilikataa nikamuambia sitaki anione mdhaifu nataka aone simhitaji. Walitaka kunilazimisha lakini nilikataa na kuamua kwenda Mwanza mwenyewe.


Lakini hiyo haikuwa sababu, sikua nikimuwaza tena mume wnagu bali Nick, bado nilikua naumiza kichwa kwanini hanitongozi na nilitaka kumuona, mume wangu nikama nilishamsahau. Nilienda Mwanza na mtu wa kwanza kumtafuta alikuwa ni Nick alifurahi kuniona kwani tulishakuwa marafiki.


Alikuja kwenye Gest niliyoshukia usiku na tukaongea sana, alitaka tutoke kupunga upepo nikamuambia nataka kupafahamu kwake. Aliniambia nitafahamu tu nisubiri kesho yake, sikukubali, nilimsisitizia na kumtania kama ana mke aseme nisiende alicheka akisem yeye si muoaji.


Nilimtania tena kua kama hajafanya usafi asijali mimi ni mshikaji tu, alicheka zaidi na kuniambia twende. Niliingia kwenye Bajaji yake na kuanza safari ya wkenda alikokuwa akiishi. Kwanzn ilipofika nnje nilishangaa nyumba yenyewe, kiuhalisia kwa kazi yake nilijua anaishi uswahilini lakini haiokuwa hivyo.


Alikuwa akiishi nyumba nzuri yenye geti zuri na wapangaji watatu kila mmoja akiwa na ki appatment chake chenye vyumba viwili, sebule, kajiko na choo cha ndani. Huko ndani ndiyo usiseme, TV kubwa, sofa nzuri kila kitu kilikua kizuri yaani sikutegemea kukuta anaishi vile.


Mpaka niliogpopa labda kulikua na mwanamke anaishi pale au si kwake, chumba kilikuwa kisafi balaa, aliuona mshangao wangu nakucheka huku akitania “Ulijua naishi getto?” Nilibaki nimeduwaa tu na nilishindwa na kumuambia kuwa kweli ndiyo niliwaza hivyo anaonekana msela sana kuishi vile.


“Maisha mafupi Dada yangu, tunaishi mara moja..” Nilitingisha kichwa nakusema kweli, huku nikijiambia kuwa humu sitoki. Aliniambia nakunywa kinywaji gani, bila kujijua nilijiachia kama Mama mwenye nyumba, nikaenda kwenye friji nikaangalia kulikua na wine na bia za kutosha tu, nlitoa chupa mbili za Castle Light na na kuziweka mezani.


Aaliniangalia na kucheka, aliingia ndani kujimwagia maji akiniacha na mawazo kibao. Nilitamani hata kumvamia kule bafuni lakini nilijizuia, nilikunywa zile bia harakaharaka nikaona silewi nikaongza nyingine mbili, baada ya kama dakika kumi na tano hivi alitoka, alishaoga na kung’aa, alivaa singlend na pens kitu kilichofanya niuone mwili wake uliojengeka kimazoezi na utanashati wake. Yaani ule udereva Bajaji wote ulimtoka, sikuvumilia nilimvamia na kumkumbatia nikibusu mwili mzima, alijaribu kunizuia lakini nilishachanganyikiwa.


Kwanza nilikuwa na muda mrefu sijafanya mapenzi, pili nilikuwa namtamani alivyo wakati ule na tatu nilishachoka kuonekana bibi na kama unavyojua wanaume wakiguswa hawalazi damu alishindwa kuvumilia alinipa shughuli pevu. Nililala pale na kesho yake nilienda tu gest kuchukua mizigo, sikujali chochote niligeuka mama mwenye nyumba.


******


Wiki iliisha nikiwa pale, nikama nilisahau kwenda kuchukua vyeti vysngu, nyumbani walikuwa wakinipiga kila siku kama nimechukua nawambia bado mume wangu kasafiri akirudi nitachukua. Wiki mbili ziliisha wakawa na wasiwasi wakataka kumtuma mdogo wangu ndipo nilipoamua kwenda kcuhukua.


Nilimuomba Nick kunisindikiza kwani nilitaka pia mume wangu aone kuwa nisha move on na maisha yangu. Labda niseme kitu, mimi na Nick bado tulikua kama marafiki kwamba nilikuwa najua kuwa hatuwezi kuwa wapenzi kwani nayeye ana mambo mengi, kusema kweli alikuwa mstaraabu lakini linapokuja suala la wanawake ni shida.


