Search This Blog

Tuesday, June 21, 2022

SITAMANI KUFA LAKINI SITAKI KUISHI

  

IMEANDIKWA NA IDDI MAKENGO

NDOA YA MAUTI; SITAMANI KUFA LAKINI SITAKI KUISHI — SEHEMU YA KWANZA


“Dada huyo ni mume wako kweli?” Aliniuliza kijana mmoja ambaye alikuwa pale dukani. Nilimuangalia kwa wasiwasi nikataka kudanganya niseme labda ni bosi wangu lakini nilikumbuka wakati ananitukana alisema “Najuta kuoa mwanamke mbinafsi kama wewe! Unawatesa sana ndugu zangu!”


JOIN US ON TELEGRAM

Nilitaka pia kutokumjibu kwani yalikuwa hayamuhusu lakini alikuwa amenunua vitu vingi na kwa muonekano wake angekuwa ni mteja wa kudumu.


“Ni mume wangu ndiyo” Nilimjibu kwa kifupi huku nikijifanya niko bize kumuandikia risiti, sikutaka aendelee kunichunguza. Aliniangalia kwa huruma huku akitingisha kichwa kusikitika.


“Wanawake mnavumilia mengi sana…” Aliongea kwa masikitiko huku akipokea risiti niliyokuwa nikimkabidhi. Tayari vijana wangu walishamaliza kupakia mizigo aliyokuwa amenunua kwenye gari aliyokuja nayo aina ya Toyota Double Cabin.


Aliwakabidhi hela ya kupakia kisha akaingia kwenye gari na kuondoka zake. Nilimuangalia wakati anaondoka huku nikimshukuru Mungu uwepo wake pale kwani nina uhakika kama asingekuwepo basi siku ile ningechezea makofi. Mume wangu aliona aibu kunipiga mbele ya mwanaume mwenzake tena akiwa hamfahamu


Siku yangu ilianza kuharibika asubuhi, wakati nimeenda kuchukua vifaranga nilimuacha wifi na mfanyakazi pale dukani, niliporudi sikumkuta wifi yangu na nilipomuuliza mfanyakazi aliniambia aliondoka pale tu nilipoondoka na kusema anaenda Kariakoo.


Sikuwaza sana kwani ilikuwa ni kawaida yake alikuwa akifanya kazi anavyojitakia. Nilikasirika pale alipokuja Mama John mteja wangu mkubwa, nilimuambia mfanyakazi wangu kumpa shilingi laki tatu nilizokuwa nimemuachia asubuhi wakati naondoka ili Mama John akija kama sijarudi ampe.


“Dada amezichukua, amesema kuna vitu anaenda kununua mjini..!” Alinijibu akimaanisha wifi yangu kazichukua zile pesa. Hasira zilinipanda kwani wakati ule sikuwa na hata shilingi mfukoni, hela zote nilinunulia mzigo na Mama John ni mteja wangu wa muda mrefu, ilinilazimu kukopa kwa jirani na kumkabidhi huku nikijifanya hakuna kitu kibaya kilichotokea.


Haikupita nusu saa wifi yangu alirejea, hata kabla sijamsemesha alitoa maronya ronya ya nguo aliyonunua huko mjini na kuanza kumuonesha mfanyakazi na wamama wengine. Nilijua alikuwa anafanya makusudi ili niongee hivyo nilimuangalia tu bila kusema chochote.


Sikutaka watu wajue nimekasirika hivyo alipomaliza na kuingia dukani bila kusema chochote nilitulia mpaka mfanyakazi alipotoka ndipo kistaarabu nilipomuuliza mbona amechukua pesa za mteja wakati akijua hatuna pesa, pesa yote tulienda kununulia mzigo, angalau hata ungeniambia nijue cha kufanya.


Aliniangalia kwa dharau kisha akasema.


“Kwani pesa ni zakwako, hizi mali ni za Kaka yangu na yeye nilimuambia akaniambia nichukue..”


“Hata kama lakini ungeniambia na mimi…”


“Bibieee! Nikuambie wewe ili? Hizo zote unazopeleka kwenu unatuambia? Mfyuuuu! Au unafikiri hatujui?”


Alisonya kwa nguvu, nilinyamaza tu bila kusema chochote. Ukimya kidogo ulitawala, ni kama alitaka niongeee lakini sikunyanyua tena mdomo wangu, alianza kuongea maneno yake ya kashfa, kusema sema na kusengenya lakini sikujibu chochote. Kuona vile alichukua nguo zake na kuondoka bila hata kuaga.


Jioni sasa baada ya mume wangu kutoka kazini ndiyo akaja pale, kakunja ndita na mihasira yake akisema ninamnyanyasia ndugu zake. Alinitukana matusi ya nguoni mbele ya wafanyakazi na wateja, nilimsikiliza bila kumjibu kwani nilijua nikinyanyua tu mdomo ni kipigo.


Hilo nalo lilikuwa kosa kuwa nina kiburi simjibu, simuongeleshi nina dharau na mambo kama hayo. Hata hivyo sikuongea, nilibaki tu kimya mpaka akaona kama anajichora akaondoka.


*****


Maisha yetu hayakuwa hivyo, baada ndoa maisha yetu yalikuwa mazuri, wakati huo ndiyo nilikuwa nimemaliza kidato cha sita, sikufaulu vizuri hivyo nilibaki nyumbani kwa kama miezi sita ndipo nilipoolewa na mume wangu ambaye alikuwa ni mhasibu.


Erick alikuwa akiishi nyumbani kwao, kama mtoto wa kwanza alichukua jukumu la kulea familia yao baada ya Baba yake kufariki. Alikuwa akiishi yeye Mama yake na wadogo zake wanne wawili wakike na wawili wakiume.


Mwanzoni mambo yalikuwa mazuri kidogo, Mama mkwe na wifi zangu ambao walikuwa wakubwa kidogo walinipenda, shemeji zangu walikuwa wadogo hivyo walikuwa wakiniheshimu na mpaka sasa wananiheshimu.


Lakini hali ya mule ndani haikunifurahisha, kila kitu tulikuwa tukimtegemea mume wangu na kama unavyojua mishahara ya serikali haitoshi.


