IMEANDIKWA NA IDDI MAKENGO
MAMA MKWE; NIHERI UNGENIUA MIMI—SEHEMU YA KWANZA!
“Mama yangu anakuja kesho kutwa”. Alianza kuongea mume wangu.
JOIN US ON TELEGRAM
“Yupo likizo?” Niliuliza. “Hapana likizo alishachukua, sema imebidi aombe ruhusa ya wiki mbili, anataka kuwepo ukijifungua…”
Hapo nilishikwa na kigugumizi kidogo, sikuona sababu ya yeye kuomba ruhusa kuja kunihudumia. Kwanza Mama yangu alikuwa pale na pili tulikuwa hatupatani sana, miaka minne ya ndoa bila mtoto ilileta maneno mengi.
Mume wangu aliuona wasiwasi wangu akanituliza. “Hakuna kitu kibaya, ni mjukuu wake wa kwanza yale mengine yalishapita, anataka tu kuhakikisha unajifungua salama.” Aliongea huku akinikumbatia.
“Hamna shida, tena ndiyo itakuwa vizuri, tangu nibebe ujauzito sijamuona…” Nilimtoa wasiwasi mume wangu.
“Sasa itabidi Mama yako aondoke, hawawezi kukaa hapa wote wawili…” Hapo ndipo nilishtuka zaidi, nilijiondoa katika mikono yake na kunyanyuka kwa mshangao.
“Mama aondoke, kivipi? Unataka Mama yangu arudi nyumbani hata kabla sijajifungua?” Niliuliza kwa mshangao na sauti ya juu kidogo.
“Ndiyo kuna haja gani ya yeye kuwepo kama Mama yangu atakuwepo hapa. Arudi Kijijini utaenda kumsalimia mtoto akishazaliwa.
Mume wangu aliongea kwa sauti ya kumaanisha huku akigeuka upande wa pili kulala. Nikama alikuwa ameshafanya maamuzi na alikuwa ananipa taarifa tu. Nilijaribu kumsihi kuwa itakuwa ngumu kwangu kumwambia Mama aondoke lakini hakunisikiliza.
Alisema Mama yake anakuja, yeye ndiyo mwanaume, mtoto yule ni wake hivyo siwezi kumpangia. Nitajua namna bora ya kumwambia Mama aondoke arejee Kijijini na kama nikishindwa basi atamwambia yeye bila kujali atachukuliaje!
*****
Usiku mzima nilikuwa nawaza ni namna gani nitamwambia Mama aondoke baada ya kuhangaika sana na mimi kiasi kile. Ni kweli hakuwa mjukuu wake wa kwanza lakini alikuwa mjukuu wake wa kwanza kwa mtoto wa kike.
Lakini hiyo haikuwa ishu, ishu ilikuwa ni namna Mama alivyohagaika na mimi, kwanza kwa kupatikana kwa ile mimba na pili katika kuilea ile mimba mpaka kufikia pale.
Unaweza kushangaa kwanini nasema hivi, lakini mwaka mmoja baada ya ndoa bila mimi kubeba ujauzito maneno yalianza kuongewa kuwa mimi sizai. Ndugu wa mume walianza kunisengenya na kupiga kelele.
Mume wangu ndiyo mtoto wa kiume wa kwanza kwao, hivyo suala la mjukuu lilikuwa likisubiriwa sana hasa baada ya yeye kuchelewa kuoa akioa akiwa na miaka 33.
Mwaka wa pili ulipita bila dalili za mimba wala mtoto, sasa walianza kumtaka mume wangu atafute mwanamke mwingine. Mama mkwe alimletea mwanamke kabisa lakini mume wangu alimkataa mpaka ikafikia hatua ya kugombana na ndugu zake kwaajili yangu.
Kuona vile Mama hakunyamaza, alianza kunitafutia dawa za mitishamba kwani hospitali tulishahangaika sana. Ni kama nilihamia kijijini kunywa mitishamba na Mungu kweli alisaidia, mwaka wanne nilipata ujauzito.
Kipindi hicho wakwe zangu walishanitenga wakisema nilimpa mtoto wao dawa ndiyo maana hawasikilizi wao ananisikiliza mimi, sikujali sana kwani mume wangu alikuwa ananipenda sana na tulijua ni mipango ya Mungu.
Baada ya kupata ujauzito bado ndugu zake walikuwa wazito, ingawa mawifi na mashemeji zangu walikuja kunisalimia kwa shingo upande kwani walikuwa wakitaka hela kutoka kwa Kaka yao lakini si Mama mkwe wala Baba mkwe walifika kuniona.