Labda niseme Nick ni wale ndugu zetu wa Bukoba, ndiyo maana hata ni mtanashati na anaishi maisha ya juu pengine kuliko kipato chake, lakini pia ndiyo sababu ni fundi na ndiyo maana hatulii, hivyo hata hizo wiki mbili nilizokaa hapo walishakuja mabinti kama watano kuja kumtafuta niliwaambia tu hayupo wakijua kweli ni Dada yake.


Nilibaki tu kucheka walivyokuwa wakimhangaikia ila kwa shughuli yake sikuwashangaa. Hakua na hiyana alinisindikiza, tulienda muda wa jioni muda ambao nilijua mume wangu atakua nyumbanai, kweli tulimkuta, alishangaa kuniona, akajisemeza semeza sana maneno mengi akijua nitapaniki lakini wapi.


Nilimuambia kilichonipeleka, mwanzoni alihisi nataka malizake hivyo akaanza kujisemesha kuwa mali zile ni zake kachuma mwenyewe sijui na mambo mengi mengi, nilimsikiliza na huyo mkewe akiniangalia kwa wasiwasi lakini muda mwingi macho yake yakiwa kwa Nick alimuangalia Nick kwa uoga huku akitetemeka tetemeka, lakini hakuongea chochote.


Baada ya mume wangu kujiongelesha nilimjibu kwa kifupi. “Sikiliza sina shida na takataka zako nimekuja kuchukua vyeti vyangu na si huu uchafu mwingine..” Niliongea kwa dharau huku nikinyanyuka na kwenda moja kwa moja chumbani kwetu, nilikuta hakuna kipya kilichobadilika zaidi ya nguo za watoto zilizokuwa chafu mule ndani, nilifungua droo ambapo naweka vitu vyangu kweli nilivikuta.


Nilichambua nakutoa vyeti vyangu, wakati huo alishakuja kanisimamia pembeni yangu, nilitoa vyeti vyangu na kuhakikisha viko sawa kisha nikanyanyuka kuondoka. Nilitoka na kumuambia Nick twende, alinyanyuka tuondoke, wakati nataka kutoka mume wnagu aliniambia kuwa kuna vinguo vayako uje uchukue.


Aliongea kwa dharau na mimi nilimuangalia kwa dharau na kumuambia “Wape wale wadogo zako nao angalau wapendeze labda wataolewa..” Nilimshika Nick kiuno na kuondoka. Ile tunatoka tu nnje Nick akaniuliza.


“Huyo ndiyo alikuwa mume wako?”


“Ndiyo kwanini? Unamfahamu?”


“Ndiyo, nilishawahi kumuona mitaa flani, nayule ndiyo mke wake mpya? Ndiyo amezaaa naye?”


“Ndiyo na yeye unamfahamu?”


“Ndiyo ni demu wa rafiki yangu…”


“Demu wa rafiki yako au alikuwa demu wa rafiki yako?”


“Hapana ni demu wa rafiki yangu, mpaka sasa ni demu wa rafiki yangu!”


Unafikiri ni nini kitaendelea


SIMULIZI; PIGO LA MUNGU—-SEHEMU YA TATU


Nilisimama na kumuangalia Nick kwa mshangao kisha nikamuuliza “Demu wa rafiki yako kivipi wakati ni mke wa mtu? Inamaana bado wako naye? Alimnyang’anya? Vipi kuhusu Mtoto? Huyo rafiki yako sasa yuko wapi? Bado wana mawasiliano naye?” Niliuliza maswali mfululizo, nilionyesha kama kupaniki hivi, Nick hakutaka kuniambia lakini nilisisitiza, niliendelea kuuliza maswali mpaka tulipofika nyumbani ndipo alipoamua kuniambia.


Wakati ninauliza nilitegemea labda nitapata furaha kua kuwa Mungu kamlipia na mtoto sio wa mume wangu labda kaibiwa na vitu kama hivyo, lakini baada ya kusikia stori nzima nilijikuta nimeduwaa tu sijui namna ya kuhisi kwamba nimuonee huruma mume wangu au nishangilie. Yule dada kwa maana ya mke mpya wa mume wangu alikuwa akitwa Agnes na huyo rafiki wa Nick alikuwa ni mpenzi wake wa muda mrefu, wakiishi pamoja mpaka alipokamatwa na Polisi.