Yani mimi, Mama mkwe ambaye hakuwa mzee sana, wifi yangu mkubwa ambaye alikuwa ameacha shule kidato cha tatu baada ya kupewa ujauzito na kutelekezwa na mwanae, wifi yangu mwingine ambaye alikuwa kidato cha nne na shemeji zangu wawili ambao mmoja alikuwa kidato cha kwanza na mwingine darasa la sita, tulikuwa ni kula na kulala tu.


Nilimuonea huruma mume wangu ndipo nilipo muomba mtaji wa kufanyia biashara, hapo ndipo mambo yalipoanza kuharibika. Alinipa mtaji wa shilingi laki moja (kipindi hicho laki moja ilikuwa hela nyingi kidogo) na nikaanza kuuza mayai ya kisasa kwa bei ya jumla na rejareja.


Nilitaka kufanya biashara ya mayai nikiwa na lengo la kufuga kuku kwani kabla ya kuolewa nilikuwa nikiishi na shangazi yangu (ndiye aliyenileta Dar)ambaye alikuwa akifuga kuku na niliona kiasi cha fedha alichokuwa akiingiza hivyo kutamani kufanya ile biashara kwani nilishapata kauzoefu kidogo.


Wakati huo huo nilijenga banda dogo la kuku pale nyumbani kwani kulikuwa na uwanja mkubwa na kuanza kufuga kuku wa mayai. Kila kitu nilikuwa nikifanya mwenyewe si Mama mkwe wala wifi zangu walionisaidia ingawa Mama mkwe na wifi mkubwa walikuwa tu pale nyumbani.


Wakati huo nilikuwa na ujauzito wa mtoto wangu wa kwanza. Baada ya kuanza biashara na kuanza kuingiza vipesa kidogo mambo yalibadilika, mwanzoni kazi za nyumbani tulikuwa tukisaidiana ila baada ya kuanza biashara kazi zote walikuwa wakiniachia mimi.


Sikuongea lakini kila siku Mama mkwe alikuwa akiongea kuwa kazi ya mwanamke ni kumuhudumia mume wake, alikuwa akiongea kwa mafumbo na mara kadhaa alimuonya mume wangu kuwa huyu mwanamke atakuja kukutawala akipata pesa.


Mwanzoni mume wangu alikuwa akipuuzia kwani kufanya kwangu kazi kulikuwa kukimpa unafuu wa maisha, angalau sasa aliweza kununua shati lingine kwani kusema kweli faida ilikuwa kubwa na namna nilivyokuwa naweza kuongea na wateja basi ilisaidia.


Pia shangazi yangu ambaye alikuwa mfanyabishara mkubwa aliniunganisha na baadhi ya wateja wake na mara kadhaa alikuwa akinikopesha mzigo mkubwa. Nilipata pesa na kujenga mabanda mawili makubwa na kuanza kufuga na kuku wa nyama.


Kazi zilinizidi ukichanganya na ujauzito ambao nilikuwa nakaribia kujifungua pamoja na ugumu wa kuhudumia kuku nilikuwa nahitaji msaidizi, nilimuomba wifi yangu anisaidie katika kuhudumia lakini alikataa akisema siwezi kumtumikisha kama mfanyakazi.


Niliongea na mume wangu ambaye alimlazimisha kufanya ile kazi kwani hakuwa akifanya kazi yoyote wakati alikuwa akila bure yeye na mwanae. Hilo lilizua balaa kubwa kwa Mama mkwe akisema nimemtawala mtoto wake namuendesha.


Maneno yalikuwa mengi kwakweli lakini nilivumilia kwani mume wangu alikuwa upande wangu, kila wakati aliniambia kuwapuuza tu. Na mimi nilimsikiliza hivyo niliyasikiliza maneno yao na kuyapuzia.


*****


Maisha yaliendelea na miezi tisa ilifika, sijui niseme kwa bahati mbaya au niseme tu kwa mipango ya Mungu nilijifungua kwa njia ya upasuaji hivyo nilitakiwa kupumzika, lakini nikiwa kitandani nahangaika na mshono kuku walianza kufa mmoja mmoja


Wifi yangu hakuwa akiwahudumia na kama mnavyojua kuku wa kisasa wakikaa na uchafu kidogo tuu basi wanakufa wote. Walianza kufa mmoja mmoja na ndani ya wiki moja kuku zaidi ya hamsini walikufa.


Cha ajabu hakuna aliyekuwa akijali hata mume wangu alikuwa hajali, kitu ambacho kilinishtua zaidi kuliko kile cha kuku kufa. Sikujua nini kilikuwa kimembadilisha mume wangu haraka haraka hivyo hasa baada ya mimi kujifungua, ni kama alikuwa hataki kujihusisha na mimi kabisa wala mtoto.


Taratibu nilianza kusikia maneno kuwa mume wangu alikasirika kwani mtoto hakufanana na yeye na kulikuwa na maneno kuwa mtoto si wake, mimi na mume wangu ni weusi lakini mtoto alizaliwa mweupe. Sikuwa na cha kusema lakini ukweli nilikuwa nikiujua mimi na Mungu wangu.


Nilivumilia ile hali na pamoja na mshono wangu nililazimika kunyanyuka na kuhudumia kuku wachache wa chotara waliokuwa wamebaki huku nikijipikia na kufua mwenyewe. Nilitamani hata ningekuwa na mdogo wangu wa kike ningemuita anisaidie kwani hawakuwa wakinisaidia chochote.


Nakumbuka mara kadhaa kidonda kilifumuka na kutoa damu lakini nilijikaza hivyo hivyo, ilikuwa ni lazima nifanye zile kazi kwani mbali na kuku lakini hata nguo za mtoto nilifua mwenyewe na nisingefanya hivyo angekosa za kuvaa, hata uji nilikuwa nikijipikia mwenyewe.


Kwa kifupi familia nzima ilinitenga na mume wangu alikuwa ni kama adui tu. Kumbuka huo ndiyo ulikuwa uzazi wangu wa kwanza hivyo nilikuwa sijui chochote. Siku pekee ambazo nilikuwa nikipumzika ni zile ambazo shangazi yangu ambaye naye alikuwa bize sana na kazi zake alikuwa akija kunisalimia.


Hapo hata wao walijifanya kunisaidia kazi na kucheka naye. Yeye ndiyo alikuwa ndugu yangu pekee Dar, wengine walikuwa kijijini, kama ambavyo nilifundishwa uvumilivu katika ndoa sikumuambia chochote na mimi niliigiza furaha.