Lakini haikuishia hapo, mimba yangu ilipotimiza miezi minne ilianza kuwa matatizo, hospitalini nikaambiwa nipumzike nisifanye chochote, hapo ndipo Mama alikuja kunihidumia, tangu mimba ikiwa na miezi minne mpaka wakati huo nakaribia kujifungua wanataka nimfukuze.
Nilijikuta nalia tu usiku mzima, nilidhani mume atanionea huruma lakini wapi, alishafanya maamuzi akisema ni lazima Mama aondoke. Sijui ni nini kilitokea lakini Mume wangu alibadilika sana, usiku ule alikuwa ni kama mtu mwingine tofauti kabisa.
Asubuhi kabla ya kwenda kazini, aliniuliza kama namwambia Mama au amwambie yeye kwani Mama yake anakuja kesho yake na hakutaka amkute pale. Niliitikia tu kwa unyonge kuwa namwambia, ingawa sikujua ni namna gani nitamwambia.
“Aandae na mizigo yake, kesho anaondoka!” Aliongea na kuingia kwenye gari kisha kuondoka. Aliniacha nikiwa na majonzi makubwa, mwili ulikuwa unatetemeka kwa hasira nikifikiria namna ya kumwambia Mama aondoke.
******
Asubuhi Mama alikuja chumbani kwangu kuniletea uji, nilijikuta nalia tu bila kuongea chochote, Mama alianza kuwa na wasi wasi na Baada ya kunibana nilimuambia huku nikisema ni bora niondoke naye kuliko kumfukuza.
“Mwanangu hicho ndiyo kinakusumbua. Hata hamnifukuzi mwanangu, wewe ni binti yangu umeolewa, huku ndiyo nyumbani kwenu, kimila mimi sitakiwi kukusafisha, si mimi wa kukukanda ni kazi ya Mama mkwe wako, Mama mpya.
Tena afadhali amekuja kunisaidia maana Baba yako anaumwa Kijijini, niende nikamuone kabisa.” Mama alidanganya kwani jana yake tu niliongea na Baba na alikuwa mzima, nilinyamaza kujifanya nimemuelewa lakini roho ilikuwa inaniuma kupasuka!
******
Nilitegemea Mama mkwe wangu kuja kesho yake baada ya Mama kuondoka lakini walikuja siku ileile, mume wangu aliwapokea stend wakati anatoka kazini. Wao walikuwa wanaishi Morogoro, alikuja na wifi zangu wawili wadogo zake mume wangu.
Tulisalimiana vizuri tu, walisalimiana na Mama, ingawa hawakumchangamkia lakini Mama alijitahidi sana kuwachangamkia, akimshukuru kwa kuja kumpokea ili na yeye aende kumhudumia Baba ambaye alikua anaumwa.
Ni kama walimsikiliza tu lakini hata hawakujali kama alikuwa anaongea. Hata chakula cha usiku ambacho alipika Mama hawakula, waliondoka na Mume wangu na gari na kurejea usiku wa manane.
Asubuhi Mume wangu alikuwa anamuwahisha Mama stend ya mabasi Ubungo ili kupanda magari ya kumrejesha moshi. Nilijitahidi kuamka kumsindikiza hata mpaka getini, nilijizuia kulia lakini nilishindwa, machozi yalikuwa yananitoka tu.
Lakini nilishangaa wifi zangu nao wanatoka, mwanzo nilijua wamekuja kumsindikiza Mama, lakini pia Mama mkwe naye alitoka, hapo nilipata na wasiwasi kidogo, bado kulikuwa na kigiza giza lakini taa ya nje zilimulika vizuri tu.
“Unafikiri tutakuacha uondoke bila kukukagua?” Mama mkwe aliongea kwa hasira huku akimnyang’anya mume wangu begi la nguo la Mama alilokuwa akitaka kulipandisha kwenye gari. Nilishtuka, hata mume wangu alishtuka.
“Mwanangu huyu mwanamke mchawi, nimekuambia miaka yote huyu ndiyo alikuwa anawafanya msipate mtoto mnakuwa hamnielewi. Ukimuacha akiondoka hapa hata huyo mtoto hatazaliwa, ni lazima tuangalie begi lake asijekuwa ameondoka na kitu, anaweza hata kuwachota unyayo huyu!”
Mama mkwe alipongea kwa hasira huku akifungua begi la Mama. Nilishindwa kujizuia na kumgeukia mume wangu, nilitaka kunyanyua mdomo lakini nilishindwa, mume wangu ni kama alielewa nilichokuwa nataka kuongea.