Rugandara au maarufu kama Ruga alikuwa ni dereva wa Bodaboda na Nick alimfahamu kwani walikuwa wakipaki kijiwe kimoja hivyo kujikuta wanakuwa marafiki lakini si wale wa karibu sana. Unaweza kusema ni urafiki tu wa kikazi ambapo huwa pamoja pale kijiweni wanapopaki na wakishatoka basi kila mtu huelekea kivyake Ruga na Agness walianzana muda mrefu tangu Agness akisoma sekondari ambapo Ruga alimpa ujauzito wa kwanza na kuacha shule.


Walianza kuishi pampoja mtoto alipokua mkubwa alimpeleka kijijini kwao Singida na kuwaachia wazazi wake. Agness alikuwa akisoma bweni hivyo kipindi yuko anaishi na Ruga wazazi walijua bado yuko shule kumbe kashaacha muda mrefu na ana mtoto. Baada ya kumuacha mtoto kule alirejea Mwanza na kurudiana na Ruga kuendelea na mapenzi yao. Alikua hajui ni namna gani walikutana na mume wangu mpaka kua wapenzi lakini kuna kipindi Ruga alikamatwa na Polisi


Mbali na kufanya biashara ya bodaboda lakini Ruga alikuwa ni mkabaji, kwamba alikuwa na tabia ya kuwaibia wateja lakini pia kupiga nondo. Kwakifupi alikua ni jambazi na katika kazi zake hizo alikuwa akishirikiana na Agness na wanawake wengine ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwalewesha wanaume wenye hela, kwenda kwenye nyumba za wageni au kwenye magari yao kisha wao huingia na kuiba, kilikuwa ni kitu cha kawaida kwao.


Anasema wakati Agness akiwa mjamzito (mimba ya pili) ndipo Ruga alikamatwa, kuna mtu aliokotwa amekufa katelekezwa kichakani baada ya uchunguzi nikuwa yeye ndiyo alikuwa mtu wa mwisho kuonekana naye kwani alimbeba kama mteja, anasema ni kama mwaka na kitu ulikua umepita na bado ndugu zake pamoja na Agness mwenyewe walikuwa kwaihangaika kumtoa Hviyo ndiyo maana alishtuka kumuona pale kwani ni kama wiki mbili tu alikutana na Agness akiwa ametoka kumsalimia mshikaji, ingawa wao hawakuwa na ukaribu lakini stori nikuwa Agness anahangaika kutafuta pesa ya kumtoa.


Anasema kesi yenyewe haisomeki kwani ndugu wa huyo mtu aliouliwa nao ni masikini tu hivyo Polisi ndiyo wanasumbua wanataka kiasi kikubwa cha pesa ili kuizima ile kesi “Hata huko kwa huyo mume wako naamini atakuwa amejishikilia tu kutafuta pesa basi…” Alimalizia kuongea. Kusema kweli sikufurahia, upande mmoja ulijisikia nafuu kuwa nilifukuzwa bure hata yeye hana mtoto lakini upande wapili ulijaa hofu hasa kusikia mhusika inawezekana hata alishawahi kuua. 


Ingawa nilikuwa nilikua na hasira sana na mume wangu lakini sikua nikimchukia. Ukweli nikuwa bado nilikuwa nampenda naamini kuliko wanaume wote, sikutaka jambo baya kumtokea, jambo kama kuachwa na kuumizwa kimapenzi labda ningefurahia lakini kupigwa na kuumizwa mwili au kuuliwa sijui kama ningeweza kuvumilia Kusema kweli nilichanganyikiwa sikujua nini chakufanya? “Au wameachana na alienda tu kumuangalia kwakuwa walishazaa mwanzoni? Mbona mwanae kafanna na mume wangu?” Niliuliza nikijaribu kujifariji.


“Hapana, hilo lakuachana hawawezi, kwanza wanapendana pili yule dada anamjua Ruga, anajua akimuacha atamuua, unajua sio mara ya kwanza mshikaji kwenda jela na kuna wakati alienda kwasababu ya Agness, alipiga hela wakakamatwa lakini hakumtaja akaenda jela mwenyewe lakini akafanya mambo mambo akatoka. Kuhusu mtoto sijui kwani sijawashikia miguu, lakini nina uhakika akitoka wanaachana na nadhani hata ndiyo mpango wao apate pesa ya kuhonga Polisi kwani nasikia wanahitaji zaidi ya milioni kumi, ndugu wa marehemu nao wanataka milioni mbili sasa kwa usawa huu hata akipiga umalaya vipi unafikiri atazipata!