Maisha yaliendelea lakini hali ilizidi kuwa ngumu, mume alikuwa hatoi pesa ya matumizi na kila nikimuuliza alisema pesa si ninazo na hawezi kutoa wakati hajui hata mtoto ni wanani? Sijui alilipata wapi hilo wazo lakini ndiyo ulikuwa kama wimbo mule ndani, yeye na ndugu zake walikuwa wakiongea kimafumbo kuhusu mwanangu.


Nilivumilia kwani nilijua kuwa ni wake na si wa mwanaume mwingine, ingawa mume wangu alizidi kuwa na hasira hasa mtoto anapolia. Aliongea akisema watoto wa kwao hawalii hivyo huku akiungwa mkono na Mama mkwe, kusema kweli nilichanganyikiwa na nilikuwa sijui cha kufanya.


Siku moja nikiwa katika banda la kuku nasafisha, kuku wote wa kisasa zaidi ya mia mbili wa nyama na wa mayai hamsini walikufa kipindi nimejifungua hivyo nilibaki na mabanda tu na kuku ishirini wa chotara.


Nilisikia kelele za mwanangu akilia kwa nguvu kisha akanyamaza ghafla, sijui kwanini lakini kilio kilikuwa ni tofauti kabisa na siku nyingine na kikubwa ukilinganisha na umri wake. Alilia tu ghafla kwa sauti ya juu na kunyamaza, kusema kweli nilikuwa sijawahi kumsikia akilia hivyo wala kusikia mtoto mdogo akilia hivyo.


Kama chizi nilinza kukimbia kuelekea chumbani nilikokuwa nimemlaza, nilikimbia kwa kasi ya ajabu na nguvu nyingi, mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, niliugonga sana huku nikiusukuma kwa nguvu, sikujua ni nani ameufunga kwani wakati natoka mume wangu alikuwa bado hajarudi.


Ndugu zake walikuwa hawaingii chumbani kwangu hata kama mtoto akilia namna gani? Kama sipo wanamuacha hivyo hivyo mpaka anyamaze mwenyewe, tofauti na shemeji zangu wifi na Mama mkwe walikuwa hawanisaidii chochote.


Nilipiga mlango kwa nguvu na kama dakika moja hivi ulifunguliwa, alikuwa ni mume wangu akihema kwa nguvu “Nini wewe mbona unataka kunivunjia mlango?” Aliniongelesha huku akinisukuma pembeni.


Alionekana kuwa na wasiwasi sana huku akiangalia angalia pembeni kama mwizi! Sikumjali nilikimbilia kitandani mwanangu alipokuwa amelala, neti ilikuwa imeondolewa, kitanda kimevurugika sana na mtoto amelala chali halii wala hasogei.


“Umemfanya nini mwanangu? Umemfanya nini mwanangu? Umemfanya nini mwanangu? Nilianza kupiga kelele huku nikimuangalia mapigo yake ya moyo kuona kama anapumua nilijikuta napiga ukunga kwa nguvu..!


Mwanangu alikuwa hapumui wala hajitingishi. Nilimuacha pale kitandani na kutaka kutoka nje kumkimbilia mume wangu ili aniambie kamfanya nini, lakini nilipofika mlangoni nilikumbuka namna ambavyo watu hufanya kwenye sinema pale ambapo mtu anakuwa hapumui.


Niliinama na kuanza kumpulizia mwanangu hewa mdomoni kwa kama dakika moja hivi lakini wapi hakupumua. Akili ilisimama kabisa sikujua nifanye nini, nilihisi kama mwanangu alikuwa amefariki, akili yangu ikiwaza kuna kitu ambacho mume wangu alikuwa amemfanyia.


Sikutaka kukata tamaa, nilimnyanyua juujuu na kumning’iniza kichwa chini miguu juu, kusema kweli sikuwa nikijua nafanya nini lakini nilikumbuka namna ambavyo mtoto anayezaliwa anapokuwa halii anavyofanywa, haikusaidia. Nilianza kuwa kama chizi sasa nikifanya kila kitu ambacho niliona kama kingemsaidia kupumua.


NDOA YA MAUTI; SITAMANI KUFA LAKINI SITAKI KUISHI — SEHEMU YA PILI


(ILIPOISHIA; Niliingia chumbani na kukuta mwanangu amelala hapumui, nilianza kumgeuza geuza huku nikimpumulia mdomoni ili anyanyuke…ENDELEA…)


Nilimgeuza geuza na ghafla nilisikia sauti ya kilio, kilikuwa kilio kama cha mara ya kwanza mtoto anapozaliwa, mpaka sasa sijui nilifanya nini mpaka akalia lakini nahisi ilikuwa ni miujiza tu ya Mungu.


Nilihisi nishampoteza mwanangu na nilijua mume wangu ndiye alitaka kumuua. Ningeweza kuvumilia vyote lakini si kumpoteza mwanangu, nilimkagua na kukuta yuko salama, aliendelea kulia, nilimnyanyua na kumbembeleza huku nikimshukuru Mungu kwa ule muujiza.


Kelele za kilio chake zilimstua mume wangu, aliingia kama anakimbia huku akihema kwa nguvu.


“Ameamka! Ameamka! Nilijaribu kumuamsha lakini hakuamka! Ahsante Mungu! Ahsante Mungu!” Alijiongelesha huku akinisogelea, alinyoosha mikono yake kutaka kumpokea mtoto lakini sikuruhusu, makusudi nilimkwepesha ili asimguse.


“Nini? Hutaki nimguse? Au sio mwanangu… sio wa kwangu huyu mtoto, sio wa kwangu!” Aliendelea kujiongelesha lakini sikumjibu, nilimuangalia kwa jicho la kumsuta na kwa aibu alitoka bila kuaga. Kusema kweli nilikuwa nimechoka na manyanyaso ya mule ndani na ilikuwa ni lazima kumuambia mtu la sivyo ningechanganyikiwa.


Nilimpigia simu shangazi yangu na kumuuliza kama yupo nyumbani, nilimuambia nataka kuonana naye kwani kuna mambo makubwa yametokea katika ndoa yangu. Niliongea huku nikilia, shangazi alishtuka kidogo kwani ilikuwa ndiyo mara ya kwanza mimi kufunguka kuhusu ndoa yangu.