Alimfuata Mama yeke kutaka kumzuia asifungue Begi la Mama lakini wifi zangu walimshikilia. “Kaka muache anakuokoa maisha yako na mwanao! Au hutaki mtoto?” Wifi yangu mmoja aliongea, mume wangu hakumsikiliza alijaribu kujitoa mikononi mwao lakini walimshikilia kwa nguvu.
Alifanikiwa kuwachomoka lakini mpaka anamfikia Mama yake tayari alishafungua Begi na kuchambua nguo. Alitoa mfuko mweusi na kuanza kuufungua. Hiki nini? Hiki nini? aliuliza kwa hasira, nilimuangalia mama ambaye alikuwa anashangaa tu.
Ule mfuko, ulikuwa na vitu kama hirizi na mchanga, nywele na mapuvu ya sabuni. Alimnyooshea Mama na kumuambia, wewe mchawi hiki nini sema, mchanga wa nini huu, na haya madudu ya nini? hizi nywele ni za nani na unapeleka wapi?
Wote tulibaki na mshangao, Mama ndiyo kabisa alikuwa hata hajui nini kinaendelea alishindwa hata kunyanyua mdomo. Mume wangu alimgeukia Mama kwa hasira na kuanza kumkunja kama vile anataka kumpiga.
“Unajifanya unakuja kunisaidia kumbe umekuja kuniloga, leo utaniambia huo mchanga ni wanini na hizi nywele ni za nani? Kila siku nahangaika kutafuta mtoto…!” Mume wangu aliongea kwa hasira, uso kaukunja, amenyanyua mikono kutaka hata kumpiga Mama.
“Mama yangu si mchawi! Hivyo ni vitu mmemuwekea!” Niliongea kwa hasira huku nikimfuata mume wangu na kumshika ili asimpige Mama,. Lakini mume wangu alinisukuma kwa nguvu, nilikosa balansi na kudondoka chini!
Nilidondokea mgongo lakini ghafla nilianza kuhisi nguo yangu ya ndani inaloa, kisha nikahisi kama nimekalia maji na nilianza kusikia maumivu makali sana tumboni. Bila kujijua nilijikuta napiga kelele nakufaaa! Hapo ndipo nilimshtua mume wangu ambaye alimuachia Mama na kunisogelea pale chini.
Umemfanya nini mwanangu! Umemfanya nini mwanangu umeniulia mjukuu wangu! umeniulia mjukuu wangu! Mama alipiga kelele huku akimsukuma Mume wangu na kunifuata pale chini, bado nilikuwa nikipiga kelele maumivu yalizidi…nilihisi kitu kibaya!
MAMA MKWE; NIHERI UNGENIUA MIMI—SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Mume Wangu Aliniambia Mama Yake anakuja kunihudumia hivyo nimfukuze Mama yangu ambaye alikuwa ananihudumia tangu nikiwa na ujauzito wa miezi, minne. Wakati Mama anaondoka walimvamia na kutoa vitu kama hirizi katika begi lake.
Wakati wakibishana mume wangu alinisukuma chini nikajikuta naanza kulowa. Wote walinifuata pale chini…ENDELEA
Niliendelea kupiga kelele za maumivu, Mama alinisogelea lakini Mama mkwe hakutaka, walimshika na wifi zangu na kumrusha pembeni. “Ondoka usije niulia mjukuu wangu!”
Mama mkwe aliongea kwa hasira, roho iliniuma, maumivu niliyopata kutokana na kitendo alichofanyiwa Mama yangu yalikua ni mara mia kuliko maumivu ya tumbo niliyokua nikiyasikia, nilitamani kunyanyuka kumtetea lakini sikuwa na nguvu.
Mtoto anatoka! Nilijikuta napiga kelele, kweli nilikuwa katika uchungu na nilishahisi Mtoto anatoka, mume wangu kwa kushirikiana na ndugu zake walininyanyua mpaka chumbani, Mama alitaka kuja lakini walimfukuza.
“Sitaki umsogelee mke wangu, ukimsogelea nakuua!” Mume wangu alimfokea Mama ambaye alibaki nje kaduwaa, waliingia ndani na kufunga mlango wa sebuleni wakimfungia Mama nje.
******
Sijui ni kwakuwa akili yangu ilikuwa kwingine au ni Mungu tu aliamua kunifanyia wepesi lakini nilijifungua haraka sana, sikupata maumivu yoyote wakati wakujifungua nilistuka tu mtoto yuko mikononi mwangu analia.
Baada ya kupumzika kidogo, mume wangu alitaka kunipeleka hospitalini na mtoto, lakini Mama yake alikataa, akasema kilichotokea ni ishara mbaya hivyo ni lazima mimi na mtoto tusafishwe kwanza.