Lakini kwa mumeo atazipata, yule hata mtoto atauza ili jamaa yake atoke na akitoka mumeo ni bora akae pembeni kwani jamaa anaweza hata kumuua…” Aliongea kwa kujiamini na uhakika kua alikua namanaisha kile alichokua akikizungumza. Hata yeye alionyesha kumhofia huyo jamaa, kusema kweli akili ilinichanganya, nilijua mume wangu aliniacha sababu ya mtoto lakini katika kipindi chote cha ndoa alikua ni mtu mwema kwangu ni shetani tu alimuingia na kunifukuza.


***


Nilikuwa nimepanga kuondoka Jumapili, siku moja baada ya kwenda kuchukua vyeti vyangu, nilishakata tiketi ya ndege kwani Baba alitaka niende kuwahi kupeleka vyeti Jumatatu na kufanya usahili katika Kampuni moja ya rafiki yake Baada ya kupata zile habari nilichanganyikiwa na nilitaka kumuambia mume wangu. Kwa muda nilisahau yote yaliyotokea, sikutaka kumuambia ili kumkomoa, kumcheka au kumuondolea furaha ambayo nilijua siwezi kumpa, nilitaka kumuambia kwakua nilijua alipaswa kujua na kujiandaa.


Nilijua anatumika ili kupatikana kwa hela ya kuhonga, hilo halikuniumiza kwani pesa zenyewe tulichuma wote kilichoniumiza ilikuwa ni kwamba angeweza kuumizwa au hata kuuliwa. Nilijaribu kumpigia simu ili tuonane lakini kila aliposikia sauti yangu alitukana tu akisema ninadharau hata hakujua ni kwanini alinivumilia kwa muda wote ule. Nilijaribu kumsihi kua nina kitu cha maana cha kumuambia lakini alikataa katkata kuongea na mimi.


Nilijitahidi mpaka muda wa kutaka kuondoka ulipofika, nisingeweza kwenda nyumbani kwake kwani nilijua mkewe atakuwepo na kwakua alituona na Nick basi angejua nimejua na angeshtuka. Kusema kweli nilishindwa. Niliamua kuondoka lakini ile nafika uwanja wa ndege ndipo nilipokumbuka kuwa kama ningemfuata ofisini kwao lazima angenisikiliza. Asingetaka kuzua vurugu ofisini kwani ingemuharibia kazi hivyo angenisikiliza kistaarabu. Niligeuza na kuahirisha safari, niliwapigia nyumbani kua naumwa na nitaenda nikijisikia vizuri. Hawakunielewa lakini hawakua na namna.


Siku iliyofuata nilienda ofisini kwao, nilimkuta na kama nilivyotegemea hakuwa na namna alinikaribisha vizuri, wafanyakazi karibu wote walikuwa wakinifahamu na walifahamu tumeshaachana, waliniangalia kwa macho ya huruma lakini sikuwajali, nilienda pale kwa lengo moja tu na hicho ndicho ningekifanya. Alinikaribisha na kufunga mlango kwa ndani, kabla sijasema chochote alianza kunitukana na kunitolea maneno mengi ya kashifa, akisema nina wivu, ninamtafuta sijui na mambo mengi mengi. Nilimuacha akaongea mpaka akachoka kisha nikamuuliza kama amemaliza akanijibu. “Mimi mbona nishamalizana na wewe na kushangaa unavyonifuatafuata…”


Nilitabasmu kisha nikamuomba tukae, kwa shingo upande alikaa ndipo nilipoanza kumhadithia kila kitu. Niliongea mpaka kumaliza kisha akaanza kucheka kwa dharau “Nilijua tu yote haya yatatokea, mke wangu aliniambia baada ya jana kuja na yule Jambazi! Nilishtuka kidogo ndipo nayeye alipoanza kuniambia stori yake. Kumbe baada ya sisi kuondoka mkewe alijua mambo yataharibika ndipo alipomuambia kuwa nilienda na Nick pale kwaajili ya kumtishia.