Aliniambia aje kunichukua na gari kwani alikuwa dukani lakini nilikataa, nilimuomba tukutane dukani kwake ambapo ilikuwa ni gari moja tu ili twende nyumbani kwake kuongea. Alinikubalia na harakaharaka nilimuandaa mtoto na kuondoka bila kumuaga mtu yeyote.


Nilimpita Mama mkwe, wifi zangu na mume wangu pale sabuleni bila kusema chochote, sikujali kitu na hakuna hata mmoja aliyenisemesha. Inaelekea wote walishajua alichokuwa anataka kufanya mume wangu au ilikuwa ni mipango yao kwani walikuwa wakiniangalia kwa wasiwasi tofauti kabisa na kawaida yao.


*****


“Una ushahidi wowote kama alitaka kumuua?” Shangazi aliniuliza nilipomuelezea kila kitu kuhusu ndoa yangu na kilichotokea siku ile.


“Hapana shangazi ila nahisi tu, kwanini mtoto alie na akutulia, halafu kwanini afunge mlango. Kuna mambo mengi yanaendelea shangazi na yananipa wasiwasi sana. Lazima kutakuwa na kitu kibaya alitaka kumfanyia mwanangu”


“Mwanangu ndoa ni uvumilivu, huwezi kumshutumu mume wako mambo kama hayo..!” Shangazi aliongea kwa sauti ya juu kama vile ananifokea. Nilishtuka kwani nilitegemea kwa niliyomueleza atakuwa upande wangu.


“Shangazi sio kama namshutumu. Mume wangu kanifanyia mengi mabaya navumilia. Hili siwezi kuvumilia, isitoshe anasema mtoto si wake na nahisi hiyo ndiyo sababu ya kutaka kumuua?”


“Tema mate chini mwanangu, hayo unayonena ni makubwa! Mumeo hawezi kufanya hivyo na kama anasema mtoto si wake labda kuna vitu umefanya unanificha, mtu hawezi kuibuka na kusema tu mtoto si wake… lazima kuna kitu umefanya hutaki kuniambia”


Maneno ya shangazi yalinikatisha tamaa kabisa, nilishajiandaa kuondoka na kuanza maisha yangu upya bila ndoa lakini nilihitaji sehemu ya kuanzia. Nilimuomba shangazi kukaa pale kwa muda wakati nikijipanga lakini alikata akisema. Aling’aka na kuona kama nilikuwa nataka kufanya kitu cha ajabu sana.


“Wewe ni mke wa mtu, siwezi kukuruhusu kukaa kwangu tu! Unafikiri Baba yako atanielewaje akijua mimi ndiyo nimevunja ndoa yako? Tatizo kidogo unataka kuondoka, unajua sisi kuna mangapi makubwa tumepitia? Unafikiri kila mwanamke anayekorofishana na mume wake angeondoka kungekuwa na ndoa kweli?


Mume wako kama kakuchoka akurudishe kama alivyokuchukua, unafikiri ukikaa hapa wazazi wako watanielewaje? Kaka atanielewa kweli kama mimi ndiyo nakuendekeza! Hapana, rudi huko huko na kama mumeo akikuleta hapa nitakupokea lakini huwezi kuja tu mwenyewe nikakupokea bila mumeo eti ndoa imekushinda.


Tena na shutuma kama hizo! Hata wazee hawajashirikishwa! Hapana siwezi! Wewe ulikabidhiwa kwa mume hukujiondokea tu nyumbani kama kichaa! Maisha hayaendi hivyo mwanangu! Jifunze kuvumilia, ndoa zote zipo hivyo!”


Aliongea maneno mengi kiasi cha kushindwa kuendelea kumsikiliza tena, kusema kweli nilichanganyikiwa, nilibaki nimeduwaa nikiwa sina hili wala lile. Nilitamani hata kurudi kijijini lakini kila nikimuwaza Baba niliishiwa na nguvu, kama shangazi amekuwa mkali vile nilijua Baba angeniua kabisa.


Nikiwa nimenyong’onyea nilimbeba mwanangu, nikachukua na pochi langu na kuanza kurudi nyumbani kwa mume. Nilishakata tamaa na maisha na sikujua ningeenda wapi tena, shangazi alitaka kunisindikiza na gari lake lakini nilikataa, niliondoka na hasira zangu nikiwa nimechanganyikiwa.


*****


Nyumbani nilimkuta mume akiwa amefura, alionekana wazi kuwa na wasiwasi kutaka kujua nilikwenda wapi? Maswali yake yalilenga kujua nilikuwa wapi, nimeongea na nani na nimewaambia nini? Alijichanganya na kuongea mambo ambayo yalionesha wazi kweli alitaka kumdhuru mwanangu.


Pamoja na kwamba sikuwahi kuongea kama ametaka kumuua mtoto lakini alianza kusema mbona sitaki amguse mtoto, “Ina maana huniamini na huyo mtoto, unaona nitamdhuru, unafikiri naweza kumfanya nini? Unaniona kama mnyama, hivi unafikri nina roho mbaya kiasi hicho kumdhuru malaika kama huyu?


Au sio mwanangu na leo nasikia bwana yako alikuja hapa! Au ndiyo Baba wa mtoto..” Alijiongelesha lakini sikumjibu kitu ambacho kilimfanya anione kiburi. Maneno yake yalinifanya kujua hasira zake zilitoka wapi, mchana alikuja Mudi kijana ambaye alikuwa akinunua mayai kwangu kwenda kuyachemsha na kuyauza.


Ni muda tulikuwa hatujaonana hivyo tuliongea kidogo na wifi zangu walimuona nadhani hicho ndicho kilimpa hasira kwani Mudi alikuwa mweupe na nilishasikia mara kadhaa wifi zangu wakinong’ona kama ndiye alikuwa Baba wa mwanangu.


Sikuongea kitu na kule kukaa kwangu kimya kulimkera hivyo niliambulia kipigo cha kufa mtu. Pamoja na manyanyaso yote lakini ile ndiyo ilikuwa siku ya kwanza mume wangu kunipiga, nililia kwa nguvu kwani kipigo chake kilitonesha mshono, damu zilianza kutoka.