Sijui mume wangu alikuwaje lakini alikubali, walimchukua mtoto na kuingia naye bafuni, sijui kama walimfanyia nini lakini walikaa naye kama nusu saa hivi kisha kutoka naye akiwa msafi na tayari wameshamfunga kitambaa cheusi shingoni na kiunoni.
Nilitaka kusema lakini mume wangu alininyamazisha akiniambia hiyo ilikuwa ni kwaajili ya usalama wetu. Mama mkwe aliniambia niingie bafuni, nilitaka kukataa lakini mume wangu alinilazimisha.
Niliingia kwa shingo upande, akili yangu yote ilikuwa inamuwaza Mama, kule bafuni walishaniwekea maji lakini hayakuwa ni maji ya kawaida. Yalikuwa maji meusi kama vile lami, Mama mkwe aliniambia nikae aniogeshe lakini niligoma.
Wifi zangu waliiingia na kunishikilia kwa nguvu kisha wakanimwagia yale maji kuanzia kichwani mpaka chini, wakati ananimwagia Mama mkwe aliongea maneno ambayo siyaelewi huku akisema. “Wamekufunga sana! Wamekufunga sana! Tusingewahi hata huyu mtoto asingezaliwa!”
Muda wote walikuwa wakimponda Mama yangu wakimuita mchawi na kunipa moyo mimi kwamba nitakuwa sawa na watanipenda kama mtoto wao. “Huna haja ya kuwasiliana tena na yule mwanamke, alikufunga uzazi yule!” sikuwa na cha kuwajibu zaidi ya kulia tu.
Walimaliza kuniogesha na maji yao kisha wakanisuuza na maji ya kawaida. Wifi zangu walitoka na Mama mkwe akaanza kunikanda taratibu, nilitamani kuongea lakini nilishindwa ni kama kuna kitu kilinikaba kwani nilikuwa na hasira sana.
Baada ya kumaliza kuoga mume wangu aliniambia nijitayarishe twende hospitalini, nilifanya hivyo na wakati natoka nilimuona Mama yangu kajikunyata pale nje na mabegi yake.
“Usijali nikirudi namuondoa huyu! Najua ni Mama yako ila alichotaka kutufanyia hapaswi kusamehewa! Asingekuwa Mama yako ningemuulia mbali kabisa!”
Mume wangu aliniambia wakati tunampita Mama, nilikuwa nalia tu, hata Mama alipotabasmau na kunipungia bado nilishindwa kunyamaza, sijui ni nini kilikua kimetokea mpaka mume wangu kuamini mambo yale ya kishirikina.
Nikiwa njiani nilichukua simu na kumtumia meseji Binamu yangu mmoja ambaye alikuwa Dar, hatukuwa na ukaribu sana lakini yeye ndiyo alikuwa ndugu pekee ninayemfahamu Dar, nilimuambia.
“Usipige wala nini acha chochote unachokifanya nenda nyumbani kamchukue Mama, atakuambia kila kitu, nimeshajifungua.”
Nilimtumia meseji na dakika mbili hivi alijibu “Poa”, hapo ndipo nilipata ahueni kidogo kujua kuwa Mama angalau atakuwa katika mikono salama. Hospitalini tulipokelewa vizuri, nililazwa na baada ya vipimo tulionekana wote tuko vizuri hakuna tatizo lolote.
Siku ile ile mimi na mwanangu tuliruhusiwa, nilirudi nyumbani sikumkuta Mama, nilishukuru Mungu kwamba alishachukuliwa. Ilipofika jioni binamu yangu alinitumia meseji “Niko na Mama, pole mdogo wangu yataisha tu”.
Nilimshukuru na kumuambia asiwasiliane na Mimi kwani sitaki wajue Mama yuko wapi wanaweza kumdhuru. Sikutaka hata yeye aje pale nyumbani mpaka nitakapofikiria nini cha kufanya kwani sikutaka kuishi na wale watu lakini sikuwa na namna mtoto alikuwa bado mdogo.
Cha kushangaza hata mume wangu hakumuulizia Mama baada ya kurejea na kumkosa, ni kama alifurahi kuona kwamba ameondoka bila kujali kaenda wapi?
*****
Kule ndani nilikuwa kama mfungwa, kila wakati wifi zangu walikuwa wananichunga, kibaya zaidi ni kuwa karibu mara zote walikuwa na mtoto, mimi nikiwa ndani walimchukua na alienda kulala kwa Mama mkwe mpaka pale alipohitaji kunyonya.