Alisema Nick anamfahamu muda mrefu kwani ni dereva wa Bajaji na kuna wakati alikuwa akimbebaga mpaka rafiki yake alipokamatwa kwaajili ya kutuhumiwa kuua. Alisema Ruga alikua ni rafiki mkubwa wa Nick na wote waliokuwa wakifanya ujambazi lakini arubaini za Ruga zilifika akakamatwa na Nick inawezekana ananitumia ili kupata hela wapooze kesi iishe kwani wanajua ikisikilizwa basi atamtaja na Nick kwani walikuwa pamoja.


Kwakifupi yule mwanamke alikuwa mjanja alibadilisha kila kitu kana kwamba Nick ndiyo yuko kwenye mipango hiyo. Hakuishia hapo alimpa tahadhari mume wangu kuwa awe makini kwani anaweza hata kumtuma Nick kwa hasira ili kumfanyia kitu kibaya kutokana na kumuacha. Alimuambia awe makini na awaonye ndugu zake kutokupanda Bajaji au Bodaboda za watu wasiowafahamu kwani kina Nick wana mtando mkubwa.


Kusema kweli niliishiwa nguvu, nilimuangalia mume wangu kwa huruma lakini yeye alionyesha hasira, chuki na kiburi akiniambia. “Sasa nakuonya kitu chochote kibaya kikitokea kwangu au kwa familia yangu, ukimdhuru mke wangu au mwanangu nakuua kwa mikono yangu!” Aliongea kwa hasira huku akinishika na kuninyanyua alinitoa mule ofsini kwake kisha akajifungia mwenyewe. Nilitoka nikiwa na huzuni tena kwa aibu.


Nilitoka na kurejea kwa Nick nilimuhadithia kila kitu na kumuomba awe makini kwani na yeye wanaweza mfanyia kitu kibaya. Alinitoa wasiwasi na kuniambia yeye ni mtoto wa mjini na hawawezi kumfanya chochote. Pamoja na hivyo bado nilimsisitiza kuwa makini, sikuwa na namna nilijiandaa na siku iliyofuata niliondoka, sikutaka kuendelea kukaa Mwanza. Ingawa roho ilikwa ikiniuma lakini nilishatekeleza wajibu wangu wakumuambia ukweli, nilishanawa mikono hivyo chochote ambacho kingetokea kisingekuwa juu yangu tena.


***


Mwezi ulipita nilishapata kazi katika kampuni moja hivi kama mhasibu, kusema kweli sikusikia chochote lakini siku zangu zilikuwa zimechelewa, kwakuwa kalenda yangu mara nyingi haieleweki na nilishasahau suala la kupata mimba sikuwaza sana nilijua zitakuja tu. Siku moja Mama alikuja chumbani kwangu na baada ya kuongea mambo mengine aliniuliza swali ambalo lilinishangaza.


“Hiyo mimba ni ya nani, ni ya mume wako au kuna mtu mwingine?” Kusema kweli sikumuelewa kwani sikujua hata kama nina mimba, nilikuwa nimeongezeka mwili kweli lakini nilihisi labda nikwakuwa nimeridhika baada ya kupata kazi na kuwa na amani, sikuwa nikiumwa au kutapika na kujisikia vibaya kama wanawake wengine ambavyo husema wakiwa wajawazito. Nilimbishia na kumshangaa nikimuambia kua mimi sina mimba. Alicheka nakuniambia ana watoto saba hivyo siwezi mdanganya kuhusu mimba, anasema alijua wiki mbili zilizopita lakini alisubiri kama ningemuambia au la.


Sikumuelewa, nilimuambia sijui lakini alisisitiza nimuamini. Nilikuwa na furaha ya ajabu, nikitamani kujua ukweli, sikutaka kumuamini Mama, nikitu ambacho nilisubiria muda mrefu, ulikuwa ni usiku na Mama aliniambia kama simuamini basi kesho yake angenipeleka kupima. Kwa mshawasha niliokua nao sikusubiri kesho yake, nilimuambia tunaenda usiku uleule, alicheka lakini sikumuelewa, alimuamsha Baba ambaye alishaingia chumbani kulala ili atupeleke kwenye kituo cha afya cha rafiki yake.