Alipoona damu aliniacha chumbani na kuondoka zake, wakati huo mwanangu alikuwa akilia kwa nguvu huku na mimi nikilia kwa maumivu. Nilijikaza na kwenda kumnyonyesha mtoto ili atulie lakini haikusaidia hakutaka kunyonya.


Nilichukua upande wa khanga na kuukandamizia kwenye kidonda ili kuzuia damu zisitoke. Nilijitahidi kunyanyuka na kuanza kumbembeleza mwanangu ambaye alikuwa akilia sana, nilikuwa katika maumivu makali lakini sikuwa na namna, hakukuwa na mtu wa kunisaidia.


Niliendelea kumbembeleza mpaka nikawa sijisikii maumivu tena, yaani niliyazoea, mwanangu alilala hivyo nikamlaza. Nilienda kusafisha kidonda na kukifunga vizuri na bandeji kisha kwenda kupika chakula cha usiku kwaajili ya familia, wifi zangu na Mama mkwe walikuwa sebuleni wakiangalia TV nilijua kama nisingepika mimi wasingepika na ingekuwa tabu nyingine, mume wangu hakurejea tena mpaka asubuhi.


*****


Mume wangu ni kama alionja asali na kuamua kuchonga mzinga kabisa, baada ya kunipiga mara ya kwanza ilianza kuwa kama tabia yake, kila akikasirika kidogo alikuwa akinipiga hata bila sababu na ndugu zake walikuwa wakishangilia wakiongea maneno ya mafumbo wakisema kama nimechoka si niondoke nasubiri nini pale? 


Lakini niliamua kuvumilia nikiamini ipo siku yataisha. Lakini hayakuisha yaliendelea kila siku mpaka nikaona kama kipigo ni sehemu ya maisha yangu, mwanangu alikuwa na Mungu alianza kuwaumbua. Kadri mwanangu alivyokuwa akikua ndivyo alikuwa akifanana na Baba yake.


Weupe ulikuwa ukiondoka siku hadi siku na alipofika miaka miwili alikwua anaelekea kuwa mweusi kama Baba yake, sura ya Baba yake ilichomoza usoni kwake kiasi kwamba hata mtu ambaye alikuwa hajui kuwa ni mtoto wake kwa kuona tu alisema wamefanana. Jambo hilo lilimpa aibu sana mume wangu akajirudi rudi ingawa manyanyaso hayakuisha.


Kutokana na maneno maneno ya mule ndani nilijikuta naelekeza nguvu zangu katika kufanya kazi, kutwa nzima nilikuwa kwenye kuku na biashara ilikubali. Niliacha biashara ya kufuga baada ya kupata mtaji nakufungua duka la kuuza vyakula vya kuku na vifaranga.


Hapo ndipo nilipoanza kuishika pesa ya kweli, biashara ilichanuka na ndani ya mwaka mmoja niliweza kununua gari pikapu na kiwanja nikimshauri mume wangu tuanze ujenzi ili tuondoke pale nyumbani lakini alikataa akisema tukarabati nyumba tuliyokuwa tukiishi kwanza.


Kwa kuwa yeye ndiyo alikuwa kila kitu nilimsikiliza. Lakini mafanikio yalikuja na changamoto, ndugu wa mume walianza maneno mengine wakisema mimi nawaloga ndiyo maana wao hawafanikiwi mimi nafanikiwa. Pia mume wangu ni kama alichoka kunipiga na kuninyanyasa, alirudisha upendo kidogo kitu ambacho kiliwaumiza vichwa.


Lakini waliumia zaidi pale walipogundua nina ujauzito wa miezi mitatu, ni muda sana mume wangu alitaka mtoto mwingine lakini nilijaribu bila kufanikiwa hivyo walipoona nina ujauzito walizidisha chuki kwani walijua Erick angezidisha upendo.


Tangu agundue ni mjamzito hakunipiga tena, hata akiwa na hasira vipi alijizuia akiishia tu kutukana huku akisema nina bahati nina mimba angenipiga mpaka kuniua. Kwao hilo waliona kama ni uchawi na kila siku waliibua kitu kipya kutaka kuonesha kama kweli mimi ni mchawi na sipaswi kuishi pale kwani nawaloga wao wasiendelee na namloga mume wangu asiwasikilize.


Walikua wakiamini kweli kama nawaloga na mara nyingi walilalamika kwa mume wangu ambaye kwa kuwa ni msomi alikuwa haamini sana hayo mambo. Hali hiyo ilizidi kuwakera na kila kitu kibaya kilipotokea walisingizia uchawi, amani iliyoanza kurejea ilianza kutoweka tena.


Kusema kweli ni kitu ambacho kilinishangaza kwani sijui ni namna gani wangefanikiwa kama wote walikuwa wakikaa tu nyumbani, kila kazi waliyokuwa wakitafutiwa walikuwa wakiharibu na hata kuja tu kukaa dukani wasingeweza kukaa kutwa nzima bila kutoka hivyo kulazimika kuajiri wafanyakazi wa nje.


Lakini haikuishia hapo, walikuwa wakiingia dukani kama kwao na kuchukua pesa tu bila taarifa na pale niliposema walisema ni pesa za kaka yao na kweli mume wangu aliwatetea na kuona kama nina wanyanyasa.


Siku moja nikiwa nimetoka dukani niliwakuta wote wakiwa wamekaa sebuleni, niliwasalimia lakini hawakuniitikia, mume wangu alionekana kukasirika sana, alikuwepo yeye, Mama mkwe na wadogo zake wote. Mezani kulikuwa na vitu ambavyo viliwekwa.


Vilikuwa vimefungwa fungwa kama hirizi, ndipo bila hata salamu mume wangu alianza kunishutumu kuwa nawawekea madawa, alininyang’anya pochi niliyokuwa nimebeba na kuanza kuikagua, aliifungua na kuangalia kila mfuko ndipo alipoona vitambaa tambaa kama hirizi sawa na vile vilivyokuwa mezani.


Alianza kunipiga kuniuliza ni nini lakini mimi sikujua kwani sikuwa mimi nimeviweka, alinipiga kweli huku akisaidiwa na Mama yake na wadogo zake, walinipiga kama mbwa wakinitukana matusi ya nguo. Mwanangu ambaye wakati huo alikuwa na miaka mitano alianza kulia na kuwaambia waniache lakini hawakusikia.