Nilivumilia nikisubiri wiki mbili za Mama mkwe ziishe ili aondoke na mimi kuchukua nafasi yangu. Lakini siku moja mwanangu alianza kulia sana, alilia mpaka niliogopa, lakini Mama mkwe hakuwa na wasiwasi.
Alimchukua na kuondoka naye lakini bado hakunyamaza, aliendelea kulia. Ilibidi kumchukua na kutaka kumnyonyesha tena lakini hakunyonya, nikiwa nimembeba alianza kujisaidia, sasa cha ajabu alijisaidia kama vile anabanwa.
Mtoto wa wiki moja na siku tatu alianza kujisaidia vitu vyeusi huku akijisaidia kwa uchungu kwani alikuwa analia sana kama vile anaumia. Nilishangaa sana yeye kujisaidia vitu kama vile kwani alikuwa hajaanza kula kitu chochote zaidi ya maziwa.
Nilitaka kumpeleka hospitalini lakini Mama mkwe alikataa katakata akisema nimuache mjukuuu wake atapona, yeye anajua nini cha kumfanya. Sikutaka kumsikiliza, nilimpigia simu mume wangu na kumwambia ambapo aliniambia muache huyo ni Mama yangu anajua nini chakufanya.
Nilivumilia kwa uchungu, nikiwa na wasiwasi sana tofauti na wenzangu ambao hawakuwa na wasiwasi kabisa. Mama mkwe alimchukua tena na kwenda naye huko chumbani kwake, alirudi ameshalala akaniambia unaona kashalala hana shida huyu.
Kweli nilitulia kidogo mpaka mume wangu aliporejea nikamwambia. Akaniambia nisiwe na wasiwasi nimuamini Mama yake kwani kama aliweza kumtunza yeye mpaka kawa mkubwa hatamshindwa kumhudumia mjukuu wake, kwa shingo upande nilivumilia.
Lakini usiku mtoto alianza kulia tena, sasa alikuwa akilia huku akiharisha vitu vyeusi kama lami, alilia sana mpaka mume wangu naye aliogopa. Mama mkwe alikuja akasema ni dawa ambazo alimpa hivyo tusiwe na wasiwasi ndiyo zinamfanya aharishe.
****
Mume wangu alitaka kukubali maneno ya Mama yake lakini niliona ujinga, yule ni mtoto wangu na kama akifa basi mimi ndiyo nitapata hasara si Mama mkwe wala ndugu zake, mimi ndiyo nilimbeba miezi tisa tumboni.
Ghafla nilinyanyuka na kumchukua mtoto wangu, nilichukua pochi na kumwambia mume wangu aniendeshe twende hospitalini, alikataa akisema tumsikilize Mama, nikamuambia yule ni Mama yake si Mama yangu, amsikilize yeye na si mimi.
“Kama unampenda sana ni wewe lakini si mimi! Huyu ni mtoto wangu nampenda kuliko ninavyokupenda wewe na nampenda kama Mama yako anavyokupenda, ni jukumu langu kumlinda na sitaruhusu kupangiwa!
Mama yako anaweza kukupangia maisha wewe lakini si mwanangu, hajui hata nusu ya niliyopitia mpaka kumpata! Naondoka mwenyewe kwa miguu kama hutanisindikiza ni wewe lakini huwezi kunizuia!’
Niliongea kwa hasira, mume wangu alijua natania, alinisogelea kutaka kunishika lakini nilimkwepa, nilichukua pasi iliyokuwa kwenye meza na kupigia chini kwanguvu ikapasuka pasuka!
Sitaki mtu aniguse nimechoka ujinga wenu, nitaua mtu kabla hamjamuua mwanangu! Kila mtu alishangaa mume hakuongea chochote, alichukua ufunguo wa gari na kunisindikiza, tukatoka tukiwaacha Mama mkwe na wifi zangu pale.
Tulienda mpaka hospitalini, kule mtoto alikuwa amezidiwa, halii tena, nilimshika mapigo ya moyo yalikuwa vizuri, tulipokelewa na manesi waliuliza nini kimetokea nikawaambia tu kuwa analia.
Kwa bahati nzuri mume wangu alikuwa anafahamiana na daktari wa zamu, hivyo mtoto alichukuliwa mara moja, alikuwa hapumui vizuri, aliwekewa mashine ya oxygen na kufanyiwa vipimo.
Walikaa huko kama masaa mawili bila kutoka, tulianza kuwa na wasiwasi, mimi na mume wangu tulikuwa hata hatusemeshani. Kila mtu alikuwa anawaza kivyake huku nikilia, sikutaka hata aniguse.