Baba hakujua naumwa nini lakini Mama alimuambia naumwa hivyo Mzee wawatu aliamka akampigia rafiki yake ambaye naye alikuwa amelala lakini kwa heshima ya Baba aliamka na kwenda. Tulifika na baada ya vipimo kweli nilikua na ujauzito wa mwezi mmoja, nilipiga kelele za furaha kama chizi, ingawa walikuwa hawajui ni ya nani lakini Baba na Mama walishangilia kama watoto wadogo, niliwapigia ndugu zangu wote na ile tunarudi nyumbani tu walishafika kunipongeza.


Hakuna hata mmoja aliyeuliza kuhusu Baba wa mtoto wote walikuwa na furaha. Mama aliwalazimisha iwe siri na isitoke mule ndani kwani alikuwa hataki mkono wa mtu kuingia. Kwa furaha niliyokuwa nayo nilikubaliana na chochote. Siku ile nikama tulikesha kila mtu nafuraha zake, asubuhi ndiyo nilipata muda wa kulala na baada ya kuamka nikijua yeye ndiyo Baba nilimpigia Nick, alinipongeza sana na kusema kweli sauti yake ilikua na furaha ingawa alikuwa na wasiwasi.


“Daa sister sema na mimi sieleweki unajua bado sijatulia kabisa…” Bado alikuwa akiniita Dada, nilijua wasiwasi wake na nilimuambia mimi sitaki mume wala mpenzi nimepata mtoto inatosha, nilimshukuru kwa kunipa mtoto na kumuomba aendelee kua rafiki, hapo alipumua kidogo kwani wasiwasi wake ulikuwa ni fedha. Ingawa alikuwa akipata pesa nyingi lakini aina ya maisha aliyokuwa akiishi ilimfanya kutokuwa na akiba na wakati mwingine madeni yalimzidi.


Uzuri wa Nick nimkweli na hakimbii majukumu, katika umri ule tayari alikuwa na watoto wanne wote wa Mama tofauti na wakwangu angekuwa watano, wote alikuwa akiwahudumia kwa kidogo alichokuwa nacho. Kwangu pesa haikuwa tatizo na nilijua atakuwa Baba mzuri kwani hata hao wanne alijitahidi sana kuwatunza. Tuliongea mengi, ile ilikuwa siku ya furaha sana kwangu, niltamani kumuambia kila mtu, nilitamani kumuambia hata mume wangu, mawifi zangu nakila mtu lakini nilijizuia, Mama alishanikataza na hata mimi sikutaka kuitia gundu mimba yangu.


***


Wiki mbili zilipita, mambo yalikuwa yakienda vizuri na furaha iliongezeka mara mbili. Wakati nikiongea na Nick aliniambia kuwa Ruga ametoka hivyo anawasiwasi na mume wangu kwani nilazima angemfuata mkewe. Haikupita siku tatu nilipata habari kuwa mume wangu alikuwa amevamiwa na majambazi walimpiga na kumwagia tindikali usoni. Waliiba baadhi ya vitu na mkewe naye alipigwa na wote walilazwa hospitalini mume wangu akiwa na hali mbaya zaidi, Agneess yeye aliumizwa mbavu tu na mkono.


Hali ya mume wangu ilikuwa mbaya sana na kulikuwa na uwezekano angepoteza uwezo wake wa kuona. Kusema kweli nilimuonea huruma na nilitamani kwenda kumuona lakini ingawa kamimba kenyewe kalikua ka mwezi mmoja na nusu nilikuwa na hofu kusafiri, sikutaka kufanya kitu chochte cha kuhatarisha afya ya mwanangu. Ingawa ndugu zangu wasingekubali niende lakini kwa nilivyosimuliwa niliumia sana. Bado nilikuwa nampenda kama mwanadamu na kwa mtu ambaye alikwa ndiyo kila kitu kwangu sikutamani yamkute mabaya kama yale.


Siku zilienda na siku tano baadaye nilipokea simu kutoka kwenye namba mpya, ilikuwa mwanamke ambaye alianza kunitukana sana kisha kuniambia kuwa mipango yangu ya kuwaua imeshindikana na wote tutakamatwa. Hakua mwingine bali Agness alishatoka hospitali na kipindi hicho mume wangu walikuwa kwenye mchakato wa kumhamishia muhimbili kwani hali ilikua mbaya sana.


Nilimsikiliza tu na kukata simu, sikutaka kujipa stress. Baaada ya kukata nilimpigia Nick lakini hakupatikana, nilijaribu namba zake zote hakupatikana, nilijua labda ni network hivyo nilitulia mpaka jioni nikapiga tena hakupatikana. Nilianza kuwa na wasiwasi kwani tangu nipate ujauzito Nick alinifanya kama mtoto kunipigia simu mara kwa mara kujua ninaendeleaje, haikuitokea kukaa masaa mawili bila kuongea na mimi achilia mbali kutwa nzima.