Aliruka na kunidondokea hivyo tukawa chini pamoja, lakini hawakujali waliendelea kunipiga mpaka nikapoteza fahamu. Hawakutaka hata kuninyanyua waliniacha pale pale chini, nilizinduka kama masaa mawili baadaye, mwanangu kalala pembeni yangu kapitiwa na usingizi.


Nilijaribu kujinyanyua lakini nilishindwa, mwili wote ulikuwa unauma nilijikuta nalala pale pale mpaka asubuhi. Asubuhi nilijitahidi na kuamka, niliingia chumbani nikiwa nimepanga kuondoka, sikutaka kwenda nyumbani kwani nilijua wataniambia nivumilie.


Nilishachoka kuvumilia kwani nilijua siku moja watakuja kuniua, nilidhamiria kuondoka, niliingia chumbani na kuanza kukusanya nguo zangu, mume wangu bado alikuwa amelala, sikua nikiogopa, nilikuwa tayari kuacha kila kitu na kuondoka.


Wakati nakusanya vitu vyangu mume wangu aliamka, aliniangalia kana kwamba hakujatokea kitu kisha akaniuliza. “Unafanya nini?”


Nilimuangalia na bila uoga nilimuambia “Nakusanya nguo zangu, nimechoka haya mateso, hapa tulipofikia ipo siku mtakuja kuniua bure, naondoka zangu, sijui nitaenda wapi lakini bora kufa porini kuliko kufia hapa…” Nilimjibu kwa kujiamini.


“Afadhali uondoke, chukua kila takataka uliyokuja nayo, kasoro mwanangu, hukuja na mtoto utaondoka hivyo hivyo ulivyokuja! Na ukijifungua huyo mwingine nakuja kumchukua! Ulijue hilo kabisa! Ingekuwa inawezekana ningekupasua tumbo sasa hivi nimchukue! Siwezi kuishi na mchawi nyumba moja!” 


Aliongea kwa dharau na sauti ya kumaanisha, alimshika mtoto mkono aliyekuwa amekaa kitandani akilia na kuanza kumvuruta kumtoa nje.


Mwanangu alianza kulia akiita huku akipiga kelele Mamaaa! Mamaaa! alijaribu kujitoa mikononi mwa Baba yake lakini alizidiwa nguvu, alimburuza kama mnyama mpaka nje, huku akimuambia 


“Tulia! Mama yako hakujali, anaondoka wewe utabaki hapa na mimi Baba yako!” alitoka haraka haraka huku akifunga mlango kwa nguvu, nilijikuta nanyong’onyea, nguvu ziliniishia nilishindwa hata kunyanyua nguo kupanga tena nilijikuta nakaa chini…


NDOA YA MAUTI; SITAMANI KUFA LAKINI SITAKI KUISHI —SEHEMU YA TATU


(ILIPOISHIA; Mume wangu aliniambia kama naondoka niondoke na kumuachia watoto, alimuambia mwanangu aliyekuwa akilia kuwa simjali hivyo atulie kwani naondoka namuacha…


ENDELEA….. 


Kusema kweli sikuwa na cha kufanya, kwa namna yoyote ile nisingeweza kuondoka na kumuacha mwanangu pale, nilijua lazima atateseka sana na nilikuwa tayari kufa kwaajili yake.


Taratibu nilianza kuzirudisha nguo kabatini, ilikuwa asubuhi hivyo nilipaswa kwenda kutayarisha chai, nilijaribu kunyanyuka kutoka pale kitandani lakini nilishindwa, maumivu ya kipigo cha jana yake niliyasikia mpaka mfupa wa mwisho.


Kila sehemu ya mwili wangu ilikuwa inauma hasa tumboni. Ghafla ndipo nilipokumbuka kuwa nilikuwa mjamzito, kusema kweli nilisahau kwa muda nikiwaza mambo mengine. Kwakile kipigo nilihisi kitu kibaya kilikuwa kimetokea, nilikuwa na wasiwasi sana na nilitaka kwenda hospitali ili kuangaliwa.


Nilichukua pochi yangu nikajilazimisha kunyanyuka na kutoka kutaka kwenda hospitalini lakini nilimkuta mume wangu kakaa sebuleni kwenye meza ya chakula.


“Nasubiri chai au unataka niingie jikoni nikajipikie?” Aliuliza kwa dharau, mwanangu alikuwa amekaa pembeni yake analia. 


“Huyu naye anatakiwa kwenda shule, unataka nikamuandae mimi?” Nilimuangalia mume wangu na kutamani kufungua mdomo lakini niliogopa kipigo, nilikuwa kwenye maumivu makali na sikutaka kumtukana tena akanipiga.


Nikiwa nawaza nini cha kufanya alitokea Mama mkwe na beseni lenye vitafunwa na chai, kwa mara ya kwanza nilimuona akipika kitu mule ndani.


“Nimekuandalia chai mwanangu, huyu mchawi asije kukuua bure..” Aliongea huku akiniangalia kwa dharau, nilimshukuru Mungu kafanya vile kwani sikuwa na nguvu hata ya kunyanyua kikombe.


“Mjukuu wangu twende nikakuandae” Aliongea akimshika mwanangu mkono. Mwanangu alikataa lakini Baba yake alimuangalia kwa hasira na kwa uoga alienda. 


Ingawa sikutaka amguse mwanangu lakini nilishukuru kimoyomoyo kwa kunisaidia.


“Naenda hospitali..” Nilimuaga mume wangu.


“Unaenda kufanya nini? Kuna kliniki leo?” Aliniuliza kwa dharau huku akinywa chai taratibu.


“Hapana naenda kucheki tu afya yangu..” Nilijibu kwa uoga kwani aliacha kunywa chai na kunyanyuka.


“Hakuna cha afya wala nini, najua unachotaka kufanya, unataka ukaongee huko kuwa umepigwa? Sasa hutoki humu ndani wiki nzima!” Aliongea kwa hasira, nilijaribu kujitetea lakini alitishia kunipiga na kuniambia nirejee chumbani.


Kwa uoga nilijikuta naingia chumbani bila kupenda, nilibakia na maumivu nikiwa sijui hatma ya mwanangu tumboni. Mume wangu hakuishia kuniambia tu nikae ndani lakini pia alikuja na kufungia mlango kwa nje, alinifungulia jioni alipotoka kazini na ndiyo wakati nilipopewa chakula mchana wote nilishinda na njaa na maumivu yangu.