“Huyu mtoto mnampa nini?” Ilikuwa ni sauti ya Daktari. Wote tulinyamaza, tukiangaliana hakuna aliyekuwa na cha kujibu. “Mnataka kumuua huyu mtoto…” Daktari aliongea huku akituangalia, alikuwa anafahamu namna tulivyohangaika kupata mtoto.
“Unajua mtoto mdogo hatakiwi kula chochote zaidi ya maziwa ya Mama, lakini vitu mnavyompa ni kama mnataka kumuua… Mtoto wenu utumbo umeoza kabisa…Lameck ni upuuzi gani huu mnafanya…”
Aliongea kwa hasira akituangalia, lakini kabla ya kutuelezea alikuwa anamaanisha nini Nesi alitoke na kumuita, alinekana kuwa na wasiwasi akitetemeka kwa uoga “Daktari njoo mtoto amezidiwa…”
Daktari alituacha na kuanza kukimbia kuelekea wodini, mimi na mume wangu tulikimbia kumfuata lakini tulipofika nesi alituzuia, haturuhusiwi kuingia…ilibidi tubaki nje huku nikilia kwa uchungu sikujua nini kimetokea kwa mwanangu…
MAMA MKWE; NIHERI UNGENIUA MIMI—SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA; Mwanangu alianza kulia usiku na kumpeleka hospitalini, Daktari alianza kumlaumu Mume wangu kutokana na hali ya mtoto. Kabla hajatuambia nini kinaendelea aliitwa na nesi kuwa mtoto kazidiwa na kwenda ndani.
Sisi tulizuiwa kuingia hivyo kubaki tukichungulia dirishani….ENDELEA….
Pale nje mimi nilikuwa nalia tu, mume wangu aliniangalia kwa uoga, hakutaka hata kunisogelea, alionekana kuwa na mawazo yake. Mara nesi alifungua mlango na kutuambia tuingie, kilikua ni chumba cha Daktari si wodi.
Mwanangu alikuwa amelala kitandani, Daktari ambaye ni kama rafiki wa familia alituangalia kwa hasira sana, kisha akatusogeza kumuangalia mtoto, walishamtoa mipira ya Oxygen waliyomuwekea mwanzoni na alionekana kama amelala.
“Mmeona mlichofanya, mnampa nini huyu mtoto unaona haya madude ndiyo yatamuua.” Alionge kwa hasira huku akituonyesha vitu vyeusi kwenye kitambaa kikubwa cheupe, kama kataulo flani, walionesha kumfutia mwanangu.
“Ni nini hicho?” Mume wangu aliuliza kwa mshangao. Lakini hata kabla Daktari hajajibu chochote, mwanangu alianza kulia huku akikohoa mfululizo kama mtu aliyekuwa anapaliwa.
Kusema kweli alikuwa anaumia, kwa umri mdogo kama ule, katoto kadogo hakana hata sehemu ya kushika alikuwa anaumia sana. Hata mume wangu hakuweza kuvumilia alianza kulia kama mtoto, nilitamani kuchukua nafasi yake pale kitandani.
Watoe nje, daktari aliamrisha na nesi alianza kutuambia tutoke. Sikutaka muone lakini nimelazimika kuna vitu mnampa huyu mtoto na ni vibaya, ni kama acid flani ambayo inakula utumbo wake, harufu inayotoka tumboni ni kama kumeoza tayari, haya si maziwa ya mama.
Utumbo wa mtoto bado haujakomaa, kama ilivyo viungo vingine sasa mkimpa mavitu ya ajabu ndiyo anakua hivi. Daktari aliongea,. Alinishika na kunisukuma ili nitoke, bado mtoto alikuwa anakohoa tena kwa nguvu na sasa kama mtu mzima.
Lakini hakuna kitu kilikuwa kikitoka tena, nikama vile kikohozi kikavu. “Unampa nini mtoto?” mume wangu alinuliza bada ya kufika nje, sikua na jibu kwani tofauti na kumnyonyesha sikuwahi kumpa kitu chochote tangu azaliwe.
Isitoshe ningempea wapi wakati muda wote alikuwa na ndugu zake, mimi ndiyo nilikuwa Mama yake lakini nilipangiwa hata kumbeba, sijui nini kiliwashika lakini ni kama waliamini kuwa hata mimi nitamloga mwanangu mwenyewe ambaye nilihangaika sana kumtafuta.
******
Baada ye mtoto alitulia kidogo, Daktari aliniruhusu nikamnyonyeshe lakini hakunyonya kabisa, alionekana kuwa na njaa lakini alikosa nguvu hata ya kuvuta maziwa, ilibidi kukamulia maziwa na mtoto kupewa kwa kijiko na hapo ndipo alipata nguvu na kulala.