Nilikumbuka kuna wakati alinipigiaga na simu ya rafiki yake mmoja, dereva mwenzake. Nilitafuta ile namba niliyoi save Nick Friend nakumpigia, nilipomuuliza alinipa jibu ambalo lilinichanganya. Aliniambia “Nick amekamatwa na Polisi kwa kosa la ujambazi, anatuhumiwa kuvamia nyumba moja wakampiga mhusika na kumwagia tindikali, hali yake ni mbaya na wakati wowote kesi inaweza kubadilika kutoka ujambazi wa kutumia silaha na kuwa mauaji..”


Nilichanganyikiwa kwani nilijua nini alichokua akizungumzia, alisema mke wa huyo mtu ndiye alimtambua Nick kama ni mmoja wa majambazi kwani naye aliumizwa ila amepona na ametoka Hospitalini. Nguvu ziliniishia, Baba alikuwepo, aliniona wakati naongea nalegea akanikamata kabla sijadondoka chini. Alinikalisha chini na kuanza kunipepea ili nipate ahueni. Baada ya hapo nililazimika kuwaambia kila kitu ikiwa ni pamoja na Baba wa mtoto na sababu za kukamatwa kwake.


Niki alikaa mahabusu kwa siku moja tu, baada ya uchunguzi iligundulika kua hakuhusika na chochote kwani Mungu alikuwa upande wake, siku ya tukio Nick alikuwa mahabusu. Alikamatwa baada ya kugonga gari ya RPC, ingawa hakukuwa na mtu aliyeumia wala kufariki lakini alikutwa amelewa hivyo kuwekwa ndani kwa siku mbili. Mimi hakuniambia lakini ilikuwa ndiyo pona yake, Agness alihojiwa tena na akawa anajichanganya kusema labda alituma watu.


Mara yeye ndiyo mwenye kisasi na mumewe, huku akisema alisikia sauti kama yake, mara aliona mtu kama yeye akamfananisha na mambo kama hayo. Polisi waliona anawasumbua hivyo kumuachia Nick. Hapo ndipo nilipokuwa na amani kidogo lakini bado hali ya mume wangu ilikua mbaya, walimhamishiwa Muhimbili kwaajili ya uchunguzi kuona kama anaweza kuona ambapo baada ya kufika walisema labda apelekwe India.


Hapo ndipo rangi halisi ya Agness ilipoonekana, Mume wangu alikuwa na akiba lakini zilipotafutwa pesa benki kulikua hakuna hata shilingi, Agness alifanya ujanja katoa pesa zote na kutumia kumtoa Ruga jela. Walianza kuhaha sasa kutafuta pesa, wakati ndugu zake wakiwa bize Dar kwenye matibabu Agness alikua bize akitafuta mteja wa nyumba, alimshawishi mume wangu pamoja na ndugu zake waiuze ile nyumba kwajili ya matibabu.


Alijifanya mke mwema ana uchungu na afya ya mume akimuambia kuwa kama ni pesa, nyumba watatafuta nyingine lakini hatakua na maisha kama atapoteza macho, nyumba kweli iliuzwa Agness akiisimamia mwenyewe lakini usiku ule ule baada ya kuuza nyumba alitoweka na pesa zote, yeye na Ruga waliondoka na kutokomea kusiko julikana wakiwa na mtoto wao. Hapo ndipo walipoona rangi halisi ya Agness, ndugu walibaki kulia tu hawana chakufanya.


Mpaka wakati huo nilikuwa sijaenda kumsalimia, bado kulikuwa na maneno yanazunguka kuwa mimi ndiyo nilipanga njama za kumdhuru hivyo wazazi wangu walinikataza kabisa kwenda. Baada ya Agness kutoroka na pesa ndipo walipojua ukweli, huko hospitalini kila siku mume wangu alikuwa akiomba tu kuonana na mimi ili aniombe msamaha kabla ya kufa. Mara mbili mdogo wake (yule yule aliyenitukana) alinipigia simu kuniambia.