*****


Naamini ni miujiza ambayo ilitokea, mimba niliyokuwa nayo haikuharibika na niliendelea na maisha yale mpaka nilipojifungua. Safari hii namshukuru Mungu sikujifungua kwa kisu lakini kama ilivyokuwa mwanzoni baada tu ya kujifungua nililazimika kufanya kila kitu mimi mwenyewe.


Nilifanikiwa kwenda nyumbani na kumueleza Mama matatizo ya ndoa yangu, jibu lake lilikuwa lile lile “Vumilia mwanangu ndiyo maisha ya ndoa yalivyo…” Kusema kweli ilizidi kunikatisha tamaa.


“Hata mimi na Baba yako tumefika hapa kwa kuvumiliana, haikuwa mteremko…” Niliishia tu kumuangalia mama bila kupata kitu cha kumjibu.


Nilijikita tu katika biashara na huko ndipo ilipokuwa faraja yangu, kuongea na wateja kutabasamu ilinisiadia sana. Tulifanikiwa kujenga nyumba nyingine mbili kwa biashara ile, mume wangu alijifanya kuisimamia lakini kila akikaa dukani wiki mbili basi huniita na kunirudisha kwani anaishia tu kupata hasara.


Mwanzoni alipoona biashara inaingiza pesa nyingi aliamua kuacha kazi ili kuisimamia mwenyewe lakini alishindwa hivyo ingawa hakurudi kazini lakini aliniachia nisimamie mimi na yeye ni kuchukua pesa.


*****


Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu na nilishayazoea. Kupigwa ilikuwa kama sehemu ya maisha yangu. Ingawa tulikuwa na nyumba tatu lakini ndugu zake hawakuondoka, kila tukihama walihama na sisi, kwa kifupi walituganda, shemeji zangu wote walikuwa shule ila wifi zangu wote walishindwa na shule na walishazalishwa wakiwa hawana kazi na watoto wao pale nyumbani.


Nilishaizoea ile hali na nilianza kuona kama kawaida. Siku moja nikiwa dukani mume wangu alikuja kutaka pesa, ilikuwa ni mchana lakini nilikuwa sijauza chochote na pesa zote alizichukua jana yake, nilimuambia hakuna pesa na bila hata kusikiliza maelezo alianza tu kunipiga akisema natumia pesa zake kuhonga wanaume ndiyo maana biashara inafilisika.


Kweli biashara ilishaanza kuyumba lakini sababu kubwa ni kuwa kila mtu alikuwa ni bosi, ndugu zake wakichukua pesa wanavyojisikia, yeye akichukua anavyojisikia na hata Mama yake akichukua anavyojisikia. 


Alinipiga sana, majirani hawakuingilia kwani walishazoea ile hali, walikuwa wakiniona napigwa na kunishauri niondoke lakini kila nikifikiria wanangu nilishindwa. Mume wangu alishajua kuwa mimi ndiyo kila kitu katika ile biashara hivyo pamoja na manyanyaso yote lakini alitaka niendelee kuwepo pale.


Alishaacha kazi hivyo kama biashara ingekufa ilimaanisha kuwa wasingeweza hata kupata pesa ya kula. Hivyo kila nilipokuwa nikisema nataka kuondoka alinitishia kuwa atawaua watoto na kweli nilimuamini kwani nilipokuwa nikilalamika angeweza kuwapiga bila sababu ili tu nimuone kuwa ni mkatili anaweza kuwaua kweli hivyo niliamua tu kukaa kimya.


Wakati ananipiga kulikuwa na Mama mmoja mtu mzima anapita zake, aliona namna nilivyokuwa nikipigwa na kuja pale dukani akikimbia.


“Hivi kuna wanaume kweli hapa, mnaona mwanamke anapigwa mpo tu!” Alifoka yule Mama huku akitupa mkoba wake chini na kuja, akaingia ndani kabisa ya duka na kuanza kumsihi mume wangu aniache.


“Wewe Mama haya ni mambo ya familia hayakuhusu!” Mume wangu alimjibu huku akijaribu kumsukuma. Lakini yule Mama hakutingishika, sijui alifanyaje lakini alimkamata mume wangu mkono na baada ya kama sekunde mbili nilisikia mume wangu akipiga kelele za maumivu.


Yule Mama hakumuachia aliendelea kuuminya mkono wake, mume wangu alijaribu kugeuka kumkabili lakini Mama alimkunjakunja, hakumpiga aliendelea kumminya tu mkono, sasa akiwa ameshikilia kiganja tu kama watu wanaosalimiana, aliuminya sana, mume wangu alipiga kelele kwa nguvu kuomba msamaha lakini wapi.


Yule Mama sasa alianza kumvuta mpaka nje, watu walianza kujazana baada ya kuona Mama mtu mzima kama yule miaka kama 65 hivi akimpigisha mume wangu kelele kwa kumshika mkono tu. 


Mama wa watu hata hakuongea chochote alimminya tu na mpaka mume wnagu akaanza kujikojolea kama mtoto, kusema kweli pamoja na maumivu niliyokuwa nayo nilijikuta nacheka. Watu walikuwa wakishangilia. Hakuna aliyeingilia na yule Mama hakumuachia, mume wangu alilia kama mtoto nahisi hasa ata alijisaidia ingawa mkojo ndiyo ulionekana ukitiririka huku akilia.


“Sasa piga magoti muombe msamaha mke wako?” Yule mama aliongea huku akimuachia, kiburi chote kilimuishia na mume wangu ambaye ni mrefu na mwenye mwili uliojazia vizuri kimazoezi alipiga magoti mbele yangu na kuomba msamaha. Sikujua hata cha kusema.


“Wanawake hawapigwi pigwi hovyo! Ondoka hapa!” Aliongea yule Mama akimsukuma mume wangu, kwa aibu mume wangu alinyanyuka na kupita katikati ya kundi la watu na kuiingia kwenye gari kisha akatokomea kwa aibu. Nilibaki natetemeka tu kwa furaha, yule Mama hakuongea sana, alinifuata na kuniomba karatasi, kisha akaandika namba ya simu akasema.