Nilijikuta napitiwa usingizi, tulihamishiwa wodini hivyo mimi nikabaki na mtoto na mume wangu akaambiwa aondoke. Lakini hakuondoka, kama mimi alikuwa na wasiwasi sana hivyo alibaki ndani ya gari, mpaka asubuhi kulipopambazuka ndipo alikuja kutuangalia.
Alikuja kuniuliza aniletee nini kwa maana ya nguo za kubadilisha na nguo za mtoto. Lakini kabla hata hajaondoka Mama yake na wifi yangu mmoja walikuja. Kuna vitu walileta lakini sikua hata na hamu ya kugusa vitu vyao.
Walikuja kistaarabu na kusalimia vizuri, ingawa nilikuwa na hasira lakini nilisalimia tu, mwili ulikuwa umechoka sana na akili yangu ilikuwa kwa mwanangu, sikutaka hata kuwaangalia achilia mbali kuwawaza na kuwaweka akilini mwangu.
Walimuita mume wangu nje na kuongea naye kidogo, kisha wakarudi. Sijui nini kilimtokea mume wangu au nini walimuambia lakini baada tu ya kuongea na Mama yake na kurudi alibadilika kabisa hakuwa yule mwanaume niliyekuwa nikiongea naye dakika tano zilizopita.
“Mama amemletea mtoto dawa…” Aliongea taratibu huku akinisogelea, alikaa pembeni yangu na kuwa kama anataka kunielewesha kitu, Mama yake alikuwa akiniangalia kwa wasiwasi, hasira zangu za jana yake zilimfunza kitu.
Nilimuangalia mume wangu na kumuona kama kichaa flani, sikutaka kumuelewa kwani ni wazi madawa ya Mama yake ndiyo yalitaka kuniulia mwanangu na sasa naona kama bado wanataka nimpe mwanangu ujinga wao.
“Kama ni madawa akupe wewe mtoto wake lakini huyu wa kwangu Mama yako hamgusi labda niwe nimekufa na hata nikifa nitatoka kaburini lakini Mama yako hatamgusa mwanangu tena!”
Sijui ni nini kilinipata lakini niliongea kwa sauti ya chini kabisa, nikiwa nimetulia, sina hasira huku nikitabasamu. Mume wangu na Mama yake walinishangaa, alijaribu kuniambia na kunibembeleza lakini sikujibu chochote niliendelea kuwaangalia tu kama machizi mpaka wakaanza kuogopa.
“Iko wapi hiyo dawa?” Niliuliza baada ya kukaa kimya kwa kama dakika tano. Wifi yangu akijua nimebadilika alinisogezea mfuko ambao pia ulikuwa na chupa ya uji, sikusubiri aitoe ile dawa, sijui nini kilitokea lakini nilimnyang’anya ule mfuko.
Ghafla niliitoa ile chupa ya chai na kuinyanyua juu kwa nguvu nikaipiga chini, ikapasuka, uji ukamwagika na kumrukia wifi yangu ambaye alikua karibu. Alipiga kelele za kuungua lakini sikujali, niliuchukua ule mfuko wenye dawa na kumpiga nao Mume wangu.
Ondokeni na Dawa zenu na narudia Mama yako hatamgusa tena mwanangu mpaka nakufa, hata wewe hutamgusa! Nimevumilia ujinga wenu lakini sasa ni mwisho, nitamlinda mwanangu hata kama ni kwa damu yangu!
Nilikuwa na hasira ambazo sijawahi kuwa nazo katika maisha yangu, hata mume wangu aliogopa na alikuwa anatetemeka kwa uoga, sura yangu ilibadilika na nilikuwa tayari kwa lolote. Sijui nilitoa wapi huo ujasiri lakini nilisimama kwaajili ya mwanangu.
Kabla hawajajibu chochote Daktari alikuja, lakini kabla hata hajauliza nini kilikuwa kimetokea mwanangu alianza kukohoa tena, haku akilia lakini alikuwa kama amepaliwa na mapovu yalikuwa yakimtoka mdomoni huku akikohoa sana.
Daktari alituamrisha kutoka nje, na kisha yeye kuendelea kumtibu. Tulikaa nje kwa muda na sasa hatukusikia tena sauti za mtoto akilia wala kukohoa, nilipumua kidogo nikimshukuru Mungu nikiamini mwanangu alikua amepona kidogo.
Lakini ghafla Daktari alitoka, alionyesha uso wa kukata tamaa, uso wa huzuni, ingawa alikuwa anajilazimishia kutabasamu lakini nilijua kuna kitu. Nilikimbia kutaka kuingia mule chumbani lakini nilizuiwa, Daktari aliomba kuongea na Mume wangu ofisini kwake.