Nilijizuia kuumia lakini ilishindikanja, walikwa wakinitumia picha zake, uso ulikua umeungua sana, sura haionekani macho amefungwa bandeji, bila kujali kama alikua mume wangu kwa ubinadamu tu mtu yeyote ungemuonea huruma. Siku moja nikiwa nyumbani Mama mkwe wengu, wifi yangu na shemeji yangu mmoja walikuja nyumbani, walikua wakilia na kupiga magoti kuomba msamaha.


Zilikuwa zikihitajika zaidi ya milioni kumi ili kumpeleka India kwa matibabu na hiyo ilikuwa ni awamu ya kwanza tu, nikiasi ambacho hawakua nacho, hata mimi kwa wakati huo sikuwa nazo. Kusema kweli walikuwa wanatia huruma, niliwasamehe lakini Baba alikuja akawakuta na kuwafukuza. Kwahali aliyokuwa nayo sikua na amani na nilianza kujisikia vibaya kutokumsaidia, nilimumba Baba atoe hizo pesa kumsaidia mume wangu lakini alikataa, Baba alikuwa nazo na angeweza kuwasaidia lakini kwa waliyonifanyia alikataa.


Sikukata tamaa niliongea na Mama ambaye alikuwa na hela ya kunisaidia ila asingeweza kuzitoa bila idhini ya Baba, nilibaki tu sina namna, siku mbili nilishindwa hata kula, sio kwamba nilikuwa sitaki lakini nilikuwa na mawazo, nilikuwa na hasira sana na mume wangu lakini sikuwa nikimuombe mabaya. Nilimpenda na nilijua nayeye alinipenda, ningefurahi kama angeachwa na kuumizwa katika mapenzi lakini sio kufa au kuwa kipofu.


Baba aliniangalia nilivyokuwa nikiumia na bila kusema chochote aliandaa safari na kutoa pesa zote za matibabu kwaajili ya mume wangu. “Natamani hata nikupige makofi kumuonea huruma mtu aliyekufanyia yote hayo lakini haitasaidia, usidhani nimetoa kwaajili ya huyo mume wako au wewe na upuuzi wako. Nimetoa kwajaili ya mjukuu wangu kwani najua kwa unavyoendelea naweza kumpoteza na sijui kama nitaweza kujisamehe kwa hilo.


Mali hizi hazitakuwa na thamani kama nitaambiwa mimba imetoka na mjukuu wangu niliyemsubiri kwa miaka mingi sitamuona kwajaili ya upuuzi wako!” Baba aliongea kwa hasira, machozi yalinitoka, nilinyanyuka na kumkumbatia ingawa hakutaka, nililia kifuani kwake kwa zaidi ya dakika tatu akalazimika na yeye kunikumbatia.


Nilienda hospitalini kumuona mume wangu, alikuwa hawezi kuniona lakini alifurahi kusikia sauti yangu, aliniomba sana msamaha na mimi kumuambia nilishamsamehe muda mrefu. Hatukuwa na muda sana maandlizi yalishafanyika hivyo alipelekwa India. Kila wakati aliniaga na kuniomba msamaha mara miamia, alikua anasikitisha sana, niliumia sana kumuona katika hali ile hawezi kufanya chochote.


Alikaa India kwa wiki tatu, walifanikiwa kuokoa maisha yake lakini alipoteza kabisa uwezo wa kuona. Sasa hivi yupo tu nyumbani kwao akiishi na Mama yake kwani hawezi kufanya tena kazi aliyoajiriwa nayo. Mara kwa mara ninapo pata vihela huwa namtumia kwani namuonea huruma kutokana na aina ya maisha anayoishi. Ni mwaka wa pili sasa tangu yote haya kutokea, Mungu amenijalia kupata mtoto wa kike.


Nick bado ni rafiki yangu si wapenzi tena ingawa ningependa sana kupata mtoto wa pili na yeye. Kusema kweli siwazi sana kuhusu ndoa, angalau sasa nina furaha na maisha yanaenda. Agness na Ruga hawajulikani wametokomea wapi na hakuna mtu anayefuatilia. Wifi yangu yule kashamaliza kidato cha sita na sasa yuko chuo na mimi ndiyo namlipia ada ili angalau asome na aweze kuisaidia familia yake kwani karibu kwao wote walikua wakimtegemea mume wangu ili kuendelea kuishi. Nimeshafuatilia talaka ya mahakamani na sasa niko huru naendelea na maisha yangu.


***MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

BLOG