“Siku akikugusa tena piga namba hiyo…”


Bila hata kujitambulisha aliondoka zake na kueendelea na safari zake. Kila mtu alikuwa akishangilia wakati Mama yule ambaye hakuonekana kabisa kama mtu wa mazoezi na mwili wake mnene wa kizeezee alifanya kitu ambacho wanaume wengi walishindwa kukifanya.


Sikutaka kusubiri nipigwe ndiyo nipige ile namba, nilijua kabisa siku ile mume wangu angeniua kwa jinsi alivyokuwa amedhalilishwa. Nilijua ile namba ni ya yule Mama kumbe ilikuwa ni ya Mama mwingine (Mungu amrehemu kwani ameshatangulia mbele za haki). Yeye alikuwa ni askari wa jeshi la polisi kitengo cha jinsia.


Nilimpigia na kumuambia mtu aliyenipa ile namba ya simu na mkasa uliotokea. Ilikuwa ni namba yake binafsi na wakati huo hakuwa ofisini lakini aliniomba tuonane, alinielekeza mpaka kwake na nilimuambia mkasa mzima wa maisha yangu.


Aliniuliza ninachotaka nikamuambia kuwa ninataka kuondoka lakini na wanangu, aliniambia ukweli kwakuwa mtoto wangu wa kwanza ana umri zaidi ya miaka saba hivyo anaweza kupewa Baba yake, nilimuambia siwezi kuondoka bila mtoto na yeye akasema kuwa atanisaidia.


Aliniambia kuwa yule Mama aliyenisaidia alikuwa ni dada yake na alikuwa mwanajeshi sasa amestaafu alikuwa na cheo kikubwa tu jeshini. Hapo ndipo nilipoelewa kwanini mume wangu hakufurukuta mbele yake.


Aliniambia niende nyumbani na kama mume wangu akinitishia tu basi vijana wake watakuwa tayari kuja kama nikiwapigia simu. Nilienda kweli na kama nilivyotarajia mume wangu alikuwa akinisubiri kwa hamu, nilipofika alianza kunipiga, nilipambana nikajitoa mikononi mwake kisha nikakimbilia chumbani na kujifungia kwa ndani kisha nikapiga ile namba niliyopewa na dakika kadhaa askari walikuja.


Sikujua lakini kumbe waliambiwa wanifuate, walimkamata mume wangu wakati ananipiga na kumuweka ndani. Alifunguliwa shitaka la kupiga na kujeruhi. Wakati kesi ikiendelea kukiwa na uwezekano mkubwa wa yeye kufungwa aliniomba msamaha, sikuwa tayari kumsamehe lakini sikuwa na namna.


Alikubali kuwaacha watoto chini yangu (kwa kuandikishana kabisa) kitu ambacho nilikuwa nikikitaka na sisi kugawana mali zote tulizochuma pamoja nusu kwa nusu. Nilitaka kukataa lakini wakili wangu alinishauri nikubali kwani hata kama angefungwa lakini akitoka ningeweza kukosa kila kitu.


Mali zote ambazo tulichuma na mume wangu alikuwa ameandika majina ya Mama yake hivyo hazikuwa zetu, kwa maana hiyo kama nigemuacha afungwe basi nisingeondoka na kitu kwani nyumba kisheria hazikuwa zetu bali za Mama yake. 


Kwakuwa pia sikutaka kuendelea kumuona nilikubali, tukagawana kila kitu sawa na tukafanya mpango kesi ikafutwa huku nikifungua kesi nyingine ya kudai talaka nikapata talaka mahakamani.


Huu ni mwaka wa tatu sasa ninaishi peke yangu na wanangu, duka ambalo mume wangu alilichukua lilishafungwa kwani hakuna kitu, mimi nilifungua duka jingine na kuhama na wateja wote. Sasa nimejenga nyumba nyingine ambayo naitumia kufuga kuku ambapo nina kuku zaidi ya elfu kumi.


Sina mawasiliano kabisa na mume wangu kwani hata kupiga simu kuwajulia hali watoto hataki, nasikia tu sasa hivi wameshauza nyumba moja ambayo tuligawana ile ambayo tulijenga pamoja na ile ambayo ilikuwa ya familia tuliyoikarabati wamepangisha na wamebaki na vyumba viwili tu yeye na dada zake kwani hana kazi na wote hawana kazi.


Nashukuru Mungu nilitoka lakini nawaelewa kuna wanawake wengi ambao bado wako kwenye ndoa za mateso. Kuna uoga mkubwa wa kutoka, kuna ile kuwaza maisha yatakuwaje na vipi kuhusu watoto na upuuzi mwingine wa kuwaza labda atabadilika labda kesho itakuwa tofauti. 


Niwashauri kitu kimoja, akikupiga nenda kamshitaki, kuna dawati la jinsia karibu katika kila kituo cha polisi, anzia hapo, katoe taarifa na anawatishia mpaka watoto akiwatumia kukunyanyasa. Ukikosa msaada nenda kituo kikubwa na ukikosa nenda maendeleo ya jamii na hata kwa mkuu wa wilaya fika.


Itakusaidia sana kama huko mbeleni akitaka kuwang’ang’ania, hata mkifika mahakamani wataamua watoto kukaa sehemu ambayo watakuwa salama zaidi. Usikae tu ndani na kuishia kulalamika kwa ndugu, wataishia kukuambia tu uvumilie mpaka pale atakapokuua. Kuna wanawake wengi huvumilia makubwa zaidi ya haya na huogopa kutoka.


Usivumilie na acha kuwasikiliza ndugu ambao kazi ni kukuambia vumilia na kukuogopesha kuwa maisha hayaendi bila mwanaume. Vumilia kila kitu lakini si kipigo na manyanyaso. Nimevumilia mengi na natamani ningekutana na yule Mama mwanzo kabisa wa ndoa yangu ningeweza kutoka mapema. Ahsanteni kwa kusoma kisa changu na Mungu awabariki natumaini mmejifunza.


***TIPS*** 


Wanawake wengi wanalazimika kuvumilia ndoa za mateso kwaajili ya watoto, wanaona kama wakiondoka basi watoto wao watateseka kwa mwanaume ambaye alikuwa mnyama kwao au kupata Mama wa kambo na kuwatesa.


Kitu ambacho hawajui ni kuwa wanaweza kuwatumia watoto haohao kuleta upendo ndani ya nyumba zao na kuwabadilisha hao wanaume. 


*MWISHO*

0 comments:

Post a Comment

BLOG