Walikaa ofisini kwa muda wa kama dakika kumi hivi ndipo nilisikia sauti ya Mume wangu akilia kama mtoto mdogo. Nilijua nini kimetokea, bila hata kuambiwa nilitaka kunyanyuka kukimbia ndani kumuangalia mwanangu lakini miguu haikunyanyuka, nilidondoka na kupoteza fahamu.
****
Nilizinduka nusu saa baadaye, ni kweli mwanangu alishafariki na hakuna kitu ambacho ningekifanya zaidi ya kulia. Sikutaka kuongea na mtu yeyote zaidi ya Mama yangu ambaye alikuja mida ile ile baada ya kupata habari.
Kusema kweli nilichanganyikiwa, akili haikukaa sawa na katika kipindi cha wiki mbili sikujua hata ni nini kilikuwa kinaendelea mule ndani, mpaka baadaye niliporudi katika hali ya kawaida, ndipo nilipopata sababu kamili za kifo cha mwanangu.
Baada ya kupimwa na matapishi yake kupimwa iligundulika kuwa alikuwa akipewa madawa makali ambayo yalikwangua mpaka kuozesha utumbo wake. Sikujua saa ngapi lakini niligundua kuwa kumbe Mama mkwe wangu alipokuwa akimchukua na kukaa naye alikuwa akimpa vitu.
Lengo lao lilikuwa ni kumlinda na wachawi, ni dawa ambazo walipewa huko kwao ili kumpa mtoto wakiamini kuwa bila hivyo basi tungempoteza kwakuwa tulimtafuta kwa shida sana.
Mume wangu naye alishazinduka, aliwafukuza Mama yake na Dada zake akiwalaumu kwa kumuulia mtoto, kule ndani kulikutwa na madawa mengi ya kienyeji na mahirizi.
Baada ya kubanwa na mume wangu kufuatilia ndipo alipogundua kuwa kumbe hata kufukuzwa kwa Mama yangu lilikua ni jambo la kupangwa, kwani alikuwa kikwazo kikubwa kwao.
Mama ni mtu wa maombi sana na mara nyingi kumbe mama mkwe wangu alitaka kuja mule ndani lakini kuna nguvu flani zilikuwa zikimzuia. Ndipo mganga wake akamuambia kuwa kama anataka kumuona mjukuu wake basi Mama yangu aondoke ndiyo na yeye anaweza kuishi na sisi.
Dawa alizopewa zisingeweza kufanya kazi mbele ya Mama yangu. Alichofanya ni kumuambia tu kuwa Mama ndiyo mchawi hivyo inabidi kuondoka kwanza.
Mume wangu naye alishatengenezwa ndiyo maana alikuwa anawaamini na kuwasikiliza sana. Mama bado alikuwa pale akiniangalia mpaka niliporudia katika hali nzuri ndipo aliondoka, mume wangu aliniomba msamaha sana kuwa hazikuwa akili zake.
Kusema kweli nimeshamsamehe lakini siwezi hata kumgusa, ni mwaka sasa naishi nyumba moja na mume wangu lakini kila nikijaribu kumgusa picha ya mwanangu akitapika hospitalini inanijia.
Najitahidi sana kusahau lakini nimeshindwa, bado mume wangu ananivumilia na hayuko tayari sisi kuachana. Sijui ni kwa namna gani naweza kusahau na hata kuendelea na maisha yangu lakini baada ya kuongea na watu mbalimbali wanasema mimi na Mume wangu tunapaswa kuwasamehe ndugu zake kwanza ndiyo na sisi tujisamehe.
Sijui kama itawezekana kwani hata mume wangu hataki kuwasikia, kwa mambo waliyotufanyia ni ngumu sana kusahau lakini bado namuomba Mungu kwani maisha ni lazima yaendelee.
Nimeamua kundika kisa changu kwakuwa nafahamu kuna watu wengi hupitia machungu na magumu kuliko yangu. najua kuwa kuandika itawasaidia wengi hasa sisi wanawake, kwamba niwajibu wetu kuwalinda wenetu.
Si lazima kusikiliza kila kitu na kukubaliana na kila kitu unachoambiwa na mume wako au wakwe zako bila kupima manufaa yake. Wewe ni binadamu sio mnyama hivyo unatakiwa kusikilizwa pia. Naamini mmejifunza kutoka kwangu, Mungu awabariki kwa kusoma kisa changu.
****MWISHO****
0 comments:
Post a Comment